
Moshi. Unaweza kusema jinamizi la kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) linaendelea kulitesa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), baada ya deni halisi na riba kufika Sh238.71 bilioni hadi kufikia Juni 30, 2024.
Kubainika huko kunatokana na ripoti kuu ya mwaka ya ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2023/2024 uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyoiwasilisha bungeni jana Jumatano, Aprili 16,2025.
CAG katika taarifa yake hiyo ameeleza katika mapitio yake ya taarifa za madeni ya Tanesco kwa mwaka wa fedha 2023/24 alibaini uwepo wa deni lililotokana na ucheleweshaji wa malipo kwa muda mrefu kwa kampuni ya IPTL.
Kwa mujibu wa CAG, sehemu ya deni hilo inahusisha kiasi cha Sh111.48 bilioni ambacho kimeafikiwa na kukubalika na pande zote mbili.
“Kufuatia ucheleweshwaji wa malipo ya deni hilo kwa muda mrefu, kiasi cha riba katika deni hilo kimeongezeka kwa kiwango kikubwa hadi kufikia Sh127.22 bilioni, ikiwa ni asilimia 114 ya deni halisi,” ameeleza CAG katika ripoti hiyo.
“Hivyo hadi Juni 30, 2024 jumla ya deni halisi pamoja na riba limefikia Sh238.71 bilioni. Ucheleweshwaji huu unasababishwa na changamoto za kibajeti ambazo zimekuwa zikijirudia kwa muda mrefu, na hivyo kuongeza gharama kwa Serikali,” amesema.
Mgogoro unavyoendelea kufukuta
CAG pia alibaini uwepo wa mgogoro unaoendelea kati ya Tanesco na IPTL, unaotokana na uamuzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) wa kutohuisha leseni ya uzalishaji umeme kwa IPTL kuanzia mwaka 2017 hadi 2022.
“Hali hii ilisababisha Kampuni ya IPTL kuwasilisha madai ya gharama za uzalishaji, fidia ya kusitisha mkataba, na ada za huduma za kisheria, huku ikiendelea kukumbushia juu ya riba katika madai hayo,”amesema CAG katika taarifa hiyo.
“Tanesco linadai mgogoro huo ulitatuliwa katika kesi ya madai ya mwaka 2015. Hata hivyo, kutokana na kutokuwepo kwa makubaliano ya pande mbili katika mgogoro huo, kunazidisha kwa kiwango kikubwa hatari za kifedha, sintofahamu na kuyumbisha sekta ya nishati nchini Tanzania,” amesema.
IPTL haijarejesha malipo kwa Serikali
Katika ripoti hiyo, CAG amebainisha kuwa kampuni ya IPTL haijatekeleza wajibu wake wa kurejesha malipo kwa Serikali ya Tanzania kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Makubaliano wa Machi 2021, licha ya kipindi cha urejeshaji wake wa miezi 12 ambacho kilikuwa kinaisha Februari 28, 2022 kupita.
Kwa mujibu wa CAG, malipo hayo ya Dola za Marekani milioni 148.4 ambazo ni sawa na Sh389.83 bilioni za Tanzania, yalitokana na matumizi mabaya ya fedha zilizohusiana na akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania.
Awali akaunti hiyo ilianzishwa ili kuwezesha malipo ya gharama za umeme.
CAG amesema katika ripoti yake kuwa hali hii inaendelea kuongeza madeni kwa Serikali kwa kiwango kikubwa, jambo linaloweza kuathiri hali ya uchumi na kupunguza imani ya umma katika mifumo ya usimamizi wa rasilimali za umma.
“Ninapendekeza kuwa Serikali ifanye tathmini kamili ya madai yote na madeni yanayohusiana na Kampuni ya IPTL ili kubaini uhalali wake, usahihi wake, na utekelezaji wa makubaliano ya kisheria,”ameeleza CAG katika taarifa yake.
CAG amesema Serikali inapaswa kutekeleza wajibu wa urejeshaji wa fedha inazoidai IPTL Dola za Marekani milioni 148.4 kwa kuzingatia Mkataba wa Makubaliano wa mwaka 2021 kwa kuchukua hatua za kisheria na kifedha, ili kuhakikisha urejeshaji wa haraka wa kiasi kilichobaki pamoja na riba.