Kinshasa. Boti iliyokuwa na abiria zaidi ya 450 imezama baada ya kuwaka moto katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuua watu 50, huku mamia wengine wakiwa hawajulikani walipo.
Associated Press imeripoti leo Alhamisi kuwa, operesheni ya uokoaji inaendelea leo Alhamisi kwa msaada wa timu za Msalaba Mwekundu na mamlaka za mkoa, kufuatia ajali hiyo iliyotokea Jumanne usiku katika Mto Congo.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Usimamizi wa Mto Congo, Competent Loyoko, boti hiyo iliyoundwa kwa mbao imeelezwa ilikuwa na abiria wapatao 450, iliwaka moto karibu na mji wa Mbandaka, baada ya kuondoka bandari ya Matankumu kuelekea eneo la Bolomba.
Loyoko amesema boti hiyo iliwaka moto baada ya abiria mmoja aliyekuwa na jiko la mkaa kuwasha moto kwa lengo la kupika chakula.
Abiria kadhaa hususan wanawake na watoto inadaiwa wamefariki dunia baada ya kuruka majini huku wakiwa hawana uwezo wa kuogelea.
Takriban watu 100 walionusurika walihamishiwa katika maeneo ya dharura kwenye jengo lililopo mji wa Mbandaka.
Mwandishi wa Al Jazeera nchini DRC, Alain Uaykani amesema ajali za boti katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.

Amesema kuwa vikosi vya uokoaji vimekuwa vikikabiliwa na ukosefu wa vifaa vya kushughulikia majanga ya dharura.
Mamia ya watu wamekufa katika ajali za boti katika miaka ya hivi karibuni, huku watu wengi wakiacha kutumia barabara zilizopo na kugeukia usafiri wa boti kwa ajili ya usalama wao.
Desemba 2024, watu takriban 38 walifariki baada ya kivuko kilichobeba zaidi ya watu 400 waliokuwa wakisafiri kwenda kusherehekea Krismasi kuzama kwenye mto.
Mwezi Oktoba, boti nyingine ilizama katika Ziwa Kivu Mashariki mwa DRC na kuua watu 78 huku wengine wakinusurika.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.