
Dodoma. Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu amewataka madaktari na wauguzi kuwa na utu katika kuwahudumia wagonjwa hasa kwenye suala la gharama.
Zungu ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi April 17, 2025 wakati Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange alipokuwa anajibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest ambaye amehoji lini Serikali itapeleka watumishi wa afya katika wilaya zilizoko pembezoni ikiwemo Kyelwa.
“Mheshimiwa Naibu Waziri, waambie madaktari na watumishi wawe na utu, mfano mtu amelazwa hasa wa magonjwa ya dialysis ambapo mgonjwa analipia kila siku gharama lakini siku moja akishindwa kulipia wanampita bila kumpa huduma, hii ni hatari sana,” amesema Zungu.
Naibu Waziri amesema mambo hayo yanafanyika wakati mishahara, umeme, vifaa na wananchi wenyewe ni mali ya Serikali lakini utu unakosekana ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mariam Kisangi ameuliza Serikali ina mpango gani wa kupeleka watumishi katika Kituo cha Afya Kilakala Manispaa ya Temeke.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri, Dk Festo Dugange amesema Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada ya afya na kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/24 jumla ya watumishi 9,384 waliajiriwa na kupangiwa kazi katika vituo vya kutolea huduma katika Halmashauri, ambapo watumishi wa afya 69 walipangwa katika Manispaa ya Temeke na watumishi watatu (3) katika Kituo cha Afya Kilakala.
“Sambamba na ajira kutoka Serikali kuu, Manispaa ya Temeke imeajiri kwa mkataba watumishi watatu (3) na kuwapangia majukumu katika Kituo cha Afya Kilakala, ambacho kina jumla ya watumishi 19 kati ya 35 wanaohitajika,” amesema Dk Dugange.
Amesema Serikali itaendelea kutoa vibali vya ajira kwa Kada za Afya na kuwapanga katika Halmashauri zenye upungufu kote nchini ikiwemo mikoa ya pembezoni na kuwajengea nyumba za kuishi.