CAG aimulika TIC ucheleweshaji vyeti vya motisha hadi siku 400

Moshi.  Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amekimulika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kuchelewesha uchakataji na uidhinishaji wa vyeti vya motisha kwa wawekezaji hadi siku 400 kwa baadhi yao.

Muda huo ni kinyume na Sheria cha kifungu cha 18 (4) cha Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania ya mwaka 2022 ambayo imeweka muda wa kikomo ni siku 7 za kazi na haya yanatokea wakati Serikali ipo katika harakati za kuvutia wawekezaji.

Hata hivyo, CAG katika Ripoti Kuu ya mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 iliyowasilishwa bungeni Jijini Dodoma jana Jumatano Aprili 16, 2023, amebaini ucheleweshaji huo wa uchakataji na uidhinishaji vyeti hivyo.

CAG ametolea mfano maombi 178 sawa na asilimia 25 ya vyeti vya motisha 705, yaliidhinishwa kwa kuchelewa kati ya siku saba hadi siku 417, kinyume kabisa na takwa la sheria ya uwekezaji Tanzania ya mwaka 2022.

“Vilevile, nilibaini ucheleweshaji wa hadi siku 336 katika uchapishaji wa vyeti vya motisha, jambo ambalo ni kinyume na Kifungu cha 18 (4) cha Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania ya mwaka 2022,” alibainisha CAG katika ripoti yake na kuongeza:-

“Hali hii ilichangiwa na kutokuwepo kwa mifumo ya udhibiti na ufuatiliaji pamoja na vigezo vya utendaji vya kufuatilia maendeleo ya idhini ya maombi tangu tarehe ya kuwasilishwa,” ameeleza CAG katika ripoti yake inayopatikana mtandaoni.

“Ucheleweshaji kama huu unaweza kuzuia uwezo wa waombaji kutumia fursa zilizopo, hivyo kuathiri matokeo ya maendeleo ya kiuchumi au ya kibiashara,” amesema.

Kutokana na changamoto hiyo, CAG amependeza TIC kiwe na utaratibu wa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa maombi ya wawekezaji kwa kuandaa ripoti itakayoelezea sababu za ucheleweshaji wa idhini kwa kila ombi na hii itasaidia uboreshaji wa mchakato wa maombi na dosari kutatuliwa kwa wakati.

TIC hakina Programu ya Uhamasishaji

Wakati wa ukaguzi huo, CAG amebaini TIC hakina programu ya kukuza uwekezaji ili kusaidia kutambua fursa za kimkakati na wawekezaji watarajiwa.

Pia CAG alibaini kuwa hitaji la program la kukuza uwekezaji halijawasilishwa kwenye Bodi ya wakurugenzi, kwani haijawahi kujadiliwa kama ajenda hadi Juni 30, 2024 wakati CAG akikamilisha ukaguzi wake kwa mwaka 2023/2024.

“Hii inakuwa ni kinyume na Kanuni ya 27(1-3) ya Kanuni za Uwekezaji Tanzania za mwaka 2023, ambayo inakitaka Kituo cha Uwekezaji Tanzania kuandaa na kuwasilisha programu ya kukuza uwekezaji kwenye Bodi ili kuidhinishwa.”

“Kwa maoni yangu, hii inaweza kusababisha kukosa fursa za kimkakati na kukatisha tamaa wawekezaji,” alisisitiza CAG katika taarifa yake hiyo iliyowasilisha Bungeni jijini Dodoma leo Aprili 16, 2025 na kuweka katika tovuti za CAG.

CAG amependekeza Kituo cha uwekezaji Tanzania kihakikishe kuwa programu ya kukuza uwekezaji inatayarishwa na kuwasilishwa kwa Bodi ya Wakurugenzi kwa ajili ya kuidhinishwa na baadaye kutekelezwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *