Mwanamitindo nchini ambaye pia ni shabiki wa Real Madrid, Hamisa Mobetto ameonyesha kuhuzunishwa na matokeo iliyoyapata timu yake dhidi ya Arsenal kwenye mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Arsenal uliochezwa kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu.
Madrid ilipoteza mchezo kwa kipigo cha 2-1, shukrani kwa mabao ya Bukayo Saka na Gabriel Martinelli kwa upande wa Arsenal na lile la kufutia machozi la Real Madrid lililofungwa na Vinicius Junior na mabingwa hao kuvuliwa taji kwa kichapo cha jumla ya mabao 5-1, baada ya pia kufungwa 3-0 katika mechi yao ya mkondo wa kwanza ya robo fainali kwenye Uwanja wa Emirates wiki moja iliyopita.
Kwa ushindi huo, Arsenal imekufuzu nusu fainali na itacheza na PSG ambayo, Gunners iliifunga 2-0 katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.

Kupitia mtandao rasmi wa Madrid baada ya posti ya matokeo hayo, mwanamitindo Hamisa alishindwa kuficha hisia zake na kwenda kuacha ujumbe wa kutoridhishwa na kilichotokea na kumtaka kocha wa timu hiyo Carlo Ancelotti amsajili kiungo wa Yanga, Stephane Aziz Ki, ambaye pia ni mume wa mwanamitindo huyo.
Hamisa aliandika: “Dah nyie hiki ni nini (what is thiiiiisssssss’, Ancelotti msaini mume wangu)” huku akimtag Aziz Ki.
Katika Ligi Kuu Bara anayoichezea Aziz Ki nyota huyo amefunga mabao saba na asisti saba, wakati pia msimu uliopita alikuwa Mchezaji Bora wa Msimu na pia Mfungaji Bora wa Msimu akiweka kambani mabao 21 na kutoa asisti nane za mabao katika Ligi Kuu.
Hii sio mara ya kwanza kwa Arsenal kuitoa Madrid kwenye mashindano haya kwani ilishafanya hivyo mwaka 2006, mchezo wa kwanza Madrid ikipoteza nyumbani kwa bao 1-0 mchezo wa pili ikipata sare ikiwa uwanja wa ugenini na kufanya jumla ya matokeo kuwa 0-1.
Arsenal pia ilifanya hivyo mwaka 2008 ambapo ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Madrid na kuipiga bao 1-0.
Baadhi ya mastaa pamoja na kocha wa timu hiyo wametoa kauli mbalimbali wakionyesha kuumizwa na matokeo hayo huku wakiahidi kupambana.
Kocha Ancelotti alisema “Tunapaswa kunyanyua vichwa vyetu juu, lazima tujifunze na kupambana katika michezo ijayo.”
Lucas Vazquez, naye aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram: “Wana Madrid mnajua kila wakati tunajitoa kila kitu kwaajili ya klabu, leo haikuwa bahati.”
Golikipa naye Thibaut Courtois aliandika: “Tunapenda kuwashukuru mashabiki kwa sapoti yao.”
Kwenye michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Madrid inashikilia rekodi ya kuwa kwabu iliyobeba kombe hilo mara 15 huku Arsenal ikiwa haijawahi kulitwaa.