
Dar es Salaam. Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoka Zanzibar, wamekiburuza mahakamani chama hicho pamoja na mambo mengine wakilalamikia upendeleo katika mgawanyo wa rasilimali za chama pamoja na stahiki nyinginezo.
Kesi hiyo ya madai namba ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, ambaye anajitambulisha kama mwanachama na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao wanajitambulisha kuwa ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.
Wamefungua kesi hiyo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema, ikiwa mdaiwa wa kwanza na Katibu Mkuu wa Chadema ni mdaiwa wa pili.
Katika kesi hiyo, wanaiomba Mahakama hiyo itamke kuwa wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusiana na vyama vya siasa na Katiba ya chama hicho.
Wamechukua hatua hiyo na kuomba Mahakama iamuru na kutamka hivyo wakidai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.
Pia, wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa msingi huo, walalamikaji hao wanaomba Mahakama hiyo itoe hukumu na amri dhidi ya wadaiwa kwamba wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Vilevile wanaiomba Mahakama itamke na kuwaelekeza wadaiwa kuzingatia kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Amri nyingine wanazoomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama.
Na wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.
Mbali na amri hizo, wanaiomba Mahakama iamuru, wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo Mahakama itaona inafaa kuzitoa.
Kesi hiyo iliyopangwa kusikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga, itaanza leo Alhamisi, Aprili 17, 2025.
Tayari Mahakama imeshatoa wito kwa Chadema kupitia Katibu Mkuu kufika mahakamani wakati kesi hiyo itakapotajwa.
Kwa mujibu wa hati ya wito ambayo Mwananchi imeiona, licha ya kukitaarifu chama hicho kuwa kesi hiyo imepangwa kutajwa leo, pia mahakama hiyo imekitaka kuwasilisha maelezo ya utetezi wake kwa maandishi.
“Pia tambua zaidi kuwa ikiwa utashindwa kuwasilisha maelezo yako ya utetezi wa maandishi kwa muda ulioainishwa, Mahakama itaendelea kesi na kutoa hukumu dhidi yako”, inasomeka hati hiyo ya wito iliyosainiwa na kugongwa muhuri wa Naibu Msajili Mwandamizi.