Wakulima wawalalamikia wafugaji, RC Homera atoa maagizo kwa Polisi

Mbeya. Wakulima wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wameiomba Serikali kuingilia kati mgogoro unaoendelea kati yao na wafugaji, wakidai kupigwa viboko kisa wanalalamikia mifugo inalishwa kwenye mashamba yao ya karanga na mahindi.

Ombi hilo wamelitoa leo Jumatano Aprili 16, 2025  kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi wilayani humo.

Mkulima aliyejitambulisha kwa jina la Tunu Mgawa, amesema kwa muda mrefu sasa wananyanyaswa na baadhi ya wafugaji na hawapati msaada wowote kutoka kwa viongozi wa maeneo yao.

“Leo ni bora umekuja ngoja tukuambie ili wewe ambaye uko huko kwenye Serikali Kuu utusaidie,” amesema Mgawa.

Amesena wamechoshwa na vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea licha ya kulalamika mara kadhaa kwa viongozi bila mafanikio.

“Mkuu wa Mkoa tunapata mateso. Kitu cha kusikitisha mifugo inaingizwa mashambani hata kama tupo eneo hilo, tukijaribu kuuliza tunapigwa viboko,” amelalamika Mgawa.
Amedai kuna mfugaji mmoja (jina linahifadhiwa)) aliingiza mifugo yake kwenye mashamba yake matatu yenye ukubwa wa zaidi ya hekari mbili, yaliyopandwa karanga na mahindi.
“Sio kwamba simjui aliyefanya hivi, namfahamu. Tatizo ni kwamba hata nikimripoti kwa viongozi sipati msaada wowote,” amelalamika mama huyo.

Mkulima mwingine, Exsaud Mwakyoma amesema:

“Tunategemea kilimo cha karanga na mahindi ili kugharamia elimu ya watoto wetu na maisha kwa ujumla. Tunaomba msaada wako Mkuu wa Mkoa, kwa kuwa wewe si mwanasiasa bali kiongozi wa serikali.”

Akijibu malalamiko hayo, Homera ameliagiza Jeshi la Polisi Wilaya ya Mbarali kuwatafuta na kuwachukulia hatua wafugaji wote waliolalamikiwa kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima.

“Hatuwezi kuwavumilia watu wanaolisha mifugo kwenye mashamba ya wananchi. OCD nataka watu hao wasakwe na kuchukuliwa hatua mara moja,” amesisitiza Homera.

Aidha, ametoa maagizo kwa wafugaji walioingiza mifugo mashambani kulipa fidia ya chakula cha mwaka mmoja kwa wakulima walioathirika.

“Hii haiwezekani, tunafahamu hali halisi ya maisha vijijini. Mwananchi anapolima ekari moja ya mazao, hiyo ndiyo tegemeo lake la kuendesha maisha ya familia yake,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *