Warioba ajitosa kusaka suluhu INEC, Chadema

Dar es Salaam. Jawabu la swali kuhusu mwafaka kati ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi, limeanza kutafutwa baada ya Jaji Joseph Warioba na wazee wenzake, kujitolea kutafuta suluhu.

Hatua hiyo imekuja baada ya Chadema kutohudhuria kikao wala kusaini kanuni hizo ilipoalikwa pamoja na vyama vingine 18, Aprili 12, 2025, huku INEC ikieleza kuwa hatua hiyo imekikosesha chama hicho haki ya kushiriki uchaguzi kwa miaka mitano.

Jaji Warioba na wale aliowaita “wazee wenzake”, bila kuwataja majina, wameingia kazini kujaribu kuishauri INEC na Chadema waafikiane, na hatimaye chama hicho kipewe nafasi, kiridhie kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi ili kuleta uchaguzi wa amani.

Sababu zinazotajwa na Chadema kususia kikao hicho ni msimamo wake wa hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi, huku tume ikieleza kuwa kutosaini kanuni hizo ni kukiuka Kifungu cha 162 (2 na 3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.

Katikati ya hayo, mjadala ukahamia kwa wadau wa sheria, wanaosema ingawa Chadema haikusaini kanuni hizo kwa siku iliyopangwa na INEC, sheria na kanuni hazijawazuia kusaini siku nyingine.

Jaji Warioba na wenzake wanasaka mwafaka wa Chadema na INEC bila kumtafuta mkosaji, ilimradi vyama vyote vishiriki uchaguzi mkuu mwaka huu na ufanyike kwa amani.

Jaji Warioba amesema hayo leo, Aprili 16, 2025 katika mahojiano maalumu na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Katika mazingira ya chama cha siasa kuzuiwa kushiriki uchaguzi kwa miaka mitano, kwa mtazamo wa Jaji Warioba aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kulikuwa na dalili za uwezekano wa kutokea vurugu na kuvunja amani.

Amesema fikra hizo zilimshawishi kushauriana na aliowaita wazee wenzake (bila kuwataja majina) kuona wanaloweza kushauri kwa ustawi wa amani katika uchaguzi wa mwaka huu.

“Baada ya kushauriana, tukachukua hatua ya kwanza, kuwasiliana na Chadema ili kujua kwa nini wamekataa kusaini kanuni za maadili,” amesema mkongwe huyo aliyebobea katika utumishi wa umma.

Amesema Chadema walimweleza hoja zao, ikiwemo kuwahi kuandika barua kwa INEC Desemba, 2024 kuhusu mambo ya kisheria yanayopaswa kushughulikiwa, na haikujibiwa.

Jaji Warioba amesema Chadema walimwambia hata uamuzi wa tume wa kuwaondoa kwenye uchaguzi baada ya kutosaini kanuni za maadili, ulipangwa kwa kuwa miaka ya nyuma vyama havikulazimishwa kusaini siku moja.

“Baada ya kuzungumza nao, tulishauri ngoja tuone namna itakavyokuwa kwa sababu tulieleza hatari tunayoiona, nao wajue kwamba uchaguzi ni wananchi, kikatiba wana haki ya uchaguzi,” amesema.

Jaji Warioba, ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais mstaafu wa Tanzania, amesema ameuona uamuzi wa Chadema kutoshiriki uchaguzi kwa miaka mitano, unalikosesha haki kundi kubwa, si tu la wanachama wao milioni nne, bali hata mashabiki.

“Ukisema kwa miaka mitano hawa hawatashiriki, ni kundi kubwa; wamo wanaotaka kugombea, wamo wanaotaka kuchagua. Tukawaambia bado mfikirie, siyo mwisho, ngoja tuone,” amesema.

Pia amesema Chadema walimweleza kuwa hata kanuni za maadili hazijaweka ukomo wa muda kwa vyama vya siasa kusaini.

Amesema hilo lilimsababisha azitafute kanuni na kuzisoma; amekuta kipengele kinachozuia chama kushiriki uchaguzi iwapo hakikusaini, lakini hakikuwekwa ukomo wa siku ya kutia saini.

“Uamuzi mkubwa kama huu unaohusu watu unauweka kwenye kanuni? Hapa hakuna kingine kilichoongezwa kwenye Katiba,” amesema Jaji Warioba akionesha mshangao.

Hata hivyo, Mwananchi ilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, azungumzie alichokisema Jaji Warioba kama ni sahihi, lakini amesema atalizungumzia hilo utakapofika wakati wa kuzungumza, kwa sasa hana cha kusema.

“Kwa sasa sipo tayari kuzungumzia hilo, utakapofika wakati tutazungumzia,” amesema Heche.

Muda uliopo unatosha?

Akijibu swali aliloulizwa iwapo muda uliobaki unatosha kufanyika kwa mabadiliko ya sheria, Jaji Warioba alianza kujibu kwa kurejea miaka ya nyuma, akisema uamuzi wa Tanzania kufuta sheria za kikoloni zilizokuwa zinaweka vikwazo kwa wananchi kupiga kura, ulilenga kuwarahisishia watu wapate haki yao ya msingi.

Hatua ya kuwekwa kifungu tena katika kanuni kinachoadhibu kiasi cha kumnyima mwananchi haki ya kushiriki uchaguzi, amesema inarudisha nyuma Taifa na kuondoa maana ya harakati za uhuru.

Ili kuondokana na hayo, Jaji Warioba amesema ahadi hazitoshi kwamba uchaguzi utakuwa huru na haki, bali Serikali itekeleze jukumu la kujibu na kufanyia kazi yanayolalamikiwa kuhusu sheria na kanuni za uchaguzi.

“Mambo yametendeka mwaka 2019, yakajirudia 2020, mwaka 2024 yamesemwa. Serikali inakaa kimya. Watu wanasema utaratibu wa kuengua watu tena wa upande mmoja hautendi haki, kura bandia zimeonekana, Serikali imekaa kimya haisemi chochote.

“Ninavyojua, nimefanya kazi kwenye Serikali. Kwa dosari kama hizi, Serikali yenyewe ingekuwa inachukua hatua, na safari hii, wakikubaliana, itoe ahadi kwa mapana kwamba Serikali itachukua hatua hizi, mawakala inachukua hatua hizi, kura bandia inachukua hatua hizi,” amefafanua.

Jaji Warioba amesema kuhusu madai ya Katiba kuwa ni ngumu, kwa sababu kipindi kilichobaki kabla ya uchaguzi ni kifupi, lakini mengine kuhusu kanuni za uchaguzi yanawezekana.

“Chadema watafakari waone msimamo wao, kwa kiwango gani, mabadiliko gani katika kipindi hiki tunaweza kuyafanya, mengine tungojee.

“Lakini Serikali nayo itafakari ni mambo gani yafanywe ili kuzuia dosari zilizotokea mwanzo katika uchaguzi. Mimi nafikiri inawezekana bila mabadiliko kabisa, mengi ni ya kiutendaji zaidi. Ukiwanyima watu haki yao, unajenga msingi wa vurugu,” amesema Jaji Warioba.

Amesema mabadiliko yanayohitajika hayahitaji kutengeneza sheria mpya hasa kwa dosari ndogondogo, badala yake ni uamuzi wa Serikali kutangaza na kuweka kwenye kanuni.

“Ni kusema tu kwamba haya sio mambo yatakayosababisha mgombea aenguliwe, hivyo hivyo kwenye mambo ya mawakala. Wasimamizi wa uchaguzi wako chini ya Serikali, inahitaji nini badala ya kuwaonya na kuwaeleza haya msifanye?

“Usifike wakati wa uchaguzi unafunga ofisi. Mambo mengi ya utendaji, inawezekana kuyabadili. Mimi sioni ugumu wowote,” amesema Jaji Warioba.

Amesema kanuni zinaweza kubadilishwa wakati wowote, hivyo inawezekana kubadilisha kwa muda mfupi na kutangaza, na uchaguzi ukafanyika kwa amani.

Mawasiliano na INEC

Baada ya hatua hiyo, Jaji Warioba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, amesema aliwasiliana na Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele, kumweleza umuhimu wa amani katika siasa na hatimaye nchini.

Amesema alimweleza kuwa hatua ya kukizuia chama kimoja kushiriki uchaguzi kwa kutosaini kanuni za maadili kunaleta mazingira ya vurugu.

“Tukamshauri, kwa kuwa kanuni haisemi kutia saini ni siku moja, wawe na subira kuona kama tunaweza kupata njia au kupata mwafaka,” amesema Jaji Warioba.

Hata hivyo, amesema wataendelea na mashauriano hayo, na wamekuwa wakishauriana, wakilenga kujaribu kuona kama wataweza kuwashawishi Chadema wakubali kusaini.

Pia, amesema kuwa kuishawishi tume sio kwamba haiwezi kubadili msimamo wake, na iwapo kuna mambo ya kushauriana yazungumzwe.

“Hasa kwa kuzingatia madai ya Chadema ya ‘No reforms, no election’, walisema katika mazungumzo yao kuwa kulikuwa na jitihada za viongozi wa vyama vinavyounda Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD) kukutana ili kukubaliana juu ya baadhi ya masuala muhimu, na baada ya kufikia mwafaka, walipanga kwenda kwa pamoja kumwona Rais.

“Hata hivyo, wanasema INEC ilichukua hatua hiyo kabla mchakato huo wa mashauriano haujakamilika,” amesema.

Wanachokitaka Jaji Warioba na wazee wenzake, amesema ni kuona namna ya kusaidia ili kuepusha vurugu itakayoharibu amani ya nchi.

Hata hivyo, nguli huyo wa sheria amesema kuwa yeye na wazee wenzake wamekuwa wakifanya mashauriano ya aina hiyo kimyakimya, hasa pale linapotokea jambo linalohitaji ushauri.

Amesema katika mashauriano hayo hawaangalii dhamira za vyama, bali wanatoa ushauri wa namna ya kuepusha hatua zinazoweza kuwaengua baadhi ya wananchi kushiriki michakato halali ya kikatiba.

“Miaka mitano ni mingi, na kama wamezuiwa kufanya uchaguzi kwa miaka mitano, wanaweza kufanya chochote kinachoharibu amani yetu,” amesema.

Amesema wameshatoa ushauri na watafuatilia, lakini nia yao ni ufikie wakati wa kufanyika uchaguzi wa amani.

“Tunachotafuta ni kwamba wakubaliane hao (INEC na Chadema) ili uchaguzi uwe wa amani,” ameeleza Jaji Warioba.

Mwenyekiti INEC

Mwananchi imemtafuta Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele, ambaye amekiri kuwahi kupigiwa simu na Jaji Warioba, akishauri kuhusu masuala ya Chadema kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi.

“Alipiga kushauri na akazungumzia hatari ya wao (Chadema) kutosaini, na alichoniambia ni kwamba anakubaliana nami kwamba mahitaji ya kanuni ni kwamba yule ambaye hajasaini hawezi kushiriki kwenye uchaguzi, na akasema kuna hatari ya kwamba chama kimoja hakijasaini, kwamba kisishiriki,” amesema.

Jaji Mwambegele amesema alichoambiwa na Jaji Warioba ni kwamba atawashauri Chadema ili wasaini kanuni hizo za maadili ya uchaguzi.

“Nikasema siwezi kufanya uamuzi peke yangu kwa sababu uamuzi wa INEC huwa unafanywa kwa vikao, siwezi kutoa uamuzi mimi mwenyewe kuhusu hilo,” ameeleza.

Alipoulizwa iwapo kisheria kuna nafasi kwa chama hicho kusaini, mwenyekiti huyo wa INEC amesema inategemea na tafsiri ya sheria husika.

“Ni tafsiri tu ya sheria, lakini maadili yanachosema ni kwamba mtu ambaye hajasaini hawezi kushiriki. Sasa whether kuna room au hakuna room, hiyo itatokana na tafsiri ya kisheria,” ameeleza Jaji Mwambegele.

Itaendelea kesho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *