Ada Tadea yatoa neno uboreshaji daftari la wapiga kura

Kahama. Kazi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili katika Jimbo la Kahama Mjini, mkoani Shinyanga, inatarajiwa kuanza rasmi Mei Mosi na kukamilika Mei 7, 2025.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), jumla ya wapiga kura 262,194 wanatarajiwa kuandikishwa katika vituo 39 vilivyoidhinishwa kwenye ngazi ya kata ndani ya jimbo hilo.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 16, 2025, katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Kahama, Dauda Hassani ametoa wito kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na kwa kumcha Mungu, ili kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa haki.

“Msingi wa amani ni haki. Ni jukumu letu sote kuiheshimu na kuilinda amani ya nchi. Namuomba msimamizi wa uchaguzi awe muadilifu na mwenye hofu ya Mungu ili kuhakikisha kila mmoja anatendewa haki katika zoezi hili,” amesema Hassani.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Ada-Tadea Wilaya ya Kahama, Perpetua Ruben akizungumza na Mwananchi baada ya kikao hicho, amesema chama chake kimepanga kushiriki uchaguzi na kwa sasa wanasubiri muongozo rasmi kuhusu uboreshaji wa daftari la wapiga kura.

Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kahama Dauda Hassani akizungumza kwenye kikao cha baraa la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga. Picha na Amina Mbwambo

“Sasa hivi hatuna maelekezo ya moja kwa moja kuhusu uboreshaji huo, kwa sababu tunasubiri muongozo wa chama. Lakini msimamo wetu kwa sasa ni kushiriki uchaguzi, hatutasusia,” amesema.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kahama Mjini, Elkana Shija naye amesema kazi ya  uboreshaji daftari itaenda sambamba na uhakiki wa taarifa kwa waliokwisha jiandikisha na usajili wa wapiga kura wapya.

“Wapo waliotimiza miaka 18 na wale ambao hawakujiandikisha katika awamu zilizopita wote wanapaswa kufika vituoni na kama kuna wananchi wenye pingamizi dhidi ya waliojiandikisha awali tunawaomba nao wajitokeze katika muda uliopangwa pia,” amesema Shija.

Amesema mzunguko wa tatu utafanyika kati ya Juni 28 hadi Julai 4, 2025 katika Gereza la Wilaya ya Kahama huku akihimiza ushirikiano wa viongozi wa dini, siasa na wananchi kwa ujumla katika kuhamasisha ushiriki wa wananchi kwenye kazi hiyo.

“Kuanzia Mei Mosi hadi Mei 7 tutakuwa na zoezi hili muhimu. Naomba sana viongozi wa dini, madiwani na wananchi wote washiriki kuhamasisha ushiriki wa watu wajitokeze kwa wingi,” amesema Shija.

Itakumbukwa Januari 16, 2025, wakati wa mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika mkoani Lindi, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Mstaafu Mbarouk Mbarouk, alikumbusha kuwa ni kosa la jinai kwa mtu kujiandikisha zaidi ya mara moja kwenye daftari la wapiga kura.

“Ukibainika umejiandikisha zaidi ya mara moja, unaweza kuhukumiwa kifungo cha miezi sita hadi miaka miwili. Ni muhimu kila mwananchi kuhakikisha anajiandikisha mara moja tu,” alisisitiza Jaji Mbarouk.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, Aprili 14, 2025 jijini Dodoma, alieleza kuwa zoezi hilo litafanyika katika ngazi ya kata kwa upande wa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa upande wa Zanzibar. Jumla ya vituo 7,659 vimeandaliwa Tanzania Bara na vituo 210 kwa upande wa Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *