
Moshi. Ndege nne za aina ya Airbus A220 za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), zilikaa bila kutumika kwa muda wa kati ya siku 279 hadi 721 hadi kufikia mwaka wa fedha 2023/2024 ulioishia Juni 30, 2024, kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Katika ripoti kuu ya mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, CAG ameeleza kampuni hiyo iliripoti ndege hizo zimekaa bila kutumika kwa muda mrefu kutokana na utendaji duni wa ndege hizo.
“Ndege hizi zilitengenezwa zikiwa na huduma duni za ukarabati baada ya uuzaji, kama vile upatikanaji wa vipuri vya injini na vipuri vingine.
“Kampuni ilitumia gharama zisizobadilika Sh9.16 bilioni kwa ndege hizo zilizokaa bila kutumika katika mwaka 2023/24 huku kampuni ikipata Sh5.49 bilioni kama motisha ya kukodisha kutoka kwa Wakala wa Ndege za Serikali,” amesema CAG Charles Kichere.
“Kiasi hiki kilifidia asilimia 60 pekee ya jumla ya gharama zisizobadilika zilizotumika kwa ndege za Airbus ambazo hazikuwa zimetumika kwa muda mrefu.
“Hii ilitokana na upembuzi yakinifu usiotosheleza kabla ya kununua ndege na kutozingatia masharti ya mkataba wa ununuzi wa ndege kuhusu kudai fidia za matengenezo ya injini pindi zinapoharibika katika kipindi cha waranti,” amesema.
“Matokeo yake, kampuni inaingia gharama zisizo za lazima ambazo zingeweza kufidiwa kupitia waranti,” amesisitiza CAG katika ripoti yake hiyo ambayo imewasilishwa bungeni jijini Dodoma leo Aprili 16, 2025 na kuwekwa mtandaoni.
Kutokana na changamoto hiyo, CAG amependekeza kampuni hiyo ishirikiane na Serikali kutathmini changamoto za kiufundi zinazohusiana na ndege za Airbus A220 ili kubaini kama inawezekana kuendelea kufanya kazi kwa mtindo huo.
Pia, amependekeza ifanye utafiti kuhusu aina za ndege zinazofaa zaidi kwa ajili ya kufanya kazi kwa ufanisi, kwa kuzingatia vigezo vya kiuchumi na hali ya kijiografia.
Ameshauri ishirikiane na Wakala wa Ndege za Serikali, kufanya mapitio ya kina ya mikataba ya ununuzi wa ndege na matengenezo ili kutambua na kudai fidia ya ndege kutofanya kazi wakati zikiwa kwenye matengenezo chini ya muuzaji.
Matengenezo yasiyo na tija
CAG amebaini kuwa Sh20.63 bilioni zilitumika kwa ajili ya matengenezo na bima ya ndege aina ya DASH 8 Q300 (5H-MWF) tangu ilipopelekwa Kisiwa cha Malta kwa ajili ya matengenezo Novemba 2020.
CAG amebainisha ndege hiyo ilikuwa haijatumika kwa zaidi ya miaka saba, ikiwa ni pamoja na miaka minne ya matengenezo ambayo hayakufanikiwa wakati huo licha ya gharama iliyotumika na mapato yaliyokosekana kutokana na kutotumika kwa ndege hiyo, hadi kufikia Juni 30, 2024.
“Sababu kuu zilizoainishwa ni kupitwa na wakati kwa muundo wa ndege na kusababisha changamoto katika upatikanaji wa vipuri huku ATCL ikishindwa kutathmini uwezekano wa kiuchumi wa kufanya ukarabati wa ndege kabla ya kuingia gharama hizo,”amesema CAG.
Kutokana na hali hiyo, ATCL imepata hasara kubwa ya kifedha na kupungua kwa uwezo wa kufanya kazi.
CAG amependekeza kampuni hiyo ifanye tathmini kulingana na hali ya sasa ya sekta ya ndege na mahitaji ya soko ili kuboresha utendaji kazi wa ndege ya DASH 8 Q-300(5H-MWF), kwa kuzingatia hali yake na upatikanaji wa vipuri.
Ukodishaji wa ndege
CAG katika ripoti yake hiyo amesema kifungu cha 4.1 cha Mikataba ya Ukodishaji wa Ndege kati ya Wakala wa Ndege wa Serikali na ATCL kinamtaka mkodishwaji kulipa ada ya kudumu ya kukodisha ndege ya kila mwezi.
Katika ukaguzi huo, CAG amebaini katika kipindi cha miaka sita mfululizo, tozo za ukodishaji zisizolipwa na ATCL ziliongezeka kutoka Sh27.89 bilioni, zilizoripotiwa Juni 30, 2018, hadi kufikia Sh369.13 bilioni Juni 30, 2024.
“Malipo yaliyolimbikizwa katika mwaka wa fedha 2023/24 ambazo ni Sh369.1 bilioni ni sawa na asilimia 63 ya jumla ya madeni yote ya sasa iliyoripotiwa kwenye hesabu za kampuni ambazo ni Sh595 bilioni hadi Juni 30,2024.
“Hii ilichangiwa na gharama kubwa ya uendeshaji na matengenezo ya ndege yaliyofanywa na ATCL, kupata hasara ya kifedha katika miaka sita mfululizo,”amesema CAG katika ripoti yake hiyo.
CAG amependekeza kampuni hiyo na Wakala wa Ndege wa Serikali wa Tanzania wajadiliane na kuweka mpango wa malipo wa kodi na tozo za ukodishaji ndege.
Mpango huo kwa mujibu wa CAG, ujumuishe pamoja na urekebishaji wa deni, kuongeza muda wa malipo, na kupunguza tozo za kila mwezi ili ATCL iweze kumudu kuzilipa.