DC Sanga atoa neno kwa wakulima, wafanyabiashara

Iringa. Katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi kwenye sekta ya biashara, kilimo na ufugaji zinapatiwa suluhisho, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Rebeca Sanga amewahamasisha wakazi wa Mkoa wa Iringa na maeneo ya jirani kushiriki katika maonesho ya biashara, viwanda na kilimo yatakayofanyika kwenye viwanja vya Polisi Mtua, Ilula.

Amesema kila sekta itakuwa na wataalamu walio tayari kutoa mafunzo Katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi kwenye sekta ya biashara, kilimo na ufugaji zinapatiwa suluhisho, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Rebeca Sanga amewahamasisha wakazi wa Mkoa wa Iringa na maeneo ya jirani kushiriki katika maonesho ya biashara, viwanda na kilimo yatakayofanyika kwenye viwanja vya Polisi Mtua, Ilula.kwa washiriki.

Akizungumza na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali leo Jumatano Aprili 16, 2025 katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDF) kilichopo Mtua Ilula, Sanga amesema  kuelekea maadhimisho ya wiki ya maonesho hayo yatakayofanyika kuanzia Mei 21 hadi 25, 2025, wananchi watapata fursa adhimu ya kujifunza, kushirikiana na kutangaza shughuli zao.

Amesema maonesho hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu: “Kilolo Mpya, Fursa Mpya za Uwekezaji na Kilimo cha Kibiashara Kuchochea Maendeleo.”

“Niwahimize wananchi kuwa haya si maonesho ya kawaida. Hii ni fursa ya pekee ya kujifunza teknolojia mpya, kutangaza bidhaa zenu, pia kupata masoko mapya. Tuichukulie hii kama darasa la maendeleo kwa kila mmoja wetu,” amesema DC Sanga.

Aidha, aliongeza kuwa maonesho hayo yatawapa wananchi wa Kilolo nafasi ya kuonyesha bidhaa na mazao yanayozalishwa wilayani humo, hivyo akatoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu.

Katika mazungumzo hayo, DC Sanga pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kukuza uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla.

Katibu wa TCCIA Wilaya ya Kilolo, Painetho Madembwe, amesema maonesho hayo yatakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Kilolo kwa kuwa yatawapa fursa ya kupata maarifa mapya yatakayoboresha biashara zao.

“Nina imani kuwa kila kundi litalitumia ipasavyo jukwaa hili, kila mmoja atajifunza kutoka kwa mwingine na hii ndiyo njia ya kukuza biashara,” amesema Madembwe.

Amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara na wakulima kutumia maonesho hayo kuimarisha mitandao ya kibiashara pamoja na kujifunza mbinu bora za uzalishaji na uendeshaji wa biashara.

Mwananchi Digital imezungumza na baadhi ya wafanyabiashara kutoka wilayani Kilolo waliothibitisha kuwa maonesho hayo yatawasaidia kukuza biashara zao pamoja na kuongeza ujuzi wa usimamizi wa shughuli zao za kiuchumi.

Tarick Mpepwa, mfanyabiashara wa mbao kutoka Ilula Mtua, amesema biashara kwa sasa inakumbwa na changamoto nyingi ikiwamo ya ukosefu wa maarifa sahihi ya soko.

“Kwa kweli, wafanyabiashara wengi tunafanya biashara bila kuelewa masoko sahihi ya bidhaa tunazouza. Kupitia maonesho haya, naamini tutapata msaada kutoka kwa serikali na wataalamu,” amesema Mpepwa.

Ameongeza kuwa maonesho hayo yatakuwa ni daraja muhimu la kutoa elimu kwa wafanyabiashara na kuwasaidia kupanua wigo wa biashara zao.

Naye Leah Mbinda, mama lishe kutoka Mtua Ilula, amesema wamejipanga kutoa huduma tofauti katika maonesho hayo kwa lengo la kuvutia wateja wengi zaidi.

“Nilisikia kuhusu maonesho haya na nikaona ni fursa ya kuonyesha ubunifu wangu katika mapishi na utoaji huduma bora. Natarajia kupata wateja wengi zaidi kuliko kawaida,” amesema Leah.

Ikumbukwe kuwa Wilaya ya Kilolo ni eneo lenye mandhari ya kuvutia na uoto wa asili, hivyo maonesho haya yanatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa wakazi wa maeneo mbalimbali.

Ni jukwaa la kipekee kwa wakulima, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali kuonyesha ubunifu wao, kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa waliopiga hatua katika sekta za kilimo, viwanda na biashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *