Kafulila atoa kauli wanaodhani ‘ubia ni kuuza nchi’

Mwanza. Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila amesema nchi kuingia ubia na wawekezaji wa kigeni katika miradi inayotekelezwa, haimaanishi imeuzwa kama ilivyo mitazamo ya baadhi ya wananchi.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 16, 2025 katika kongamano la Kitaifa lililohusu ubia wa sekta ya umma na binafsi katika muktadha wa dira ya Taifa 2050 lililofanyika jijini Mwanza, Kafulila amesema kwenye ubia katika uwekezaji umiliki hauhamishwi unabaki kumilikiwa na Serikali ingawa mwekezaji analeta mtaji na uendeshaji kwa kipindi fulani.

“Ubia ni kama ndoa kati ya sekta binafsi na Serikali. Kwenye ubia hatuhamishi umiliki. Leo tukisema tunajenga barabara ya kulipia kati ya Kibaha kwenda Chalinze mpaka Morogoro haimaanishi kwamba lile eneo siyo mali ya Serikali tena, hapana! Ni kwamba Serikali ndiyo mmiliki lakini sekta binafsi inakuja kuleta teknolojia, mtaji, kujenga na kuendesha kwa miaka kadhaa kisha uwekezaji unarudi kwa Serikali,”amesema Kafulila.

Amesema hiyo ni kwa maeneo yote ambayo Serikali inaingia ubia na Sekta binafsi yakiwemo masoko bandari na stendi ambapo wawekezaji hupewa muda maalumu ambao ni mkataba wa muda mrefu kulingana na ambavyo hesabu zitafanywa na kuamua ni apewe miaka mingapi kutekeleza mradi husika.

Amesema hakuna kinachouzwa isipokuwa ni ushirika wa sekta binafsi katika muda maalumu kufanya uendeshaji kwaajili ya kuisaidia Serikali iweze kutumia rasilimali zake kuwekeza kwenye elimu, afya na lishe ambako sekta hiyo haivutiwi kufanya kwa wananchi.

“Kwahiyo ubia siyo ubinafsishaji…ubinafsishaji maana yake unahamisha umiliki kwenda kampuni binafsi. Mradi wa ubia ni mali ya Serikali kabla, wakati na baada ya utekelezaji,”ameeleza Kafulila.

Katika hatua nyingine, Kafulila amesema kuna umuhimu wa wananchi kujua masuala ya ubia kutokana na dunia nzima kufanya hivyo ili kuinua uchumi wan chi husika pamoja na wa wananchi wake.

“Serikali zote duniani imekuwa ni ngumu kutekeleza matarajio ya wananchi kwa kutumia kodi na mikopo, na ushahidi wake ni takwimu za hali ya uchumi wa dunia kufikia Novemba, 2024 Ilikuwa takribani Sh115 trilioni ukilinganisha na deni la serikali zote duniani ni Sh102 trilioni huku deni la dunia yote kwa maana ya serikali, sekta binafsi, na kaya ilikuwa ni Dola trliioni 315,” amesema.

“Tafsiri yake uchumi  wa dunia unaendeshwa kwa mikopo ambapo deni la dunia ni asilimia zaidi ya 90, kwenye upande wa Afrika ni asilimia 67 na Tanzania ni 47 hivyo Pamoja mijadala ya deni la taifa kuwepo ni kielelezo kwamba serikali ya awamu ya sita inafanya vizuri,” ameongeza Kafulila.

Akifungua kongamano hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo amesema kuna ugumu wa sekta hiyo kushirikiana na umma kufanya biashara huku akieleza Serikali itaendelea kuweka mazingira bora, wezeshi na shindani ili kuiwezesha sekta hiyo kufanya kazi kwa ufanisi.

Akitoa maoni yao kwenye kongamano hilo, Mkurugenzi wa Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake na Wajasiriamali Kanda ya Ziwa (TWCC), Happiness Mabula amesema miongoni mwa changamoto ambazo angependa ziangaliwe kwenye dira ya Taifa 20250 upande wa ubia ni utitiri wa kodi unaofanya wanawake kukata tama na kujifungia ndani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JAET, Dk Elibariki Mmmari amesema kinachokwamisha ubia kati ya wafanyabiashara na wawekezaji ni mtaji akishauri Serikali kuja na sera ya kuwezesha wananchi.

Akizungumzia faida ya ubia,  Mkurugenzi w Huduma za Sheria Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), Stanslaus Kagisa amesema ubia umeinufaisha sekta ya bandari kwakuwa kutokana na teknolojia na tehama waliyokuja nayo wawekezaji hakuna mapato ya Serikali yanayopotea.

Hata hivyo, Kagisa amesema wameondokana na gharama ya kununua mitambo ya kushusha na kupakia mizigo na matengenezo yake pamoja na kupunguziwa mzigo wa gharama ya mishahara kwa baadhi ya wafanyakazi.

Amesema hata mitazamo ya baadhi ya watu kuwa bandari imeuzwa siyo ya kweli bali kuna ubia kati ya sekta binafsi na Serikali kwakuwa hata katiba ya nchi inazuia ardhi kuuzwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *