Mongella awatwika zigo wanawake nchi kujitegemea, amkumbuka Nyerere

Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe na mwanaharakati wa uwezeshaji wa wanawake nchini, Getrude Mongella amesema uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump wa kusitisha misaada ya maendeleo kwa nchi nyingi duniani, umemkumbusha falsafa ya kujitegemea ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Trump alitoa uamuzi huo siku moja tu baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Marekani huku ikielezwa kuwa ni amri ya kiutendaji, iliyosainiwa na rais huyo ili kupisha tathmini ya ufanisi, uwiano na sera yake ya kigeni.

Akizungumza leo Jumatano, Aprili 16, 2025, jijini Dar es Salaam katika kongamano maalumu la kuadhimisha miaka 30 ya Mkutano wa Beijing, Mongella amesisitiza kuwa kufikia hatua ya kujitegemea kwa taifa, kunahitaji ushiriki wa kila mmoja. Ametoa wito mahususi kwa wanawake kutobaki nyuma katika safari hiyo ya maendeleo.

“Kama kuna jambo ambalo Mwalimu Nyerere alilitilia mkazo kwa uchungu, ni dhana ya kujitegemea. Kila siku alikuwa akisisitiza kwamba hatuna wajomba, ni lazima tujitegemee,” amesema Mongella.

Amewahimiza wanawake kujitokeza na kuwa sehemu ya mabadiliko ya kweli, wakisaidia pale ambapo wanaume wamefikia, ili kwa pamoja wajenge taifa linalojitegemea.

“Wanawake mnapaswa kujiuliza, mnafanya nini kupitia nafasi zenu kuhakikisha nchi inajitegemea,” amesema mama huyo.

Amesema ili kufikia lengo hilo, ni lazima kuwe na juhudi zaidi za kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Maendeleo katika vipaumbele vya Beijing

Akizungumzia miaka 30 tangu Mkutano wa Beijing, Mongella amesema Tanzania imepiga hatua katika utekelezaji wa baadhi ya vipaumbele 12 vilivyowekwa, ikiwemo masuala ya wanawake na umaskini, uchumi, afya, uongozi, ukatili dhidi ya wanawake na haki za mtoto wa kike.

Amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa uwakilishi wa wanawake katika uongozi, sheria za ardhi zinazozingatia usawa wa kijinsia, sheria ya kudhibiti makosa ya kijinsia na bajeti ya taifa yenye mtazamo wa kijinsia.

“Ninakumbuka wakati fulani tulikuwa kazini, umeolewa na unajifungua, lakini hakuna sheria ya likizo ya uzazi. Mimi nilizaa watoto wawili mfululizo nikiwa kazini, bila likizo hiyo,” ametoa ushuhuda huo.

Mongella ambaye sasa ana miaka 80, amesema anatamani kuona mapinduzi ya kiteknolojia yanayomwezesha mwanamke kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

“Natamani nione siku mwanamke hawezi tena kulima kwa kutumia jembe la mkono bali trekta; badala ya kutwanga kwa mkono kuwepo na teknolojia rahisi. Tunahitaji mkakati wa makusudi wa kuwasaidia wanawake kutumia na kutengeneza teknolojia,” amesema.

Mwakilishi Mkazi wa UN Women, Hodan Addou amesema mapambano ya kupigania usawa wa kijinsia yanapaswa kuendelezwa kwa kuwawezesha vijana wanaharakati ili wapaze sauti zao kwa ujasiri.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande amesema mwanamke ana nafasi kubwa katika maendeleo ya jamii.

“Mama ni kiungo kikuu cha maendeleo ya kila mmoja wetu. Ni mama pekee anayeweza kutafsiri sauti ya mtoto wake au chozi la huzuni na kulitatua kwa vitendo,” amesema.

Amesema mafanikio ya mkutano wa Beijing na juhudi za kumkomboa mwanamke yameleta manufaa si kwa wanawake pekee, bali pia kwa wanaume.

“Bila mabadiliko yaliyotokana na Beijing, kuna watu leo wasingejulikana au hata kuwepo,” aliongeza.

Hivyo, Chande amesisitiza kuwa ili wanawake wapige hatua zaidi, ni muhimu kumweka Mungu mbele, kupendana na kuepuka wivu, choyo na husuda.

“Wivu, choyo na husuda vinaweza kumfanya mwanamke kumchukia mwingine ambaye ungeweza kujifunza mengi kutoka kwake. Hili ni jambo muhimu sana kuliepuka,” amesisitiza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *