Maagizo ya Rais Mwinyi kwa mabalozi waliokwenda kumuaga

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewasisitiza mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa ya nje kuzingatia diplomasia ya uchumi na fursa za uwekezaji zilizopo.

Rais Mwinyi amesema hayo leo Aprili 16, 2025 Ikulu, Zanzibar alipozungumza na mabalozi wa Tanzania katika mataifa ya Rwanda, Zimbabwe, Sweden na Msumbiji waliokwenda kumuaga kabla ya kwenda kwenye vituo vyao vya kazi baada ya kuteuliwa hivi karibuni.

“Kafanyeni juhudi maalumu za kuitangaza sera ya uchumi wa buluu na utalii katika mataifa mnayokwenda ili kuvutia wawekezaji zaidi kuja kuwekeza nchini,” ameagiza.

Dk Mwinyi amesema Zanzibar bado inahitaji wawekezaji wengi, hususan katika sekta hizo kuu za kipaumbele kutokana na kuwapo fursa nyingi zikiwamo za uvuvi, utalii, mafuta na gesi.

Amesema suala la uhusiano wa kimataifa hivi sasa limeelekezwa zaidi katika uchumi, hivyo wanapaswa kuzingatia zaidi kuimarisha uhusiano wa kiuchumi.

Ameyataja maeneo yenye fursa za kutosha kuwa ni uwekezaji katika sekta ya bandari, ikiwamo kwa ajili ya makontena, usafirishaji wa mizigo, mafuta na gesi.

Akizungumzia sekta ya biashara amewaagiza mabalozi kuzitafutia masoko bidhaa za Tanzania zikiwamo za viungo vinavyozalishwa kwa wingi Zanzibar.

Kwa upande wao, mabalozi wameahidi kuyatumia maelekezo ya Rais Mwinyi kama nyenzo na dira ya kufanya kazi kwa ufanisi.

Pia kuyazingatia maeneo muhimu ya kiuchumi kwa kushawishi wawekezaji kuwekeza.

Mabalozi hao ni Habibu Kambanga (Rwanda), Suzane Kaganda (Zimbabwe), Mobhare Matinyi (Sweden) na Hamad Hamad (Msumbiji).

Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Balozi Matinyi amesema amepokea maelekezo hayo na anaahidi kwenda kuyafanyia kazi kwa bidii ili kuiletea Tanzania fursa za uwekezaji, biashara na ukuzaji utalii.

“Nchi za Nordic na Baltic zipo katika kundi la nchi zenye kipato kizuri kwa watu wake na huzalisha watalii wengi duniani. Hivyo, tukiongeza juhudi za kuitangaza Tanzania hakika tutapata watalii wengi zaidi kutoka huko.

“Nchi hizi pia zimepiga hatua kubwa katika uchumi wa buluu, hususan katika sekta ya uvuvi na katika uchimbaji wa mafuta na gesi asilia. Hii itakuwa fursa adhimu ya kuendelea kuziunganisha nchi hizi na Tanzania katika sekta hizo ili tujenge zaidi ushirikiano kama nchi rafiki za muda mrefu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *