Dar es Salaam. Simba leo imetangaza kuingia mkataba wa miaka mitano na kampuni ya Jayrutty Investment wa kubuni, kuzalisha na kusambaza jezi na bidhaa nyingine zenye nembo ya klabu hiyo ambao utakuwa wenye thamani ya Sh38 bilioni.
Mwenyekiti wa kamati ya tenda ya Simba, Dk Seif Muba amesema kuwa ofa ya kampuni hiyo imeishawishi Simba kuwapa haki za matumizi ya nembo yao kwa vile mbali na fedha, inaenda sambamba na manufaa mengi kwa klabu hiyo.
“Tulipokea barua nyingi za maombi lakini bodi iliamua makampuni yashindane kwa tenda. Kampuni nane zilichukua ‘tender document’ (hatu ya zabuni) lakini kampuni sita zilirudisha ‘document’ (hati). Maombi ya wazabuni yalifunguliwa kwa uwazi na baada ya mchakato wazabuni wote walijulishwa mzabuni ambaye ameibuka mshindi kwa kuweka fedha na vitu vingi ambavyo tulihitaji. Tuliingia mkataba wa miaka mitano na kampuni hiyo.
“Mshindi aliyeshinda tenda hiyo ameshinda kwa kuweka kiasi cha fedha cha Tsh. 38 Bilioni. Napenda kuitangaza kampuni ya Jayrutty Investment Company Limited kama mshindi. Klabu ya Simba inakwenda kupata Tsh. 5.6 Bilioni kwa mwaka,” amesema Dk. Muba.
Mkurugenzi wa kampuni ya Jayrutty Investment, Joseph Rwegasira ameorodhesha baadhi ya faida ambazo Simba itazipata katika kipindi chote cha mkataba huo.

“Kiasi ambacho kimetajwa ni kiasi ambacho tumezingatia mambo mengi kama klabu. Nipende kuwahakikishia kabla hata hatujafanya kitu chochote tumeshaweka 30% ya hiki kiasi cha mwaka wa kwanza.
“Jambo la kwanza ambalo tunakwenda kutekeleza ni kujenga uwanja wa mpira, uwanja ambao utachukua mashabiki 10,000 hadi 12,000 na tumekubaliana kwamba Simba wana uwanja Bunju na tutakwenda kujenga uwanja Bunju lakini kama watakuja na mapendekezo mengine basi tutayafata.
“Tunajua kwamba Simba makao makuu yapo Msimbazi lakini tunakwenda kujenga ofisi za kisasa. Lakini pia kila mwaka tutatoa Tsh. 100 milioni ya kusaidia kukuza soka la vijana. Kila mwaka pia tutachangia Tsh. 100 milioni kuchangilia pre-season. Pia tumeahidi kujenga kituo maalumu cha matibabu ya wachezaji. Kila mwaka pia tutashiriki bega bega katika Simba Day, tutachangia Tsh. 100 milioni kila mwaka,” alisema Rwegasira.
Aliongeza pia kuwa watatoa kiasi cha Sh450 milioni kwa mwaka kwenda kwa wachezaji huku akifichua kuwa jezi za timu hiyo zitatengenezwa na kampuni kubwa duniani.
“Tumeenda kimataifa kuhakikisha tunapata international brand, niwahakikishie kwamba msimu unaokuja jezi ambayo Simba watavaa, watavaa jezi ya kimataifa. Tumeingia mkataba wa kimataifa na brand mojawapo kubwa duniani ambayo inazivisha klabu nyingi kubwa.
“Hivi karibuni tutaitangaza brand ambayo itavalisha jezi. Tutapata ubora wa hali ya juu katika bei rafiki kabisa, kama Mwanasimba jivunie, kama uliweza kununua jezi zilizopita basi hata hivi utaweza. Nitoe pongezi kwa wazabuni waliopita, nitoe pongezi kwa Vunja Bei, nitoe shukrani kwa Sandaland na kubwa tuendelee kushirikiana,” amesema Rwegasira.
Naibu waziri wahabari, utamaduni, sanaa na michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ amesema kuwa serikali inapongeza udhamini huo.
“Hili nililosikia leo la ujenzi wa uwanja limenivutia sana. Mkiwa na kiwanja cha watu 10,000 au 12,000 kinaweza kutumika kwa michezo ya ndani, michezo ya nje ndio mkawa mnatumia Uwanja wa Mkapa, mtaupunguzia hata majukumu.
“Itoshe kusema ni uwekezaji wa mkakati ambao umekuja wakati sahihi. Serikali kama mlezi wetu tunawapongeza sana,” amesema Mwana FA.