Yanga, Inonga kuna jambo! iko hivi

KIKOSI cha Yanga kimeanza maandalizi ya mchezo wa ugenini wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate, lakini kukiwa na taarifa kwamba mabosi wa klabu hiyo wameanza hesabu za kumrejesha nchini beki wa zamani wa Simba, Henock Inonga anayekipiga kwa sasa FAR Rabat ya Morocco.

Inonga alikuwa kwenye hesabu za Yanga hata kabla ya kutua Msimbazi na kuitumikia kwa misimu miwili, lakini umafia waliofanyiwa mabosi wa Jangwani ndio uliowanyima kupata huduma ya beki huyo wa kati, ila kwa sasa inaelezwa viongozi wa klabu hiyo wameamua kumfuata tena ili atue kikosini.

Inaelezwa, Yanga imeonyesha nia ya kutaka kutimiza hesabu walizokuwa nazo tangu beki huyo alipokuwa DC Motema Pembe ya DR Congo, kabla ya Simba kumnasa kwa mkataba wa miaka miwili.

Habari kutoka ndani ya Yanga, zinasema tayari mabosi wa klabu wameanzisha mazungumzo na FAR Rabat ili kuona kama kuna uwezekano wa kuipata saini ya beki huyo, kwa vile bado ana mkataba wa mwaka mmoja na kikosi hicho kilichomsajili msimu huu kutoka Simba.

Beki huyo wa kimataifa wa DR Congo, anapigiwa hesabu za kuja kuongeza nguvu eneo la ulinzi la Yanga linaloongozwa kwa sasa na Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ nyota ambao ni panga pangua kikosi hicho na hata timu ya taifa, Taifa Stars.

“Yanga inauhitaji mkubwa wa kusajili mchezaji wa eneo hilo. Ila kuhusu nani anakuja ni mapema kuzungumza kwa sasa, lakini mchakato unaendelea na majina ya wachezaji wanatazamwa kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo hilo tumekuwa tukilifanyia kazi, kwa muda sasa yapo mezani na tayari yameanza kufanyiwa mchakato jina la Inonga ni miongoni mwao,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi.

Chanzo hicho kilisema mchakato wa kutafutwa kwa beki huyo ulianza baada ya kuachana na Gift Fredy kutoka Uganda na tangu hapo Yanga wamekuwa na wakati mgumu kupata mchezaji ambaye ataweza kuendana na ushindani uliopo hasa kwenye eneo hilo.

Inonga amekuwa beki tegemeo kwa sasa wa kikosi cha AS FAR Rabat, kilichoondolewa katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa na Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 4-3 baada ya awali kufungwa 4-1 ugenini na kuja kushinda nyumbani mabao 2-0.

“Kwa sasa mikakati mikubwa ambayo inafanywa ni kuhakikisha taji la Ligi Kuu Bara linabaki Jangwani kwa msimu wa nne mfululizo huku mambo mengine ya usajili yakifanyiwa kazi kimya kimya kabla ya msimu mpya kuanza kwani mikakati ni kuhakikisha timu ikianza kambi msimu mpya kila mchezaji ambaye ataitumikia Yanga atakuwa anafahamika,” alisema mtoa taarifa huyo.

Kabla ya kutua Simba mwanzoni mwa 2021/22, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kumtaka Inonga na mwenyewe aliithibitishia Mwanaspoti katika mahojiano akisema mazungumzo na Wananchi yalifika mbali kwa kukubaliana kila kitu.

Alisema akiwa katika hatua za mwisho kufanya uamuzi Yanga alipokea simu kutoka kwa kiongozi mwingine wa juu wa Simba ambaye naye alimueleza kuhitajika katika timu hiyo huku wakimuwekea maslahi makubwa mezani kuliko yale ya Yanga.

“Nikiwa katika tafakari ya kufanya uamuzi tena muda huo nikiwa nimepima mpaka Uviko 19 kwa pesa niliyotumiwa na Yanga na tiketi ya ndege wamenitumia pia, nilifanya mawasiliano na wachezaji wa DR Congo waliokuwa hapa nchini wakaniambia kwa wakati ule Simba ilikuwa ni bora kuliko Yanga,” anasema Inonga na kukiri kwamba baada ya kufika nchini alilazimika kurejesha fedha za Yanga walizomtumia kulipia gharama za kupima Uviko.

Kuhusu tiketi ambayo Yanga walikuwa wamemtumia anasema kwamba hakulazimika kuilipa kwavile hakuitumia, alisafiria tiketi ya Simba kuja Dar es Salaam. “Katika kufanya mawasiliano wenzangu waliokuwapo hapo na hata waliowahi kucheza waliniambia Simba ni bora kuliko Yanga kwa wakati ule, kwa hiyo nilibadili uamuzi na kuamua kutua Msimbazi.”

Inonga alisema Yanga walifanya kila kitu kwa ajili yake na walikuwa wanamsubiri nchini ili kuja kumalizana nao kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili.

“Dah! Nadhani ilikuwa imepangwa tu nije kucheza Simba, kwani nilifika mpaka uwanja wa ndege wa Kinshasa ili nije Tanzania, lakini hilo lilishindikana na nilibadili uamuzi na kuja siku nyingine kwa ajili ya Simba,” alinukuliwa Inonga katika mahojiano hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *