
Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, wamebaini uwepo wa shule zinazofundisha masomo ya sayansi zisizo na maabara, huku zikiwa zimedahili wanafunzi ambao baadhi watafanya mitihani ya miwisho Mei 2025.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Aprili 16, 2025 na mwenyekiti wa kamati hiyo, Justin Nyamoga wakati akisoma maoni ya kamati yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2025/26.
Nyamoga amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uthubutu wake na kuweza kujenga shule nyingi za sekondari na hasa sekondari za wasichana za Mikoa na sasa sekondari za wavulana za kanda.
“Tunapongeza zaidi hasa baada ya shule hizi za sekondari za wasichana za mikoa kuwa maalum kwa ajili ya kufundisha watoto wa kike sayansi na hivyo kuongeza idadi kubwa ya wanansayansi nchini,” amesema Nyamoga.
Hata hivyo, Nyamoga amesema kamati inatambua ili masomo ya sayansi yafundishwe vyema na ili wanafunzi hawa waweze kuielewa vyema sayansi ni muhimu kuwepo na maabara pamoja na vifaa vyote vya maabara kwenye shule zote.
Amesema wakati wa ukaguzi wake kwenye miradi mbalimbali ya shule za sekondari nchini wamegundua kuwa hakuna kabisa vifaa vya maabara.
Nyamoga amesema kamati imebaini asilimia kubwa ya shule hizo tayari zimeshadahili wanafunzi na wengine wanatarajia kufanya mitihani yao ya mwisho Mei mwaka huu wa 2025.
“Kamati inahofu wanafunzi hao kama Serikali isipokuwa na mpango wa dharura, watafanya mitihani yao bila kuwa na uwezo wa kufanya mitihani ya mafunzo kwa vitendo (practical) kutokana na kutokuwepo kwa maabara,” amesema.
Amesema kutokana na hali hiyo imeshauri Serikali iweke mpango makakati wa dharura wa kuhakikisha kwamba inapeleka vifaa vya maabara kwenye shule zote 26 za wasichana za mikoa bila kuathiri mipango iliyowekwa ya upelekaji wa vifaa vya maabara katika shule nyingine za sekondari nchini.
“Kwa kuwa tatizo la uhaba wa vifaa vya maabara katika shule za sekondari nchini ni la muda mrefu na linaonekana kuwa gumu, Kamati inashauri Serikali itenge fungu maalumu kwa kutumia chanzo maalumu na cha kudumu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara kwa ajili ya shule za sekondari nchini wakati wote vinapohitajika,” amesema Nyamoga.
Shule za kingereza zifutwe
Nyamoga amesema kamati ilibaini halmashauri nyingi zimeanza kujikita katika ujenzi wa shule maalum za msingi za mchepuo wa kiingereza (English Medium School) kwa kutumia fedha ya Serikali na kutoza ada kubwa kwa wanafunzi wanaokwenda kusoma katika shule hizo.
Amesema kamati haikuridhika kabisa na utaratibu wa halmashauri kujikita katika ujenzi wa shule hizi na kutoza ada kubwa na kwa kufanya hivyo kunaondoa usawa wa upatikanaji wa elimu kwa Watanzania na hivyo kujenga madaraja nchini.
“Hii si dhamira ya Serikali na si tamko la Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023,”amesema.
“Kamati inashauri halmashauri kuacha kabisa kujihusisha na ujenzi wa shule hizi kwa kutumia fedha yoyote ile ya Serikali na kuzitoza ada kubwa kwa kuwa inakwenda kinyume na mipango ya Serikali ya utoaji wa elimu bure kwa shule za sekondari,” amesema.
Amesema kama kuna ulazima kwa halmashauri yoyote ile kuanzisha shule za mchepuo wa kiingereza iombe kibali kutoka Tamisemi na ieleze sababu za msingi zinazolazimisha uanzishwaji wa shule za mchepuo wa Kiingereza katika halmashauri husika.
“Serikali iwarejeshe walimu wote wazuri waliochukuliwa kutoka shule ze umma na kupelekwa kwenye shule hizi maalumu za mchepuo wa kiingereza katika shule zao za awali ili waendelee kuinua ubora wa elimu katika shule hizi za umma,”amesema.
Kuhusu madeni ya watumishi, kamati hiyo imebaini kuwa halmashauri nyingi zimekuwa zikizalisha madeni makubwa bila kuyalipa na hivyo kuiweka Serikali kwenye wakati mgumu wa utekelezaji wa majukumu yake.
“Kamati ilihoji sababu ya uwepo wa madeni hayo na kutaarifiwa kuwa ni sababu ni pamoja na malipo ya uhamisho wa watumishi pamoja na posho mbalimbali za watumishi katika halmashauri husika,”amesema.
Ametoa mfano Mkoa wa Dodoma peke yake umezalisha madeni yenye thamani ya Sh12 bilioni yanayotokana na utumishi.
“Haya ni makubwa mno. Hii ni dalili mbaya sana. Kutokana na changamoto hii kutishia usitawi wa halmashauri nchini. Kamati inashauri Serikali kuweka mkakati wa ulipaji wa madeni haya kwa wakati ili kuziweka huru halmashauri,” amesema.
Ameshauri pia Serikali kusimamisha uzalishaji wa madeni mengine ya namna yoyote ile katika halmashauri hadi pale madeni yaliyozalishwa awali kuwa yamekwishakulipwa kwa walau asilimia 50.
Kwa upande wa vyoo, Nyamoga amesema kamati ilibaini kuwa kuna upungufu mkubwa wa matundu vya vyoo katika shule nyingi na inaona kuwa hali hiyo si nzuri kwa ustawi wa Taifa la Tanzania.
“Serikali ifanya tathmini ili kubaini ukubwa wa tatizo la upungufu wa matundu ya vyoo katika shule zake zote za msingi na sekondari nchni. Serikali ifanye tathmini ya ubora wa vyoo katika shule zake zote za msingi na sekonda nchini (hasa kwenye shule kongwe),” amesema.
Ameshauri pia Serikali iweke mkakati wa kumaliza kabisa tatizo la vyoo katika shule zake za msingi na sekondari nchini.
Aidha, amesema kila mkoa na halmashauri zake zote zenye upungufu wa vyoo zisimamiwe kwa kuweka mkakati wa kutatua na kukomesha kabisa tatizo laa ukosefu pamoja na ubora hafifu wa vyoo katika shule zake za msingi na sekondari nchini.