Wanafunzi wa kike wabuni mashine ya kuhesabu kura

Arusha. Katika kusaidia kuharakisha mchakato wa kuhesabu kura, wanafunzi wawili wa kike wa kidato cha tatu, wamebuni kifaa kinachoweza kutumika kuhesabu kura.

Aidha wamesema licha ya kutambua kuwa kifaa hicho hakijafikia viwango vya kuweza kutumika katika chaguzi mbalimbali ikiwemo Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka huu, wameiomba Serikali kuwasaidia kuboresha mashine hiyo ili iweze kutumika.

Wanafunzi hao wa kidato cha tatu ni Thuraiya Makame kutoka Shule ya Sekondari Mpapa (Zanzibar) na Jorim Buntu kutoka Shule ya Sekondari Kibasila ya jijini Dar es Salaam.

Wanafunzi hao wameitambulisha mashine hiyo leo Jumatano Aprili 16, 20225 jijini Arusha wakati wa kufunga mafunzo ya Tehama kwa wasichana kwa mwaka 2025, yaliyoratibiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (Ucsaf) na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Akizungumza katika mafunzo hayo, Jorim amesema yeye na mwenzake wamekuja na wazo la kutengeneza kifaa hicho na kikiboreshwa, kitasaidia kupunguza muda wa kuhesabu kura.

“Tunajua makarani wanahesabu kura kwa muda mrefu na sisi tunachoka kusubiri matokeo mpaka yatoke, hivyo tumekuja na kifaa hiki ambacho kitapunguza muda unaotumika kuhesabu kura,” amesema mwanafunzi huyo na kuongeza;

“Tungetamani Serikali na taasisi zinazohusika zitusaidie kukiboresha kifaa hiki, tunajua hakijafikia kiwango ambacho kinatakiwa, lakini tunaweza kukiboresha ili kitumike katika uchaguzi kuanzia shuleni, kwenye na katika uchaguzi mkuu mwingine.”

Naye Thuraiya ameiomba Serikali isaidie kutoa mafunzo zaidi kwa wasichana kusudi waweze kuleta mifumo na mawazo yatakayoendelezwa kwa kutumia teknolojia ili yalete maendeleo chanya katika taifa.

Amesema wasichana hawapaswi kuogopa masomo ya Tehama, badala yake wachangamkie yaweze kutatua changamoto zao na za wengine.

“Kupitia mafunzo haya sisi tumejifunza mambo mengi na tunaamini msichana akiwezeshwa zaidi ataweza kufanya mambo ya kibunifu yenye kusaidia jamii,” amesema.

Akifunga mafunzo hayo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema kumefanyika tafiti mbalimbali zilizoonyesha ili kuziba pengo la kijinsia katika sekta ya Tehama lazima wasichana waendelee kuhamasishwa kwani bado wanaochagua masomo hayo ni wachache.

Waziri Silaa amesema hiyo inapunguza nguvu kazi ya taifa na kuwa ni muhimu kuwashirikisha wasichana na wanawake ili wawe sehemu ya kizazi cha ubunifu na masuala ya teknolojia.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha Shule za Serikali zinarejea katika hali ya juu ikiwemo kuendelea kuimarisha miundombinu ya Tehama, kuweka mazingira bora ya wanafunzi na walimu lengo ni kuhakikisha kila wanafunzi anapata fursa sawa ya elimu bora na ya kisasa.

“Serikali inaendelea kujenga msingi imara kwa kuwekeza katika elimu, usawa wa kijinsia katika Tehama hivyo ninyi mliopata fursa ya mafunzo haya muendelee kujiendeleza kwani teknolojia inakua kila siku,”amesema.

“Mlioonyesha bunifu pale nje mmeonyesha ujasiri na uwezo wa hali ya juu, nawatia moyo muongeze juhudi na mkawe chachu kwa wanafunzi wenzenu ili wajue mtoto wa kike hakuna kizingiti kwenye maisha yake na Serikali inafanya kila inachoweza kuhakikisha ndoto za mtoto wa kike zinatimia,” amesema waziri huyo.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Ucsaf, Mhandisi Peter Mwasalyanda amesema mafunzo hayo yameshirikisha washiriki 31 kutoka Shule mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar yenye lengo la kuhamasisha wasichana kuchagua masomo na taaluma katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati, ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya kimataifa ya wasichana katika Tehama Aprili 24, 2025.

Amesema kwa mwaka huu wanafunzi 246 kupitia vituo sita vilivyokuwa mikoa ya Arusha, Dar Es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Zanzibar, wamepatiwa mafunzo hayo.

Mhandisi huyo amesema mafunzo hayo ya Tehama kwa wasichana wameanza kuyatoa mwaka 2016 ambapo hadi sasa wanafunzi wa kike 1,400 wamenufaika na program hiyo.

Mwakilishi kutoka Costech, Dk Athuman Mgumia amesema miongoni mwa majukumu ya tume hiyo ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa makundi mbalimbali ili mawazo yao ya kibunifu yaweze kutatua changamoto katika jamii.

Amesema tume hiyo iko tayari kuendelea kuwasaidia wasichana hao kukuza bunifu zao ili zitambulike na ziweze kutumika katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili jamii.

“Moja ya majukumu yetu ni kuweka mazingira wezeshi kwa makundi mbalimbali ikiwemo wasichana.Wasichana hawa wametoka kwenye shule mbalimbali nchini, tunawasihi msiziache bunifu zenu hizi mziendeleze nasi tuko tayari kusaidia kuziendeleza,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *