ACT Wazalendo kushiriki uchaguzi, waeleza sababu

Unguja. Kamati ya Uongozi ya ACT Wazalendo imeridhia kwa kauli moja kwamba chama hicho kishiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 huku kikitaja sababu tatu ikiwamo ya kupigania mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi.

Uamuzi huo umefanyika jana Aprili 15, 2025 mjini Unguja, Zanzibar katika kikao cha Kamati ya Uongozi kilichokaa na kupitisha uamuzi huo utakaokiwezesha chama hicho kushiriki uchaguzi katika ngazi zote.

Akiwasilisha uamuzi huo wa Kamati ya Uongozi, Dorothy amesema uamuzi huo umezingatia uchambuzi wa kina wa kisiasa nchini Tanzania na uzoefu kutoka katika nchi mbalimbali duniani zilizo katika hali ya kisiasa kama Tanzania.

“Naomba kuwajulisha kuwa baada ya tafakuri ya kina, Kamati ya Uongozi ya Taifa imeamua kuwa chama cha ACT Wazalendo kitashiriki kwenye Uchaguzi Mkuu 2025 kwa nafasi zote za Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, urais wa Zanzibar, ubunge, uwakilishi na udiwani,” amesema Dorothy.

Amesema Kamati ya Uongozi, kabla ya kufikia uamuzi huo, ilifanya tafakuri ya kina na kujiridhisha kuwa huo ndio uamuzi sahihi unaopaswa kuchukuliwa na chama kwa kuzingatia hali halisi ya kisiasa katika nchi na wajibu wa kimapambano ambao ACT Wazalendo imeubeba.

Dorothy, ambaye pia ni mtia nia wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amebainisha kwamba sababu tatu ziliifanya Kamati ya Uongozi kufikia uamuzi huo ikiwamo kutaka kutetea na kulinda thamani ya kura ambayo imeporwa kutoka kwa wananchi.

“Uzoefu unaonyesha thamani ya kura imepotea. Wananchi hawana tena nguvu ya kuchagua viongozi wao, viongozi wanachaguliwa kwa nguvu ya dola,” amesema.

Amesisitiza kwamba chama chake kinakusudia kuongoza vuguvugu nchi nzima kutetea na kulinda thamani ya kura. Amesema watatumia uchaguzi ujao kutetea na kulinda demokrasia.

Sababu nyingine, amesema kususia uchaguzi ni kuimarisha hujuma dhidi ya demokrasia. Amesema watawala wanafurahi vyama makini vya upinzani vikisusia uchaguzi.

Amebainisha kwamba uzoefu katika mataifa tofauti kama Kenya, Misri, Ivory Coast, Venezuela na Zanzibar ambapo upinzani uliposusa, watawala hawakubadilika, bali walifurahia kujiondoa kwao.

Dorothy amesema wanashiriki uchaguzi kwa kuwa wamejiandaa vizuri kushika dola kwa kuwa CCM kimeshindwa kuendesha nchi. Amesema chama hicho kimeshindwa kuitetea jamii, ndio maana rushwa imekithiri.

“Kwa mujibu wa ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali) ya mwaka 2022/23, Sh3.14 trilioni zimepotea. Tunashiriki uchaguzi ili kutoa jukwaa kwa wananchi kukataa ufisadi. Tunashiriki kupigania Taifa la wote kwa maslahi ya wote,” amesema Dorothy.

Othman arudisha fomu

Katika hatua nyingine, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amerejesha fomu akiomba ridhaa ya chama chake kuwa mgombea urais wa Zanzibar kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Othman, aliyetangaza nia ya kugombea nafasi hiyo Januari Mosi, 2025 na kuchukua fomu Aprili 13, 2025, amerejesha fomu hiyo katika makao makuu ya ACT Wazalendo Zanzibar na kumkabidhi, Katibu wa Kamati ya Uchaguzi ya chama hicho, Mhene Said Rashid.

Tukio hilo limeshuhudiwa na viongozi wengine wa chama hicho, akiwemo Kiongozi wa Chama, Dorothy, Makamu Mwenyekiti Bara, Issihaka Mchinjita, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Ismail Jussa, Katibu Mkuu, Ado Shaibu na viongozi wengine.

Akizungumza baada ya kumkabidhi fomu, Othman ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho, ameahidi kutowaangusha wananchi kwani anakusudia kubadilisha maisha yao.

Othman amesema Zanzibar inahitaji kukwamuliwa na huu ni mwaka wa kuinusuru Zanzibar kupitia uchaguzi ili kuiwezesha kunufaika na rasilimali zake, kuboresha mifumo ya uchaguzi, kuleta umoja wa kitaifa na kujenga mifumo ya kitaasisi na kuzuia ubadhirifu wa mali za umma.

“Kwa uzoefu nilioupata katika maisha yangu ya utumishi wa umma, ninaamini nina weledi wa kutosha kuwatumikia wananchi katika nafasi ya Rais wa Zanzibar.

“Nimechukua nankurejesha fomu, mnibebeshe huo mzigo wa kuwatoa Wazanzibar katika maisha ya umasikini, dhuluma na kutopata haki zao za msingi,” amesema Othman.

Amesisitiza kwamba kinachoongeza thamani ya ushindi wao kwenye uchaguzi ujao ni uelewa wa wananchi wa Zanzibar ambao wanaona ufisadi mkubwa unaofanyika.

“Ninaingia kwenye uchaguzi huu na moyo kama ule wa ntangulizi wangu, Maalim Seif Sharif Hamad, moyo wa ushindi. Wazanzibar wanahitaji mabadiliko mkubwa,” amesema Othman.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *