
Viwanja vya Mkwakwani Tanga na Tanzanite Kwaraa, Babati, Manyara vimechaguliwa kuandaa mechi za nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, Mei mwaka huu.
Mchezo wa Yanga dhidi ya JKT Tanzania, utachezwa katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga, Mei 16.
Siku mbili baadaye kwa maana ya Mei 18, Simba itaumana na Singida Black Stars katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati.
Yanga ina historia nzuri na Uwanja wa Mkwakwani Tanga kwenye mechi za mashindano hayo kwani ndipo ilitwaa ubingwa katika msimu wa 2022/2023 ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC.
Simba katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, imecheza mechi moja ya ligi ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Fountain Gate.
Yanga imeingia hatua ya nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 8-1 dhidi ya Stand United wakati Simba iliichapa Mbeya City kwa mabao 3-1.
Singida Black Stars imefuzu kwa kuifunga Kagera Sugar kwa mabao 2-0 na JKT Tanzania imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Pamba Jiji FC.