
Dodoma. Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo ameibua tuhuma za ufisadi juu ya matumizi mabaya ya fedha kwenye miradi ya maendeleo.
Gambo amesema hayo leo Jumatano, Aprili 16, 2025 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka wa fedha 2025/26.
“Mimi naamini ukiwa mnafiki ukiwa kijana ukizeeka unakuwa ni mchawi na uchawi si sifa nzuri,” amesema Gambo ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Gambo amesema Jiji la Arusha wanajenga jengo la utawala ambalo baadhi ya viongozi wanalipigia debe.
“Lakini nikuombe waziri uunde timu yako ikakae pale ikaangalie kinachoendelea pale ndani. Katika jengo la utawala gharama zake za jumla hazipungui Sh9 bilioni.”
“Jengo la ghorofa nane unajenga kwa Sh9 bilioni maana yake kila floo moja ni Sh1 bilioni na ushee kitu ambacho kama una akili nzuri hakiwezekani,” amesema.
Amesema ukiangalia wameingia mkataba juzi wa Sh6.2 bilioni ambapo katika ule mkataba kuna baadhi ya vipimo walivyoandika kwenye thamani ya makadirio ya ujenzi (BOQ) na kwenye utekelezaji ni tofauti.
Amesema kwenye BOQ ni 1,821 mita za mraba, mkandarasi ametoa zabuni kwa mita za miraba 11,828, vipimo ambavyo vimeongeza gharama ya Sh252 bilioni.
“Wameingia mkataba wa Sh6.2 bilioni, gharama zilitakiwa ziwe Sh3.4 bilioni kuna ziada ya Sh8 bilioni leo wananchi wa Arusha wanapata taabu ya barabara za ndani. Ni shida watu wanachezea fedha namna hii na badala ya viongozi mliowaamini kusimamia ndio wao wanakwenda kushabikia,” amesema.
Ameomba kuongeza jicho za ziada kwenye usimamizi wa miradi kwa sababu Rais anatafuta fedha dunia nzima kwa ajili ya Watanzania, lakini badala ya kusimamiwa vizuri zinakwenda kuliwa na watu wachache, jambo ambalo halikubaliki.
“Utasikia mheshimiwa mbunge anagombana na kila mtu ujinga wa namna hii, utaachaje kugombana na kila mtu kwa sababu mimi nimechanguliwa pale kulinda masilahi ya watu hasa wanyonge, kwa hiyo nikuambie mheshimiwa waziri utusaidie kwa sababu hili jambo ‘very serious’,” amesema.
Amesema Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) wanao ushahidi kuhusiana na jambo hilo lakini hatua hazichukuliwi.
“Tuliwaambia kuna wizi ulifanyika pale, CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) akaleta timu kukawa na timu maalumu madudu ya kufa mtu, hakuna mtu aliyechukuliwa hatua, wanafanya kuzuga zuga tu, utasimamishwa kidogo lakini hatua serious hakuna,” amesema.
Aidha, amesema bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) ni Sh4.39 bilioni lakini watu wanachezea fedha wakati zingeenda kwenye barabara zingemaliza kelele zinazosikika katika jiji hilo.
“Wanataka zije huku kwa sababu ni rahisi kuzila na wanashirikiana kulimaliza jiji lile la Arusha,” amesema.
Ameshauri wakae kwa pamoja ili mipango ya maendeleo inayopangwa kutokana na mapato majiji hasa makubwa Arusha na Mbeya yasipangwe kimazoea bali kulingana na changamoto za watu.
“Eti unatenga Sh1.6 bilioni kwenda kubomoa eneo dogo la stendi ambalo linaingizia mapato ya Sh800 milioni halmashauri kwa mwezi leo mnaenda kulibomoa, eti mjenge jengo jingine wakati mapato mnapata pale,” amesema.
Amehoji kwa nini fedha hizo zisingekwenda katika ujenzi wa vivuko na barabara na wanafanya hivyo ili wakimaliza kujenga watapata vibanda katika eneo hilo.
Amesema pia wanataka kujenga ukumbi wa zaidi ya Sh3 bilioni si kwamba wanataka kutatua shida za wananchi bali wanataka kujipatia fedha.
Baada ya mchango huo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema kutokana na uzito wa tuhuma hizo na Bunge haliwezi kuliacha kama mchango wa kawaida.
Ametaka Waziri Mchengerwa ampelekee bungeni taarifa ndogo kuhusu ujenzi wa jengo hilo.
“Tutakupa nafasi hapa bungeni kwa sababu tuhuma zimetolewa hapa bungeni, utakapojibu hapa bungeni tutaona Bunge lichukue hatua gani, juu ya jambo kama hilo,” amesema.
Naye Mchengerwa amesema mipango katika miji na majiji haipangwi na Tamisemi inapangwa katika vikao maalumu vya mabaraza ya madiwani, kupitia kamati mbalimbali za fedha.
“Sasa hili la fedha pengine ingeenda kufanya shughuli fulani wanaoamua kutuletea ni madiwani ambao sisi wote ni wajumbe kwenye vikao hivyo, kwa hili lingine nimelipokea tutalifuatilia kwa karibu kama ambavyo mheshimiwa mbunge ameweza kuonyesha ‘consign’ yake,” amesema.
Amesema wakati wa kuhitimisha bajeti hiyo, watakwenda na taarifa bungeni ya namna walivyolichukulia jambo hilo.