TRC ilivyobeba abiria ‘kiduchu’ Dar, kuboresha huduma

Moshi. Shirika la Reli Tanzania (TRC), limeshindwa kufikia malengo ya mkakati wake wa miaka mitano (2019/2020-2023/2024) wa kubeba abiria milioni 10 katika utoaji wa usafiri jijini Dar es Salaam, na kuishia kubeba asilimia 28 tu ya lengo.

Hayo yamebainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere katika ripoti Kuu ya mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka 2023/2024, iliyowasilishwa Bungeni jijini Dodoma leo Aprili 16, 2025.

CAG amesema Mpango Mkakati wa TRC wa mwaka 2019/2020 hadi 2023/2024 unaonesha ilianzisha huduma za treni za abiria za Pugu na Ubungo ili kuongeza mapato na kupunguza msongamano wa watu kwenye usafiri jijini Dar es Salaam.

Lengo la uwezo wa kusafirisha abiria lililowekwa lilikuwa abiria 4,231,513 kwa mwaka wa fedha 2018/19 na kuongezeka hadi abiria 10,696,977 kufikia mwaka 2023/24, kama ilivyoainishwa katika mpango mkakati huo wa miaka mitano.

Hata hivyo CAG katika mapitio yake ya utendaji wa TRC alibaini hadi kufikia Juni 30,2024, lilikuwa limesafirisha abiria wapatao 3,053,428 sawa na asilimia 28, huku lengo likiwa halijafikiwa kwa abiria wapatao 7,643,549 sawa na asilimia 72.

“Kutofikia lengo kulitokana na ushindani ambao shirika linakabiliana nao, ikiwa ni pamoja na ruti mpya za mabasi na uhamisho wa kituo cha mabasi cha abiria kwenda Kamata na Kariakoo,” amesema CAG katika ripoti hiyo.

CAG amebainisha pia uwepo wa ukosefu wa treni za kisasa na zenye uwezo wa kutoa huduma bora za abiria zinazoweza kushindana kwa ufanisi na hiyo inaweza kusababisha lengo la TRC kuondoa msongamano jijini Dar lisifikiwe.

“Kwa maoni yangu, hii inaweza kusababisha shirika kutofikia malengo yake ya mapato iliyoyakusudia. Zaidi, shirika halitofikia lengo la kupunguza msongamano wa watu katika jijini Dar es Salaam,”amesisitiza CAG katika taarifa yake hiyo.

“Shirika la Reli Tanzania lilieleza kuwa liko katika mchakato wa kununua treni nne ambazo zitatoa huduma inayofaa kwa abiria,” amekumbushia CAG.

Kutokana na changamoto hiyo, CAG amependekeza TRC iongeze kasi ya mchakato wa kupata treni mpya au kufanyia matengenezo zilizopo ili kuwezesha mzunguko wa haraka na wa ufanisi kwa abiria.

TRC ilivyoshindwa

kutekeleza makubaliano

Katika ripoti hiyo, CAG amesema muundo wa TRC, ulioidhinishwa Mei 2018, ulianzisha Kurugenzi ya Maendeleo ya Biashara yenye jukumu la kutoa utaalamu katika maendeleo ya biashara, masoko, utafiti na kutafuta fursa za kibiashara.

Ili kufikia malengo hayo, TRC iliingia makubaliano na kampuni kubwa kwa ajili ya kuwasafirishia mizigo yao, lakini CAG alibaini kuwa shirika hilo lilishindwa kutekeleza kwa asilimia 67 masharti ya makubaliano hayo ya kisheria.

“Hadi Juni 30, 2024, TRC ilikuwa limesafirisha tani 115,400 pekee sawa na asilimia 33 kati ya tani 351,038 zilizotakiwa kusafirishwa. Hii inamaanisha TRC halikuweza kusafirisha tani 235,638 (asilimia 67).Hali hii, ilichangiwa na treni zisizo na ufanisi”.

Hali hiyo kwa mujibu wa CAG, inaweza kusababisha kuchelewesha kufikia malengo yaliyokusudiwa na shirika hilo na ili kutatua suala hilo, TRC  linakusudia kununua injini mpya 10 za treni hadi mwisho wa Juni 2025.

Injini nyingine nane za ziada kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG, zinatarajiwa kununuliwa ifikapo robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025.

CAG ameishauri TRC kufanya mchakato wa ununuzi wa injini mpya za treni kwa uwazi na uzingatiaji wa sheria za ununuzi na kuweka mfumo wa ufuatiliaji unaoeleweka, ili kufuatilia maendeleo na kupunguza ucheleweshaji wowote unaoweza kutokea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *