
MSHAMBULIAJI wa Namungo, Pius Buswita amekiri msimu huu amekuwa na wakati mgumu katika kasi ya kutupia mipira nyavuni, lakini amesema kama hataifikia rekodi ya msimu uliopita ya mabao saba, basi hata akimaliza na matano kupitia mechi zilizosalia kwake itakuwa freshi tu.
Kwa sasa nyota huyo wa zamani wa Mbao na Yanga, ana mabao matatu na asisti tatu, akiwa na deni ya mabao manne ili kuifikia rekodi binafsi ya msimu uliopita alipomaliza na saba, huku Namungo ikiwa na mechi nne za kufungia msimu na nyota huyo amesema anapaswa kupambana kuweka heshima.
Buswita alisema kiu yake ni kutomaliza msimu chini ya mabao manne, ndio maana ameanza kupiga hesabu kwa mechi zilizosalia ili angalau afunge mabao mawili au zaidi na sio kusalia hapo alipo sasa.
Katika mechi 21 katia ya 26 ilizocheza Namungo, Buswita amefunga mabao matatu na asisti tatu akiwa mmoja ya wachezaji wenye mabao mengi wa timu hiyo inayiopambana kuepuka kushuka daraja au kuangukia katika play-off.
“Nimecheza mechi 21 mbili nilianzia benchini, zilizobakia nilikuwa naanza ila sio kumaliza dakika 90 zote, mwanzo wa msimu ndoto yangu ilikuwa nikuvunja rekodi yangu ya mabao saba, cha ajabu hadi sasa nimeshindwa kuyafikia,” alisema Buswita na kuongeza;
“Ligi ya msimu huu imekuwa ngumu, lakini bado sijakata tamaa, kama nitashindwa kuyafikia angalau nimalize msimu nikiwa na mabao matano maana kwa asisti msimu uliopita nilikuwa nazo tatu kama ninazomiliki sasa.”
Nje na malengo yake binafsi alisema kila mchezaji anapambana kuhakikisha timu inasalia Ligi Kuu, kwa sababu nafasi ya 11 anaiona bado haipo salama ikiwa imeshinda saba, sare saba, imefungwa michezo 12, pointi 28.
“Japo tumepambana ila bado, tunahitaji kumaliza mechi kwa umakini mkubwa ili kujihakikishia usalama wa kusalia ama kukwepa kucheza mtoano,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Yanga.
Namungo imesaliwa na mechi nne za kumaliza ligi dhidi ya Mashujaa nyumbani Majaliwa, Ruangwa, kabla ya kuifuata Yanga kisha nyumbani dhidi ya Kagera Sugar na KenGold.