Kocha Mwingereza aitabiria Simba makubwa

KOCHA wa zamani wa Simba, Dylan Kerr aliyepo kwa sasa Marekani kwa mapumziko, ameshindwa kujizuia na kuwatabiria Wekundu wa Msimbazi kufika fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika akitaja sababu zitakazowabeba mbele ya Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Kocha huyo aliajiriwa na Simba katikati ya msimu wa 2014-2015 kisha kutimuliwa baada ya kupoteza ubingwa wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2016 akiicha Simba ikishika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2015-2016 ambapo Yanga ilitetea ubingwa.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Marekani, Kerr amesema amekuwa akiifuatilia Simba na kubaini imetinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza na itakumbana na Stellenbosch ya Afrika Kusini, nchi aliyowahi kufundisha soka kwa muda mrefu.

Kerr amesema hiki ndicho kipindi ambacho Simba wanapaswa kuwa ‘laser-focused’ na nishati ya kushiriki michuano mitatu tofauti kwa wakati mmoja ni jambo ambalo linahitaji akili kubwa na umoja wa kweli.

Kwa sasa, Simba ipo katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, nusu fainali ya Kombe la FA Tanzania, na nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiifukuzia ubingwa kwa karibu dhidi ya Yanga.

Kocha huyu amesema ni jambo linalowapa nafasi ya kufanya makubwa: “Hii ni fursa ya dhahabu. Huwezi kujua lini utakuwa tena katika nafasi kama hii. Lakini sharti la kwanza ni kuwaheshimu wapinzani wote, bila kujali jina au kiwango chao kuupa uzito kila mchezo,” alisema kocha huyo Mwingereza na kuongeza;

“Rotation lazima iwe ya kimkakati. Unawapumzisha nani dhidi ya nani? Je, ni mechi ya FA au ya nyumbani CAF? Hizi ni hesabu ambazo benchi la ufundi linatakiwa kuwa nazo usiku na mchana.”

Mbali na mbinu za uwanjani, Kerr amegusia jambo la tatu ambalo kwa maoni yake ndilo msingi wa yote ni umoja:  “Wachezaji, benchi, viongozi, mashabiki wakati kama huu, huu ndiyo wakati wa kushikamana kama Simba moja. Hamna nafasi ya lawama wala migongano. Huu ni wakati wa moyo mmoja, sauti moja, Simba moja na wakipenya hapo hawatakuwa na kizuizi tena,” alisema kocha huyo.

Kuhusu kocha wa sasa wa Simba, Fadlu Davids, kocha Kerr hakuficha pongezi zake: “Ni kocha mzuri sana. Huu ni msimu wake wa kwanza na tayari amefanya mambo makubwa. Ni vigumu sana kuingia klabu kama Simba, yenye matarajio makubwa, halafu ukaleta utulivu kama huu ndani ya muda mfupi. Namuona akifika mbali katika michuano yote anayoshiriki.”

Katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba itakutana na Stellenbosch ya Afrika Kusini Jumapili hii ya Aprili 20 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kabla ya kurudiana tena ugenini wiki moja baadaye huko Afrika Kusini.

Wekundu hao wametinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) kwa kuing’oa kwa mabao 3-1 Mbeya City na sasa inajiandaa kuvaana na Singida Black Stars iliyoitupa nje Kagera Sugar kwa mabao 2-0 mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, mjini Babati mkoani Manyara.

Mshindi wa mechi hiyo ya nusu fainali ya Shirikisho la Tanzania, atavaana na mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Yanga na JKT Tanzania itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga kusaka ubingwa ambao kwa misimu mitatu mfululizo unashikiliwa na Yanga.

Katika Ligi Kuu, Simba inachuana na watetezi Yanga iliyotofautiana nayo pointi 10, Yanga ikiongoza na pointi 67 kupitia mechi 25 ilihali Simba ikiwa imecheza mechi 22 na kuvuna pointi 57 mbali na kiporo cha Dabi ya Kariakoo iliyoshindwa kupigwa Machi 8 mwaka huu baada ya Bodi ya Ligi kuiahirisha.

Kama kila timu itashinda mechi zote nane zilizosalia ikiwamo kiporo cha Dabi itafikisha pointi 81, mbili zaidi na itakazomalizia nazo Yanga kama itapoteza Dabi kwa vile itafikisha 79 tu, lakini kama Simba itapoteza Dabi itafunga hesabu ikiwa na pointi 78 dhidi ya 82 za Yanga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *