UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2024/25, UJENZI WA BARABARA ZA LAMI WAONGEZEKA KWA ASILIMIA 71

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kuwa urefu wa barabara za Vijijini na Mijini zilizojengwa kwa kiwango cha lami umeongezeka  kutoka kilomita 2,025 hadi kilomita 3,467.30 sawa na asilimia 71.22.

Hayo ameyasema leo Aprili 16, 2025 wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2025/26 Bungeni, jijini Dodoma.

Kwa upande wa ujenzi wa barabara za changarawe Mhe. Mchengerwa amesema kuwa umeongezeka kutoka kilomita 24,493 hadi kilomita 44,372.21 sawa na asilimia 81.16 na kuongeza mtandao wa barabara kutoka kilomita 108,946.19 hadi kilomita 144,429.77 sawa na asilimia 32.57.

kuhusu matumizi ya teknolojia mbadala katika ujenzi wa Miundombinu ya barabara Mhe. Mchengerwa amelieza bunge kuwa barabara zenye urefu wa kilomita 61.7 zinaendelea kufanyiwa tafiti Ili kupunguza gharama za ujenzi, matengenezo na ukarabati.

“tulipotoka kulikuwa na vumbi, lakini leo tunatembea kwenye lami.  Tulipotoka kulikuwa na miteremko isiyopitika, leo tuna barabara zinazounganisha ndoto na fursa. 

Kuongezeka Kwa barabara za changarawe kwa asilimia 81.16 na lami kwa asilimia 71.22 ni ushahidi wa nchi inayojenga msingi wa maendeleo kwa kila mtanzania, kuanzia kijijini hadi mjini. Huu sio Mradi wa barabara tu, huu ni Mradi wa matumaini” amefafanua Mhe. Chengerwa.

Mhe. Mchengerwa amebainisha kuwa kila kilomita moja ya barabara ni daraja kati ya umasikini na maendeleo na kuongeza kuwa ni njia ya mtoto kufika shuleni, mama kufika hospitali, mkulima kupeleka mazao sokoni  na taifa kusonga mbele.

Kwa mujibu wa Mhe Mchengerwa kuongeza mtandao wa barabara kutoka kilomita 108,946 hadi zaidi ya kilomita 144,000 si takwimu tu ni mabadiliko ya kweli yanayoonekana, yanayogusika na yanayogusa maisha.

“Barabara hizi ni sauti ya Serikali inayosema: ‘Hatukuwaacha nyuma. Hizi ni njia zinazotufikisha kwenye Tanzania ya viwanda, fursa na mshikamano” ameongeza Mhe. Mchengerwa.

Katika bajeti ya Mwaka wa fedha 2024/25 Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA iliidhinishiwa shilingi bilioni 908.16 kwa ajili ya ujenzi, ukarabati, matengenezo ya barabara na hadi mwezi Machi, 2025 shilingi bilioni 468.40 zimetolewa sawa na asilimia 55.68 ya fedha zilizoidhinishwa.

The post UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2024/25, UJENZI WA BARABARA ZA LAMI WAONGEZEKA KWA ASILIMIA 71 appeared first on Mzalendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *