
Wiki iliyopita, vyama vya siasa, Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) walitia saini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025, ikiwa ni hatua za awali za kuanza kwa mchakato wa uchaguzi.
Wadau hao walikutana jijini Dodoma na kusaini kanuni hizo ambazo baadaye zitatangazwa kwenye gazeti la Serikali kwa ajili ya kutumika rasmi kama mwongozo wa kimaadili kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Kanuni hizo zinatoa mwelekeo wa utekelezaji wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024. Sheria hiyo ni moja kati ya sheria tatu za uchaguzi zilizotungwa na Bunge mwaka jana, nyingine ni Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi.
Kati ya vyama 19 vyenye usajili wa kudumu nchini, ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pekee ndicho hakikuhudhuria shughuli hiyo ya utiaji saini wa kanuni hizo, jambo ambalo limeibua mjadala mzito.
Mjadala huo unatokana na kauli ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Kailima Ramadhan kueleza kwamba kwa kutosaini kanuni za uchaguzi, chama hicho hakitaweza kushiriki uchaguzi mkuu ujao wala chaguzi ndogo zitakazofuata katika kipindi cha miaka mitano.
Kauli hiyo ya Kailima inapata nguvu kutokana na kifungu cha 1.5(a) cha kanuni hizo kinachoeleza kuwa: “Kila chama cha siasa, Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi watawajibika kusaini Kanuni hizi za Maadili. Chama cha siasa ambacho hakitasaini Kanuni hizi za Maadili kitazuiliwa kushiriki katika kampeni za uchaguzi.”
Hata hivyo, kifungu hicho cha kanuni, kama wanavyoeleza wanasheria mbalimbali, hakijaweka ukomo wa muda wa kusaini kanuni hizo, hivyo siyo sahihi kuhitimisha kwamba Chadema hakitaruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi kwa sababu hiyo.
Kanuni hizo zinaelekeza katika kifungu (b) kwamba kila mgombea, kabla ya kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi atathibitisha kuheshimu na kutekeleza kanuni hizo kwa kujaza na kusaini Fomu Namba 10 iliyoainishwa mbele ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kadiri itakavyokuwa.
Kifungu hicho kinaeleza kwamba fomu hiyo itatolewa na Tume au msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi na itarejeshwa pamoja na fomu ya uteuzi.
Baadhi ya vifungu vya Kanuni ya Maadili ya Uchaguzi vinavibana vyama vya siasa, wagombea na Serikali, kila upande ukitakiwa kutimiza wajibu wake wakati wa uchaguzi bila kuathiri ufanisi wa uchaguzi huo.
Kibano kwa vyama, wagombea
Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025 zinatoa angalizo kwa maeneo ambayo yamekuwa yakitumiwa vibaya na vyama vya siasa au wagombea.
Yafuatayo ni maeneo yanayoangaziwa kwenye kanuni hiyo.
Kifungu cha 1.5(n) kinavielekeza vyama kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili itakuwa ndiyo lugha itakayotumika katika kampeni za uchaguzi.
Iwapo lugha hiyo haieleweki, na itakapolazimu, mgombea atazungumza katika lugha ya Kiswahili na mkalimani atatafsiri katika lugha inayoeleweka kwa jamii husika.
Kadhalika, kifungu cha 2.2(b) kinavionya vyama na wagombea kutumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli, udhalilishaji na vitisho au lugha inayochochea uvunjifu wa amani au kuashiria ubaguzi wa kijinsia, ulemavu, rangi au maumbile kwenye mikutano na kwenye shughuli zote za kampeni.
Kifungu 2.2(c) kinakataza kufanya kitendo chochote cha unyanyasaji au ukatili wa kijinsia kwa mgombea kinyume na masharti ya kifungu cha 135 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya mwaka 2024.
Moja ya mambo yanayojitokeza ni kubanduliwa kwa matangazo ya wagombea. Kifungu cha 2.2(h) kinakataza kubandua, kuharibu au kuchafua matangazo ya kampeni ya vyama vingine vya siasa na matangazo ya uchaguzi yanayotolewa na Tume au kutumia viongozi, wanachama au wafuasi wao kufanya hivyo.
Vilevile, kifungu kidogo cha (i) kinapiga marufuku kubandika mabango ya kampeni, matangazo au michoro yoyote kwenye nyumba, majengo au vyombo vya usafiri vya watu binafsi au taasisi mbalimbali bila idhini ya wamiliki husika.
Mambo mengine yanayokatazwa ni pamoja na kukosoana kwa tuhuma zisizokuwa na uthibitisho bali ukosoaji ujikite katika sera, programu na kazi zao walizofanya; na kutumia mitandao ya kijamii kufanya kampeni za chuki, uchochezi, udhalilishaji au ubaguzi wa kijinsia.
Onyo kwa Serikali
Mbali na kanuni hizo kutoa makatazo kwa vyama vya siasa na wagombea wao, kanuni hizo za maadili zinaielekeza pia Serikali wajibu wake na kuepuka baadhi ya mambo. Mambo yasiyotakiwa kufanywa na Serikali wakati wa uchaguzi ni pamoja na:
Kifungu cha 3.2 (a) kinaikataza Serikali kuingilia au kuzuia isivyo halali mikutano iliyoitishwa na vyama vya siasa au wagombea kwa mujibu wa ratiba za uchaguzi.
Kifungu kidogo (b) kinavionya vyombo vya ulinzi na usalama kutumia madaraka yao kukandamiza wagombea, wafuasi au chama chochote cha siasa. Kanuni inavitaka vyombo hivyo vitekeleze majukumu yake kwa weledi.
Pia, kifungu kidogo (c) cha kanuni hiyo kinaikataza Serikali kumhamisha mtumishi yeyote wa Serikali anayehusika na shughuli za uchaguzi mpaka mchakato wa uchaguzi ukamilike.
“Endapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaona kuna ulazima wa kumhamisha mtumishi kama huyo ni lazima ishauriane na Tume,” kifungu hicho kinaeleza.
Wakati huohuo, kifungu cha 3.3(a) kinaeleza mambo ambayo watendaji wa serikali hawapaswi kufanya wakati wa uchaguzi ili kuepusha mgongano wa maslahi.
Mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wanakatazwa kuchanganya ziara za kikazi na shughuli za kiuchaguzi na kutumia vyombo au watendaji wa Serikali katika shughuli za uchaguzi kwa manufaa yao.
Kifungu kidogo (b) kinaelekeza kwamba kuanzia kipindi cha kampeni za uchaguzi hadi kutangazwa kwa matokeo, mawaziri hawaruhusiwi; kwanza, kutangaza katika vyombo vya habari au kwa namna yoyote misaada au ahadi ya aina yoyote.
Pili, kutoa ahadi za shughuli za maendeleo ya jamii kwa mfano, kujenga barabara, kusambaza maji na mambo mengine kama hayo kwa lengo la kuungwa mkono kisiasa; na
Tatu, kutumia madaraka au rasilimali za Serikali kwa shughuli za kampeni za uchaguzi kwa manufaa ya chama chochote cha siasa au mgombea yeyote.
Tume nayo yamulikwa
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, kama mdau katika uchaguzi ujao, nayo inaangaziwa katika kanuni hizo huku ikikumbushwa wajibu wake wa msingi na kuelekezwa kuepuka baadhi ya mambo kwenye uchaguzi.
Mambo yasiyotakiwa kufanywa na Tume kwa mujibu wa kifungu 4.2 ni pamoja na: kupendelea chama chochote cha siasa au mgombea yeyote; kubadili ratiba za kampeni za uchaguzi bila kushirikisha vyama vya siasa.
Mambo mengine ni kuchelewa au kupeleka vifaa pungufu katika vituo vya kupigia kura bila sababu za msingi, kuchelewa kufungua vituo bila sababu ya msingi; na kuchelewa kutangaza matokeo ya uchaguzi bila sababu za msingi.
Azichambua kanuni
Mchambuzi wa siasa, Buberwa Kaiza anabainisha kwamba kanuni zilizosainiwa na vyama vya siasa hazielezi namna wadau walioshiriki kusaini kanuni hizo, kwa maana ya Tume, Serikali na vyama vya siasa, watakavyoadhibiwa endapo watakiuka kanuni hizo.
“Serikali ikikosea, polisi wakikosea, utaiwajibisha wapi? Tume ikikosea utaiwajibisha wapi? Kwa hiyo, tafsiri ya kanuni hizo ni kwamba kanuni zote kwa ujumla zinaweka ustaarabu wa kisiasa, haikusudii kuadhibu chama chochote wala kuadhibu upande wowote uliotia saini.
Anaongeza kwamba kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani hakijaonyesha kwamba kuna siku maalumu ya kusaini kanuni na kwamba wanatakiwa wawepo wote wasaini.
Kaiza anasema kanuni inayoelekeza kwamba chama ambacho hakijasaini kanuni hizo hakitashiriki uchaguzi, kinakiuka sheria hiyo ambayo inatekelezwa na kanuni hizo, hivyo hazipaswi kutofautiana.
“Uchaguzi siyo wa Tume, Serikali au vyama vya siasa, uchaguzi ni wa raia. Raia ndio wanaamua kuchagua ama kutochagua. Shughuli zote zinazofanyika zinalenga kumwezesha raia kuchagua viongozi wake,” anasema.
Anasisitiza kwamba kupiga kura ni haki ya kisiasa ya kila raia na haki hiyo haiwezi kuondolewa kwa mamlaka ya mtu mmoja.
Anasisitiza kwamba haki hiyo inapaswa kulindwa na kila mtu kwa kuwa ni haki ya msingi ya kikatiba.
Maoni ya ACT Wazalendo
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, chama hicho kinaangazia baadhi ya vifungu vya kanuni hizo na kutoa mapendekezo yao ili mchakato wa uchaguzi uende vizuri kwa namna wanayoona ni bora zaidi.
Kuhusu muda wa kuanza na kumaliza kampeni na matangazo ya kampeni, ACT Wazalendo kinapendekeza muda wa kumaliza mikutano ya kampeni iwe saa 12:45 jioni na muda wa kutoa matangazo ya mikutano itakayofuata iwe mwisho saa 4 usiku.
Suala la kukutana kwa misafara ya vyama wakati wa kampeni, chama hicho kinapendekeza kifungu hicho kifutwe kwa sababu hakitekelezeki.
Wanasema ni vigumu kwa misafara ya kampeni, hasa za ubunge na udiwani isikutane.
ACT Wazalendo inapendekeza Tume kuhakikisha mawakala wanakuwa huru kukagua vitambulisho na vifaa vya uchaguzi.
Pia, ihakikishe upigaji kura unakuwa kwenye mazingira ambayo mpiga kura anaonekana bila kuathiri faragha yake ya kupiga kura.
Kuhusu wapigakura kutakiwa kuondoka eneo la tukio, chama hicho kinapendekeza kifungu hicho kiboreshwe kwa kutakiwa wapigakura kukaa umbali wa mita 100 baada ya kupiga kura ili washuhudie kutangazwa kwa matokeo ya kura.
“Marufuku hii inaweza kutumika na vyombo vya ulinzi na usalama kuumiza raia wema ambao wamekuja kufuatilia matokeo ya uchaguzi,” inaeleza taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Shaibu.