CCM yapangua ratiba uchukuaji fomu ubunge, uwakilishi na udiwani

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza mabadiliko ya ratiba ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba kuwania udiwani, uwakilishi na ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Taarifa kwa umma iliyotolewa usiku wa kuamkia leo Jumatano, Aprili 16, 2025 na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi imeeleza uamuzi wa kubadili ratiba hiyo umetokana na mashauriano na wanachama wake na kutafakari kwa kina hivyo, kimeamua kusogeza mbele ratiba hiyo.

Dk Nchimbi amesema shughuli hiyo sasa itaanza Juni 28 hadi Julai 2, 2025 saa 10 jioni.

Fomu hizo zitakuwa kwa makatibu wa jumuiya  za chama hicho zikiwamo UWT, UVCCM na Wazazi ngazi za mikoa kwa nafasi ya  viti maalum za ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Uwakilishi, fomu hizo zitatolewa na Makatibu wa CCM wa wilaya.

Ratiba iliyotolewa Aprili 10, 2025 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ilieleza  uchukuaji na urejeshaji wa fomu hizo ungeanza Mei Mosi hadi 15, 2025.

Mabadiliko hayo yanamaanisha shughuli hiyo sasa itakuwa ya siku tano pekee kuanzia Juni 28- Julai 2, 2025 badala ya siku 15 zilizotangazwa awali.

Kwa ratiba ya sasa, ina maana fomu hizo zitaanza kutolewa siku moja kupita tangu Rais wa Tanzania kulihutubia Bunge la 12 na kulivunja Juni 27, 2025.

Hivi karibuni, Dk Nchimbi alionekana akifanya vikao ofisini kwake, makao makuu ya CCM, Dodoma na mwenyekiti wa kamati ya wabunge wa CCM ambaye ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Kikao hicho kilichofanyika Aprili 11, 2025 kilihuduhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Bara wa CCM, John Mongella. CCM ikitoa picha pekee bila maelezo ya nini kilizungumzwa.

Aidha, siku tatu baadaye yaani Aprili 14, 2025, Dk Nchimbi alifunga safari hadi visiwani Zanzibar kwenda kuonana na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Rais Hussein Mwinyi.

Kikao hicho kilifanyikia Ikulu ya Zanzibar na kuhudhuriwa pia na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa.

Katika picha iliyowaonyesha viongozi hao wakiwa pamoja,  CCM ilieleza kuwa  viongozi wa CCM wakutana pasipo kueleza kwa kina ama uchache malengo ya kukutana kwao.

Hata hivyo, mmoja wa kiongozi mwaandamizi wa CCM aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina amesema moja ya sababu ya kusogeza mbele ni kutoa nafasi kwa wabunge na wawakilishi kutekeleza majukumu yao wakati huu wa bajeti kwa ufanisi.

“Kama tungeacha ratiba ya awali ya Mei 1-15, utulivu usingekuwepo kwa wabunge na wawakilishi. Akili zao zingekuwa majimboni tu, kwa sababu ushajua fulani na fulani wamechukua fomu unafikiri unaweza kukaa kwa amani bunge ni. Na kwa sababu hiyo ndiyo maana imeonekana isogezwe mbele,” amesema kiongozi huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *