Wanawake wanaopenda kubusu ndevu hatarini

Dar es Salaam. Katika jamii nyingi, ndevu zimekuwa ishara ya uanamume, mvuto na hata heshima.

Wanawake wengi huvutiwa na wanaume wenye ndevu nadhifu na nzuri.

 Hata katika utafiti uliochapishwa na tovuti ya VWO testing inayojihusisha na masuala ya mitindo kwa wanaume kupitia mfumo walioupa jina la A/B testing, umebaini kuwa wanawake wengi  huvutiwa sana na wanaume wenye videvu vyenye ndevu kuliko wale wasiokuwa nazo.

Utafiti huo ulifanywa kwa njia ya mtandao kwa siku 15 kupitia tovuti hiyo kwa kuweka picha mbili; moja ikiwa ni ya mwanaume mwenye ndevu na nyingine ya asiye na ndevu.

Asilimia 70 ya walioshiriki katika utafiti huo wanaokisiwa kuwa ni wanawake, walieleza kuvutiwa zaidi na wanaume wenye ndevu kuliko wale wasio na ndevu huku wakibainisha sababu mbalimbali.

Hivyo si jambo la kushangaza kuona baadhi yao wakipenda kuwabusu au wenza wao mara kwa mara ndevu zikiwa sehemu ya mvuto huo.

Busu la hatari

Hata hivyo, licha ya mvuto huo wa kimapenzi, kwa mujibu wa maandiko mbalimbali ya afya, kuna hatari zinazoweza kuambatana na tabia hiyo kama ndevu za mwanaume huyo hazitakuwa katika hali ya usafi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na maambukizi ya ngozi na bakteria, kuharibika kwa ngozi ya midomo pamoja na mzio.

Kwa mujibu wa tovuti ya Beard Growing Pro katika moja ya makala yake kuhusiana na umuhimu wa kutunza ndevu, ndevu kama nywele nyingine za mwilini, zinaweza kubeba vimelea mbalimbali kama vile bakteria na fangasi.

Katika makala hiyo amenukuliwa mmoja wa wataalamu wa maabara aliyewahi kuhojiwa na kituo kimoja cha televisheni huko New Mexico Marekani,  ambaye alisema kuwa ndevu zisipotunzwa na kuzingatiwa usafi zinaweza kuwa na kiwango cha bakteria sawa au hata zaidi kuliko choo cha umma.

“Busu kwenye ndevu zisizo safi husababisha maambukizi ya ngozi kwa wanawake, hasa kwenye midomo, mashavu, au maeneo ya karibu”imeeleza sehemu ya makala ya tovuti hiyo.

Pia imeeleza kuwa ndevu zinapokaa muda mrefu bila kusafishwa vizuri, zinaweza kuwa na uchafu, mafuta, au vipande vya chakula hivyo kuwabusu wanaume wenye ndevu zisizo safi, huongeza uwezekano wa kuathiri ngozi ya midomo, ambayo ni nyororo sana na rahisi kupata maambukizi.

“Baadhi ya wanawake wanaweza kuwa na mzio na bidhaa ambazo mwanaume amepaka katika ndevu zake kwa ajili ya kutunzia ndevu kama mafuta au manukato ya ndevu, hivyo kuwabusu wanaume walio na bidhaa hizo kunaweza kusababisha muwasho, vipele, au hata uvimbe katika maeneo ya uso,”imesema.

Katika moja ya makala iliyochapishwa katika tovuti ya gazeti la Taifa Leo, daktari na mtaalamu wa afya, Dk Myro Figura ametahadharisha dhidi ya kuwapiga busu wanaume wenye ndevu, akisema hatua hiyo inaweza kukusababishia maambukizi na muwasho kwa ngozi.

Kutokana na hilo amewataka wanawake wanaobusu wanaume wenye ndevu wajihadhari, kwa sababu hiyo ni njia moja ya kujiletea maradhi.

“Kupiga busu mwanamume mwenye ndevu kunaweza kukusababishia maradhi. Kama ndevu zenyewe si safi huwa ni hifadhi ya bakteria, na wakati wa kupiga busu vijidudu hivyo hatari vikigusana na ngozi basi huleta ugonjwa wa upele wa malengelenge (impetigo),” anasema Dkt Figura.

Impetigo ni ugonjwa wa ngozi ambao unasambaa kwa urahisi.Huanza kwa ngozi kuwa na uvimbe kisha kutoa uchafu mwekundu. Unaweza kuupata ikiwa utagusana na mwenye ugonjwa huo kwa kupitia ngozi au nywele zikiwamo ndevu.

“Uvimbe ukipasuka huacha vidonda vidogo na husambaa sehemu mbalimbali za mwili. Kibaya zaidi ni kuwa aliyeathirika hujikuna sana na kuhisi uchungu kutokana na mwasho,” aongeza mtaalamu huyo katika utafiti uliochapishwa kwenye jarida la habari la Daily Mail nchini Uingereza.

Tiba ya maambukizi haya ya bakteria ni kupaka mafuta yenye kemikali ya ‘hydrogen peroxide’ ama kumeza tembe za kukabiliana na bakteria mwilini.

Anachosema daktari wa ngozi

Akizungumza na Mwananchi,  daktari wa ngozi kutoka hospitali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Tumpale Luhanga amesema inawezekana kwa mwanamke anayependa kubusu ndevu za mwanaume wake kupata maambukizi ya bakteria na ngozi kama mwanaume huyo atakuwa hazingatii usafi na kuzitunza ngozi.

“Hili linaweza kutokea japo hujitokeza kwa uchache hasa pale mwanaume anapokuwa sio makini wa usafi wa ndevu zake,”amesema.

Ushauri kwa wenye ndevu

Kwa mujibu wa tovuti ya Beard Growing Pro,  wanaume kama wanavyozingatia kuoga na kuvaa nguo safi , pia wanapaswa kuzipa  kipaumbele ndevu zao, kwa kuhakikisha wanaziosha kwa sabuni au shampoo mara kwa mara ili kuondoa uchafu na vijidudu.

Pia wanaaswa kutumia bidhaa  za mafuta ambazo ni salama  na azisizo na kemikali kali kwa ajili ya kutunza ndevu hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *