UCHAMBUZI WA SARAMBA: Watanzania tupige kelele kukemea ‘ukaburu’

Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kufichua kuwa mara zote alikuwa akibeba na kusoma kwa kurejea mara kadhaa Biblia Takatifu na kitabu cha Azimio la Arusha.

Naamini Mwalimu Nyerere alitembea na Biblia kwa sababu ya imani yake ya Kikristo; na kuhusu kitabu cha Azimio la Arusha, nadhani alifanya hivyo kutokana na kuamini na kuishi misingi yake. Haki na usawa kwa wote.

Kwa imani, malezi na makuzi, nami nimejikuta nikisoma na kurejea Biblia Takatifu mara kwa mara kama ninavyofanya kwa kitabu cha Azimio la Arusha pamoja na zile Ahadi 10 za Mwanatanu; na kote huko nakutana na maonyo dhidi ya dhuluma na nasaha kuhusu haki, utu upendo na usawa kwa wote.

Kwa leo, nitajikita katika Ahadi saba kati ya 10 za Mwanatanu, nikianza na ya kwanza inayosema; “Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika (soma Tanzania) ni moja.’’

Ahadi ya pili inasema; “Nitatumikia nchi yangu (Tanzania) na watu wake wote (bila ubaguzi wala upendeleo wa aina iwayo yote).’’ Katika ahadi ya tatu tunaaswa kujitolea kupiga vita maadui wanne kwa kusema; “Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa (maradhi) na dhuluma (uonevu, ubaguzi, upendeleo n.k).”

Katika ahadi ya tano, tunakumbushwa kwamba; “Cheo ni dhamana, sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.’’

Kuhusu ujenzi wa Taifa, ahadi ya saba inasema; “Nitashirikiana na wenzangu wote (bila kujali tofauti za itiadi za kisiasa, kidini, kikabila wala maeneo ya Kijiorafia) kujenga nchi yetu (Tanzania).”

Kwenye uaminifu, ahadi ya nane inasisitiza kwamba; ‘’Nitasema kweli daima. Fitina kwangu mwiko,’’

Nimenukuu ahadi za Mwanatanu kujenga hoja yangu kuhusu hatari ya tabia, hulka na vitendo vya kikaburu vinavyoanza kumea na kuota mizizi katika jamii na Taifa letu kwa jumla.

Katika umri wangu wa utoto nikiwa shule ya msingi, tulifundishwa na hata kuimba nyimbo kadhaa za kuonyesha ubaya wa makaburu wa Afrika Kusini.

Hatukuimba na kulaani ukaburu pekee, bali pia Tanzania tuliunga mkono kwa hali, mali, jasho na damu vita dhidi ya ukaburu Afrika Kusini na duniani kote. Kwetu, ukaburu (ubaguzi wa aina yoyote) ulikuwa ni unyama. Kama alivyowahi kusema Hayati Baba wa Taifa, kamwe hatukuwapinga makaburu kwa sababu ya rangi zao. La hasha! Tulipinga tabia, maneno na matendo yao. Ubaguzi.

Lakini japo la kusikitisha, Watanzania tumeanza kusikia, kuona na kutenda yale tuliyoyapinga.

Tumeanza ukaburu kwa kubaguana kwa misingi ya tofauti zetu kidini, kisiasa, kikabila na hata kwa maeneo yetu ya Kijiografia.

Watanzania tumeanza kutamba na kujivunia itikadi zeti kidini, kisiasa na hata makabila na maeneo yao ya kijiografia.

Zamani tuliulizana makabila yetu ili tutaniane, lakini sasa tunaulizana ili kujua yupi ni wa kwetu na nani siyo wetu.

Cheo siyo dhamana tena. Viongozi wetu hawaoni soni kujinufaisha wao wenyewe, ndugu, jamaa na marafiki zao kwa kutumia vyeo vyao au vya wengine. Ni aibu!

Watanzania wa Mwalimu Nyerere wamewahi kunyukana kugombea nani achinje na nani asichinje. Sijui nani katuloga?

Kwenye uwanja wa siasa, tunawafanyia mizengwe na kuwaengua wagombea wasio wa upande wetu na wale wachache wanaopenya tunamalizana nao wakati wa kupiga, kuhesabu kura na kutangaza matokeo.

Kwa lugha yao wanadai eti wanaochagua viongozi wa kisiasa wanaopigiwa kura siyo wapigakura, bali wale wanaohesabu na kutangaza matokeo. Hapo ndipo tunasikia msamiati wa goli la mkono.

Wenye dhamani ya kugawa keki ya Taifa wanathubutu kufanya ukaburu kwa ama kusuasua au kutopeleka kabisa mafungu ya maendeleo katika maeneo ambayo wananchi wametumia haki yao kikatiba kuchagua wasio wa upande wao.

Dhambi ya ukaburu inatafuna hadi eneo la utoaji wa haki na usimamizi wa sheria. Wale wa kada tawala siyo tu wanajihesabia haki, bali pia haki hukaa upande wao hata pale wasipostahili.

Ukiwa nje ya kada tawala ukajishibia ugali au wali wako kwa maharagwe kamwe usithubutu kujiropokea eti utakinukisha kudai mabadiliko; halali yako itakuwa korokoroni.

Waropokaji wanaoketi meza kuu wenyewe wako salama hata pale wanapoibua taharuki kwa kutaja magonjwa hatari yanayotikisa dunia.

Kila Mtanzania mwenye mapenzi mema asimame ahesabiwe kwa kupiga kelele kuonya dhidi ya ukaburu unaotunyemelea.  Tusipopiga kelele mawe yatainuka kupiga kelele.

Peter Saramba ni mwandishi wa kujitegemea, anapatikana kwa simu namba 0766434354.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *