
KATIKA hali isiyo ya kawaida kwa timu mbili zilizo katika nafasi tofauti kabisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, Tabora United na KenGold zimejikuta kwenye mkondo mmoja wa matokeo baada ya kukumbana na vipigo mfululizo.
Tabora United, ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 37, haijapata alama hata moja katika mechi tatu za mwisho ikipoteza zote dhidi ya Mashujaa (3-0), Pamba Jiji (1-0) na Yanga (3-0).
Hali hiyo inazua maswali mengi kwa timu hiyo ambayo ilikuwa kwenye kiwango bora ikipambania nafasi nne za juu kabla ya malengo hayo kutibuka.
Kwa upande mwingine, KenGold ambayo inashika mkia kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 16, katika mechi 26, inaonekana kupoteza mwelekeo kabisa na sasa iko hatarini kuwa timu ya kwanza kushuka daraja msimu huu.
Timu hiyo yenye maskani Chunya mkoani Mbeya, imepata vipigo vitatu mfululizo dhidi ya Tanzania Prisons (3-1), Dodoma Jiji (3-0) na Azam FC (2-0) ambavyo vimezidi kuiweka pabaya, na matumaini ya kupona yanazidi kuyeyuka.
Tabora na KenGold ndiyo timu pekee ambazo zimepoteza mechi zote tatu za mwisho katika ligi, huku Azam FC, Fountain Gate, Coastal Union, KMC na Kagera Sugar zikipoteza mechi mbili kati ya tatu zilizopita. Hili linaashiria kuwa kuna sintofahamu kubwa katika viwango vya timu kadhaa, siyo zile tu zilizo mkiani.
Licha ya kuwa na tofauti kubwa ya pointi, hali ya kupoteza mechi mfululizo inatoa ujumbe kuwa Tabora United haiwezi kujiona iko salama kabisa, hasa kama mwelekeo huu mbaya utaendelea katika raundi nne zilizobaki.
Kwa KenGold, mechi zao mbili zijazo dhidi ya Coastal Union ugenini na Pamba Jiji nyumbani, zinaweza kuamua hatima yao. Kushindwa kupata ushindi katika mechi hizo kunaweza kuwa ndiyo sababu ya kushuka daraja na kurejea Champioship.
Wakati hayo yakiendelea, Tanzania Prisons wameonyesha dhamira ya kupambana kusalia ligi kwa kuvuna pointi sita katika mechi tatu zilizopita, jambo lililowasaidia kupanda kutoka nafasi ya 15 hadi 14 wakiwa na pointi 24.
Ikiwa wataendelea na kasi hiyo katika mechi mbili zijazo dhidi ya JKT Tanzania na Coastal Union zote nyumbani, wanaweza kujinasua kabisa kutoka kwenye mstari wa kushuka daraja.
Kwa upande wa mafanikio, Yanga SC inaongoza kwa kuwa timu pekee iliyoshinda mechi zote tatu za karibuni, ikifuatiwa na Simba SC na Dodoma Jiji ambao kila mmoja amevuna pointi saba katika kipindi hicho.
Kwa ujumla, mzunguko huu wa ligi umeonyesha wazi kuwa kuporomoka kwa kiwango hakuchagui timu iwe juu au chini. Tabora United na KenGold ni ushahidi kuwa soka halina fomula moja na ni nidhamu ya ushindani pekee inayotofautisha waliodumu juu na wanaopotea taratibu.