Nabi avujisha faili la Wasauz, Fadlu ashindwe mwenyewe

KUNA sababu tatu ambazo kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi amezitaja ambazo zinaipa Simba nafasi kubwa ya kuitoa Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Nabi ambaye kwa sasa anaifundisha Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, amesema anawafahamu vizuri Stellenbosch kwani hivi karibuni amecheza nao mara tatu na kuwapiga nje ndani.

Kocha huyo raia wa Tunisia, katika mechi hizo tatu alizocheza dhidi ya Stellenbosch na kushinda zote, mbili za Ligi Kuu Afrika Kusini na moja Kombe la Nedbank hatua ya robo fainali.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi aliyeifundisha Yanga kuanzia Aprili 20, 2021 hadi Juni 15, 2023, alisema tangu afike Afrika Kusini na kuanza kuifundisha Kaizer Chiefs kuanzia Julai Mosi 2024 amekutana na Stellenbosch mara tatu na kubaini ni timu isiyotabirika ikiwa na kikosi kizuri.

Mbali na kubadilika huko, lakini Nabi amesema hawapo imara sana kwenye ulinzi huku wakitegemea zaidi eneo la mbele kuwabeba.

Kocha huyo amefichua kwamba, kutokana na udhaifu Stellenbosch na uimara wa Simba katika kushambulia, kuna uwezekano wakafanya vizuri, huku pia akilitaja benchi la ufundi la Simba chini ya Fadlu Davids kuwa na Wasauzi wengi inaweza kuwabeba. Pia akasema uzoefu wa Simba kimataifa unawabeba.

“Simba wana uzoefu mkubwa kwenye mashindano ya Afrika, kuliko Stellenbosch, ukizingatia ina wachezaji wenye uzoefu mkubwa hasa kwenye mechi kubwa.

“Kwa kuwashauri Simba, ni kwamba wanatakiwa kuwa makini wasiwadharau wapinzani wao, wanaweza kushtuliwa kama ilivyo tokea kwa Zamalek,” amesema Nabi.

Stellenbosch waliowatoa Zamalek hatua ya robo fainali kwa kuifunga bao 1-0 kwao Misri, walishangaza wengi kutokana na kuwakazia Waarabu hao walipocheza Afrika Kusini na matokeo kuwa 0-0.

Nabi alianza kukutana na Stellenbosch Januari 8, 2025 akashinda 2-1 nyumbani, kisha akaenda ugenini Februari 7, 2025 na kushinda 1-0, hizi zikiwa ni mechi za ligi, kisha ya tatu pia ugenini Machi 8, 2025 katika Kombe la Nedbank akashinda 3-1.

FAIDA IKO HAPA

Katika hatua nyingine, Nabi amesema Simba wana faida kubwa ya kufanya vizuri mbele ya Stellenbosch kutokana na uwepo wa Kocha Fadlu Davids ambaye ni raia wa Afrika Kusini, sambamba na wasaidizi wake wanaotokea nchi hiyo ambao ni Darian Wilken (Kocha Msaidizi), Wayne Sandiland (Kocha wa Makipa), Riedoh Berdien (Kocha wa Fitness) na Mueez Kajee (Mchambuzi wa Video).

“Faida kubwa kwa Simba wana Fadlu na makocha wengine wanaotoka Afrika Kusini, ni rahisi kutegua mitego yote migumu ambayo wapinzani wao wanaweza kuiweka.

“Lakini pia, nao (Stellenbosch) wana kocha mzoefu (Steve Barker) anayemjua Fadlu, kwa hiyo atakayefanya makosa ataumia, kwani hizi ni timu ambazo zinafahamiana vizuri kupitia makocha wao,” amesema.

UIMARA, UDHAIFU

Kocha huyo ameendelea kufichua maeneo ambayo Stellenbosch ni imara na dhaifu na kama Simba itayatumia vizuri, itawashinda kirahisi kutokana na Wekundu hao wa Msimbazi kuwa na rekodi nzuri za kufunga na kujilinda.

“Wapinzani wa Simba wako imara kwenye maeneo mawili na yote ni ya mbele ambayo ni kiungo na safu ya ushambuliaji. Kuna wakati wana makosa mengi kwenye ulinzi, ila bado wako vizuri ndio maana wanashika nafasi za juu kwa upande wa ligi,” amesema Nabi. Katika Ligi Kuu Afrika Kusini msimu huu kabla ya mchezo wao dhidi ya Amazulu, Stellenbosch ilikuwa imeshuka dimbani mara 22, imefunga mabao 27 na kuruhusu 17, huku ikifikisha pointi 35. Kimataifa, Stellenbosch imefunga mabao 18 na kuruhusu 11 katika mechi 12. Jumla imefunga mabao 38 na kuruhusu 28 katika mechi 34.

Kwa upande wa Simba, iko vizuri katika kufunga kwani kwenye ligi imecheza mechi 22 na kutupia mabao 52 ikiruhusu manane, huku kimataifa ikifunga 13 na kuruhusu saba katika mechi 10. Jumla imecheza mechi 32 na kufunga mabao 65 ikiruhusu 15.

REKODI NA WASAUZI

Simba inakutana na Stellenbosch kwa mara ya kwanza huku ikiwa ni mara ya nne kucheza dhidi ya timu kutoka Afrika Kusini katika mashindano ya CAF huku ikiwa na rekodi nzuri inapocheza uwanja wa nyumbani kwani haijawahi kupoteza ikishinda mara zote tatu zilizopita.

Mbali na kuwa na rekodi nzuri ya kushinda nyumbani, lakini Simba imeiondosha mara moja tu timu ya Sauzi katika mtoano huku nyingine ikishindwa kupenya.

Hiyo inaifanya Simba kuwa na mtihani mzito mbele ya Stellenbosch kwani licha ya rekodi yao nzuri ya nyumbani kuwabeba, lakini inahukumiwa na rekodi ya jumla kwa kuvuka hatua inayofuata.

Katika mara tatu zilizopita Simba ilipocheza nyumbani dhidi ya timu kutoka Afrika Kusini, ilishinda kwa penalti 9-8 dhidi ya Santos kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003. Mikwaju hiyo ya penalti iliivusha Simba ambayo ilikwenda kukutana na Zamalek na kuiondosha pia, kisha ikafuzu makundi.

Katika michezo miwili ya mtoano dhidi ya Santos, ilianzia ugenini Aprili 13, 2003 matokeo yakiwa 0–0, kisha marudiano nyumbani ikawa 0-0, ndipo penalti zikaivusha Simba.

Baada ya hapo, Mei 15, 2021, Simba ilikutana na Kaizer Chiefs katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ugenini ilipoteza kwa mabao 4–0, kisha nyumbani Mei 22, 2021 ikashinda 3–0 kwa mabao mawili ya John Bocco dakika ya 24 na 56, huku Clatous Chama akifunga moja dakika ya 86. Licha ya ushindi huo wa nyumbani, lakini haikutosha Simba kuvuka kwenda nusu fainali kufuatia matokeo ya jumla kuwa 4-3.

Aprili 17, 2022, Simba ilikutana na Orlando Pirates katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Simba ilianzia nyumbani na kushinda bao 1-0 lililofungwa na Shomari Kapombe dakika ya 68 kwa penalti, ugenini Aprili 24, 2022, Simba ikafungwa 1-0, ikafanya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1. Simba ilipoteza kwa mikwaju 4-3, huku wachezaji wake wawili, Jonas Mkude na Henock Inonga Baka wakikosa penalti. Pia ilishuhudiwa mshambuliaji wa Simba, Cris Mugalu akionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 58.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *