
“Kuongezeka kwa kasi kwa ghasia” nchini Sudan Kusini kumesababisha vifo vya watu 180 na wengine 125,000 kuhama makazi yao tangu mwezi Machi, inaonya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA).
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Nchi hii changa zaidi duniani, yenye utajiri wa mafuta lakini hata hivyo maskini, inatikiswa na ghasia katika maeneo kadhaa, hasa kaskazini mashariki. Pia kuna watu 250 waliojeruhiwa.shirika hilo limesema katika taarifa.
Hivi karbuni Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Pembe ya Afrika, IGAD, ilisema Sudani Kusini iko ‘katika ukingo wa vita’.
Mvutano wa hivi majuzi nchini Sudani Kusini unaisukuma nchi hiyo maskini na isiyo na utulivu “karibu zaidi na ukingo wa vita,” Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Pembe ya Afrika, IGAD imeonya siku ya Jumatano.
Mapigano mapya kaskazini mashariki yanatishia amani nchini Sudani Kusini, ilisema IGAD.
Mnamo Machi 4, “takriban wapiganaji 6,000 kutoka White Army,” kundi lenye silaha linalojumuisha vijana kutoka kabila la Nuer la Makamu wa Rais Riek Machar, lilichukua udhibiti wa kambi ya jeshi la Sudani Kusini, inabainisha IGAD, kundi linalojumuisha Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Uganda, Somalia, Sudani na Sudani Kusini. Wakati Rais Kiir alisema wiki iliyopita kwamba nchi yake haitakumbwa tena na machafuko, IGAD inabaini kwamba “msururu wa matukio na ghasia za mzunguko zinaweka shinikizo kubwa kwa makubaliano ya mwaka wa 2018 na kusukuma Sudani Kusini karibu zaidi na ukingo wa vita.”
Tangu kupata uhuru wake kutoka kwa Sudani mwaka 2011, nchi hiyo imekumbwa na ghasia ambazo zimeizuia kujikwamua kutoka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha umwagaji damu kati ya Rais Salva Kiir na Makamu wa Rais Riek Machar. Mzozo huu ulisababisha vifo vya karibu watu 400,000 na watu milioni nne kukimbia makazi kati ya mwaka 2013 na mwaka 2018, wakati mkataba wa amani ulipotiwa saini.