Mama Ali aeleza chanzo cha jina ‘Alikiba’

Dar es Salaam. Tombwe Njere ambaye ni mama mzazi wa mkali wa Bongo Fleva, Alikiba, ameeleza  historia ya jina la nyota huyo. Huku akiweka wazi kuwa jina “Kiba” halikutokea kwa bahati mbaya bali alipewa tangu akiwa tumboni.

“Kwanza jina lenyewe la Kiba lilitolewa na jirani yangu, nilikuwa na kitumbo changu mwenyewe cha Kiba. Jirani yangu anaitwa Mohamed Mawamba alikuwa ni rafiki sana wa mume wangu alikuwa ni kijana mdogo lakini alikuwa akifundishwa kazi na mume wangu.

“Sasa akawa ananifanyia utani mama kibanio mama kibanio, na hilo kibanio lilitokana na meli ilikuja hapo bandarini iliandikwa kibanio. Sasa yeye akawa ananitania mama kibanio. Basi hivyo hivyo siku nimejifungua Ally jina likaamia kwa mtoto akawa anaitwa kibanio na Ali mwenyewe kwenye swaga zake akakata ile kibanio ikabakia Kiba,”amesema mama Kiba

Aidha mbali na hilo ameeleza kuhusiana na nyota huyo kuonesha kitu cha tofauti siku saba baada ya kuzaliwa kwake.

“Alikuwa ndio kwanza ana siku saba, baba yake alimletea tenga. Basi siku hiyo baba yake akamuweka kwenye kile kitenga akawa amelala. Lakini baba yake alikuwa anapenda sana taarabu za Juma Balo alivyoplay tu ile taarabu mtoto akaanza kucheza.

“Sijakariri ule mwimbo ambao alimuwekea lakini ulikuwa wa Juma Balo. Basi mtoto akawa anatingisha kichwa watu tukajazana kushangaa mtoto anacheza, kwa hiyo mtu na chake alipewa tokea akiwa mdogo,”ameongezea mama Kiba

Ikumbukwe Alikiba akiwa na miaka zaidi ya 20 katika muziki, ameshinda tuzo za kimataifa ikiwemo All Africa Music Awards (AFRIMA) 2017 kama Wimbo Bora wa Kushirikiana Afrika (Aje) ft. M.I (Mr. Incredible) na MTV EMAs 2016 kama Msanii Bora Afrika.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *