Umri huu hatari kupata ugonjwa wa presha

Presha ni maradhi yanayotokana na kuongezeka kwa msukumo wa damu katika mishipa hali inayosababisha kazi ya moyo ya kusambaza damu iwe ngumu kuliko kawaida.

Maradhi hayo kwa kawaida hupimwa ujazo wa 120/80 cha makyuri, ambapo ili mgonjwa aonekane kwamba ana shinikizo la juu la damu, huanzia kipimo cha 140/90mm/hg.

Wataalamu wa afya wanatueleza kuwa uwezekano wa kupata maradhi ya hayo unaongezeka kadiri ya umri wa mtu unavyoongezeka. Wenye umri wa miaka 40 au zaidi wanakabiliwa na hatari kubwa ya kupata maradhi hayo.

Mwingiliano wa kifamilia, mazingira, mtindo wa maisha na aina za vyakula vinaweza kuwa sababu ya kupata maradhi ya presha.

Baadhi ya maradhi kama kisukari au kuzaliwa na uzito mdogo pia inaweza kuwa sababu za kupata maradhi haya ambayo takwimu zinaonyesha hadi Agosti 2024 yalikuwa yakiongoza kwa asilimia 34.

Pia takwimu za Serikali zinaonyesha wagonjwa wanaohudhuria vituo vya afya wameongezeka kutoka  1,112,704 mwaka 2019 hadi 1,482,911 mwaka 2023.

Makundi ya presha

Kundi la kwanza hujulikana Kiingereza ‘Primary’. Taarifa za kitafiti zinaonesha kuwa asilimia 90 hadi 95 ya wagonjwa wa presha wanasumbuliwa na aina

hii ya presha. Hata hivyo sababu zake hazijulikani.

Aina ya pili hujulikana kama ‘Secondary’. Wagonjwa

wanaosumbuliwa na presha hii ni kati ya asilimia tano  hadi 10. Mara nyingi presha hii husababishwa na maradhi ya figo, “adrenals” na mishipa ya damu.

Watu wenye umri wa miaka 18 au zaidi hutambulika kuwa wana presha iwapo kipimo cha presha ya juu kitazidi 139mmHg na kipimo cha chini kitazidi 89 mmHg.

Dalili na ishara za presha

Maradhi ya shinikizo la damu kwa kawaida huwa hayana dalili za wazi na za dhahiri katika hatua ya awali. Kufanya vipimo ndiko kutakakokufanya ujibaini kuwa una tatizo la ugonjwa huo.

Mara nyingi watu wanaosumbuliwa na presha huhisi dalili, zikiwamo kuumwa na kichwa hasa sehemu ya

nyuma, kizunguzungu, kukosa pumzi au kushindwa kupumua vizuri.

Dalili nyingine ni pamoja na nuru ya macho kupungua, kutoona vizuri, kuvimba miguu, wakati mwingine mgonjwa anaweza kuwa na dalili mbaya zaidi kama, kupooza, kupata mshtuko wa moyo, figo kushindwa kufanya kazi na nyinginezo.

Athari za presha

Maradhi ya presha yanasababisha athari mbalimbali ikiwemo kupata kiharusi, maradhi ya moyo, matatizo ya figo na upofu.

Aidha presha ni miongoni mwa maradhi yanayoweza kusababisha kifo ghafla hasa kwa watu ambao hawana utamaduni wa kuchunguza afya zao mara kwa mara.

Shinikizo la damu lina vipimo viwili; kipimo cha juu na kipimo cha chini vinavyotokana na mapigo ya moyo. Katika hali ya kawaida kipimo cha juu kinatakiwa kiwe baina ya 89 – 139 mmHg, na kipimo cha chini ni baina ya 60 – 90 mmHg.

Mtu ambae vipimo vitaonesha kuwa presha yake ni 140/90 mmHg au zaidi, presha yake itakuwa imepanda, na iwapo itakuwa 90/60 au chini ya hapo, presha yake itakuwa imeshuka.

Upimaji presha

Kwa kawaida presha hupimwa kwa mashine maalum inayofungwa kwenye mkono. Mgonjwa anatakiwa awe amepumzika angalau kwa muda wa dakika 10 asiwe amefanya mazoezi mazito, amevuta sigara au kunywa

kahawa angalau kwa muda wa saa moja kabla ya kupimwa

Pamoja na kuwa presha inayozidi 140/90 huhesabiwa kuwa kubwa, haina maana kuwa wagonjwa wote wenye presha kwa kiwango hicho watahitaji kutumia dawa.

Wagonjwa wengine hupoa kwa kufanya mazoezi, kuweka miko kama kutotumia chumvi kwenye chakula na kwa maelezo mengine watakayopewa na daktari.

Chukua tahadhari hizi

Maradhi ya presha mara nyingi zaidi huwapata watu wenye umri wa miaka 40 na kuendelea. Inasisitizwa kwa mtu yeyote aliyefikia umri huu kupima presha mara kwa mara, kupunguza matumizi ya chumvi katika chakula na kupunguza nyama zote nyekundu kama nyama ya ng’ombe, mbuzi

Pia kufanya mazoezi angalau dakika 30 kwa siku, kupunguza unene. Ikumbukwe kuwa unene wa kitambi

una uhusiano mkubwa na presha.

Cha kufanya ukigundulika una presha

Baada ya kugundulika kuwa na presha, tumia dawa za presha kama ulivyoelekezwa na daktari (usiziache

unaposikia nafuu) Usiache kuhudhuria kliniki ya presha mara kwa mara kama ipasavyo na acha matumizi ya chumvi na mafuta.

Acha utumiaji wa sigara na pombe, hakikisha unafanya vipimo vya macho na figo, fanya mazoezi angalau kwa muda wa nusu saa kila siku. Hata hivyo, ili mazoezi yawe na faida kimwili, lazima yafanywe wakati uleule kila siku.

Unapoiona presha yako imeshuka na kurudi presha ya kawaida baada ya kuanza kutumia dawa, utatakiwa kutoacha dawa, kwani presha yako itakuwa imekuwa ya kawaida kutokana na dawa.

Utakapoacha dawa, presha inaweza kupanda sana na kusababisha kupooza au kupata matatizo ya moyo, figo na macho.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dk Peter Kisenge aliwahi kulieleza Mwananchi kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaogua presha.

 “Tunapoenda kwenye jamii tunaona takwimu kama hizo, kwa JKCI hapa asilimia 30 ya wagonjwa tunaowaona wana shinikizo la juu la damu na kwenye kambi tukiwafuata mitaani tunawapata asilimia 26,” anasema.

Dk Kisenge ambaye pia ni bingwa wa magonjwa ya moyo anashauri jamii kubadili mtindo wa maisha, akisema asilimia kubwa ya watu hawafanyi mazoezi huku wakiwa na ulaji mbaya, unywaji pombe uliokithiri, uvutaji sigara uliokithiri na kuwa na unene kupita kiasi vitu vinavyochangia tatizo hilo.

Makala haya yaliyoboreshwa ni kwa hisani ya Jarida la Afya la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, toleo No 5.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *