Mtwara. Ikiwa imesalia miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwaka 2025, Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kujipanga kuhakikisha kinadumisha himaya yake katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kuzuia majimbo na kata zake kuangukia mikononi mwa upinzani.
Mikoa ya Lindi na Mtwara imekuwa sehemu muhimu ya CCM kwa muda mrefu, na chama hicho kimeendelea kuhakikisha kinadumisha uungwaji mkono wake huku ikichukua hatua kadhaa za kisiasa na maendeleo.
Hata hivyo, licha ya Mkoa wa Lindi kuwa na majimbo ya uchaguzi ambayo yako chini ya CCM kwa sasa, historia inaonyesha kuwa upinzani umefanikiwa kutikisa ushawishi wa chama hicho katika baadhi ya maeneo, hasa kutokana na changamoto zinazozikumba jamii na wananchi.
Katika uchaguzi wa miaka ya nyuma, CCM ilijikuta ikichuana kwa karibu na Chama cha Wananchi (CUF) na baadaye ACT Wazalendo, katika baadhi ya maeneo ya mikoa hiyo miwili.
Hata hivyo, ndoto ya CCM kuendeleza ushindi wa kishindo inakumbwa na changamoto sugu ambazo zimekosa ufumbuzi kwa muda mrefu, hali inayowafanya wananchi na viongozi wa chama hicho kupaza sauti, hasa katika mkoa wa Lindi.

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, mkoani Mtwara, leo Aprili 15, 2025 katika mwendelezo wa ziara yake mkoani humo.
Changamoto hizi ni pamoja na ucheleweshwaji wa fidia kwa wananchi waliopisha upanuzi wa viwanja vya ndege, miundombinu mibovu ya barabara, tishio la tembo wanaosababisha vifo vya watu na hasara kwa wakulima, pamoja na madai ya usaliti unaofanywa na baadhi ya wanachama wa CCM.
Katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025, Katibu wa Halmashauri Kuu (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, amekutana na malalamiko kutoka kwa wananchi, wabunge na viongozi wa chama katika mikoa hiyo miwili.
Wananchi walia na fidia
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilwa, Said Timami, amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa CCM, bado kuna masuala yanayotia doa katika utendaji wa Serikali na chama.
“Hapa Kilwa, kazi nzuri imefanyika, tunashukuru sana. Bandari inajengwa, huduma za maji, afya na umeme zipo. Lakini kuna changamoto ya fidia kwa wananchi 446 waliopisha upanuzi wa mradi wa uwanja wa ndege tangu mwaka 2013 ambao hadi sasa hawajalipwa. Hili ni doa kwetu kama chama,” amesema Timami.
Ameongeza kuwa barabara ya Rufiji hadi Kilwa yenye urefu wa kilomita 30 bado ni kero kubwa kwa wananchi, na kwamba kutatua changamoto hizo kutazima kabisa uwezekano wa upinzani kurejea katika eneo hili.
Mbunge wa Kilwa Kusini, Ally Kasinge, ameiunga mkono hoja hizo akieleza kuwa kucheleweshwa kwa malipo ya fidia na changamoto za barabara vimekuwa kero kubwa kwa wananchi wa jimbo lake.
“Tangu mwaka 2013, wananchi walizuiwa kufanya shughuli zozote za maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba, baada ya Serikali kufanya tathmini na kuahidi kuwalipa wananchi Sh6 bilioni. Hadi sasa hawajalipwa,” amesema Kasinge.
Hali hiyo imekuwa ni chanzo cha maumivu kwa wananchi, ambapo wanadai kuwa kucheleweshewa malipo hayo kumekuwa kikwazo cha maendeleo kwao, kwani wameshindwa kujenga nyumba mpya wala kuendeleza mashamba yao tangu walipohamishwa kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege.
Makalla, akijibu hoja hiyo kwa vitendo, alimpigia simu Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba mbele ya wananchi, ambapo waziri huyo alithibitisha kuwa fedha hizo zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 na malipo yatafanyika kabla ya Juni 30, 2025.
“Nitahakikisha wananchi hawa wanapata haki yao. Nitawasiliana na wenzangu wizarani ili walipwe ndani ya mwaka huu wa bajeti,” amesema Dk Mwigulu.
Changamoto hiyo ya fidia haipo Kilwa pekee, kwani hata wilayani Nachingwea wananchi waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege, nao wamekuwa wakilalamika kwa zaidi ya miaka mitano sasa. Makalla aliahidi kuwa changamoto zote hizo zitafanyiwa kazi haraka.
Tishio la tembo Liwale
Katika wilaya za Liwale na Nachingwea, wananchi wamelalamikia kero ya tembo ambao wamesababisha vifo na uharibifu wa mazao. Wamesema hali hii inatia hofu kwa wakulima na wananchi, na inachangia kukwamisha juhudi za maendeleo katika maeneo hayo.

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, mkoani Mtwara, leo Aprili 15, 2025 katika mwendelezo wa ziara yake mkoani humo.
Mbunge wa Liwale, Zubeiry Kuchauka, amesema: “Tangu Machi 23, 2025, watu wanne wamepoteza maisha kutokana na mashambulizi ya tembo. Hili ni jambo kubwa. Si rahisi tembo kutoka Morogoro hadi Liwale bila Tanapa (Shirika la Hifadhi za Taifa) na Tawa (Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania) kuona.”
Amesema tembo hao wamekuwa wakivamia maeneo ya makazi na mashamba ya wakulima, na mashambulizi yao yamekuwa yakisababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mazao ya chakula na biashara. Hii ni changamoto kwa wananchi wa Liwale na Nachingwea na inahitaji utatuzi wa haraka.
Makalla amemhakikishia mbunge huyo na wananchi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana, atatembelea wilaya hizo ili kujionea hali halisi na kushughulikia tatizo hilo.
“Nalijua tatizo la tembo maana nilikuwa Mbunge wa Mvomero na Mkuu wa Mkoa wa Katavi. Waziri amekubali kuja kuangalia maeneo yaliyoathirika,” amesema Makalla.
Miundombinu na nishati
Akijibu kero ya barabara inayounganisha Nangurukuru na Liwale, Makalla amesema tayari amezungumza na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ambaye ameahidi kuwa barabara ya Nangurukuru hadi Liwale itajumuishwa kwenye bajeti ijayo na kujengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hiyo ni kiunganishi muhimu cha kusafirisha mazao, hasa korosho.
Katika sekta ya nishati, Makalla amesema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amethibitisha kuwa makandarasi wamelipwa ili kukamilisha mradi wa kuifikisha gridi ya Taifa wilayani Liwale.
“Tutahakikisha suala hili linaingizwa rasmi kwenye Ilani ya CCM ili liweze kufanyiwa kazi kwa haraka,” ameongeza.
Usaliti ndani ya chama
Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga alisema kuna watu ndani ya chama hicho ambao wamekuwa wakitoa siri kwa wapinzani wao hususan Chadema ana kwamba wanapaswa kushughulikiwa haraka.
“Ukweli lazima usemwe, kuna wahuni hapa Mtwara ambao wanaenda kuwatia sumu wananchi na hawa wahuni wako ndani ya CCM, hili halikubaliki.
Mkakati uchaguzi mkuu 2025
Akizungumzia uchaguzi wa baadaye mwaka huu, Makalla amesema CCM imejipanga vizuri na itawasilisha wagombea wanaokubalika na ilani bora zaidi. Amesema CCM itatilia mkazo ujenzi wa uchumi imara na kuboresha huduma muhimu kwa wananchi.
Ameongeza kuwa CCM itatumia kampeni za kistaarabu kwa misingi ya dhana ya 4R za Rais Samia: Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Uvumilivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding (Ujenzi wa Taifa). “Hatutajibu matusi bali kwa kazi na hoja,” amesema.
Kuhusu changamoto ya mawasiliano kati ya mikoa ya kusini na Dar es Salaam, Makalla amesema Serikali inatambua tatizo hilo na Rais Samia amemuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufika maeneo husika kutafuta suluhisho.
Mkazi wa Mpilipili mkoani Lindi, Mzee Said Kalembo, amesema kazi kubwa imefanyika lakini kuna changamoto chache ambazo inatakiwa zifanyiwe kazi ikiwamo kusaidia uboreshaji wa barabara katika maeneo korofi, na kudhibiti tembo ambao wamekuwa changamoto kwa wananchi.
“Ikiwa changamoto hizi zitapatiwa ufumbuzi kabla ya uchaguzi, huenda CCM ikaendelea kufanya vizuri katika mkoa huu wa Lindi,” amesema Kalembo.
Upande wake, Mwajuma Ramadhani, mkazi wa Kilwa Masoko amesema wanasubiri kwa shauku kubwa kuona wakilipwa fidia yao ambayo yameisubiri kwa muda mrefu.
“Kwa kweli baba yangu hiki nilichokisikia hapa sasa nina amani kwani tumemsikia waziri mwenyewe akitoa fedha, hivyo tuna imani na chama chetu kuwa kitaendelea kufanya mambo mazuri,” amesema Mwajuma.