
Dodoma. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ameionya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutowalazimisha wakulima kutumia mashine za kutoa risiti za kielektroniki (EFDs), akibainisha kuwa hakuna sheria iliyopitishwa na Bunge inayowataka kufanya hivyo.
Bashe ameyasema hayo leo Aprili 15, 2025 wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2025/26.
Mjadala huo ulianza Aprili 9, 2025 baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi, kuomba kuidhinishiwa na Bunge Sh782.08 bilioni kwa mwaka 2025/26.
Akichangia mjadala huo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kuna kilio kikubwa kutoka kwa wakulima nchini kuhusu sharti la kutakiwa kuwa na mashine za EFDs, akisisitiza kuwa wakulima hawalazimiki kumiliki mashine hizo kwa ajili ya kutoa risiti za kielektroniki.
Amesema siyo shughuli ya wakulima wala vyama vya ushirika iliyopitishwa na Bunge na kushirikiana na wizara hiyo katika kurasimisha sekta ya kilimo.
“Kurasimisha wafanyabiashara wawe na mashine, waingie katika orodha ya walipa kodi…Niwaombe TRA wawaache wakulima wafanye kazi ya uzalishaji,”amesema.
Amesema Bunge halikupitisha wakulima wawe na mashine za EFDs na wala siyo maelekezo ya ilani ya uchaguzi wala chama kilicho madarakani.