NCC yatoa njia mbadala kutatua migogoro bila kuishtaki mahakamani

Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) limesema kuwa migogoro ya kibiashara, madai ya kimkataba na mingine inayojitokeza katika sekta mbalimbali nchini, ikiwemo ya ujenzi, inaweza kutatuliwa bila wahusika kupelekana mahakamani.

Hali hiyo, kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya usuluhishi na utatuzi wa migogoro wanaotoa mafunzo kuhusu eneo hilo chini ya uratibu wa NCC.

Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni, wakati mafunzo hayo, Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu, Dk Fauz Twaib, ambaye ni miongoni mwa wanaofundisha njia hizo, amesema, “kinachotakiwa ni wasuluhishi kuzingatia maadili, sheria na taratibu za usuluhishi.”

Amesema kuwa kuna zaidi ya njia nne za kusuluhisha migogoro, mbali na kushtakiana mahakamani, ambazo zinafundishwa na kuwawezesha waliopata mafunzo hayo kuamua kwa weledi ipi inafaa kulingana na mazingira na hali halisi ya mgogoro husika.

Kwa mujibu wa Dk Twaib, kwa kutumia njia hizo mbadala, hakuna upande unaojeruhiwa kwa sababu pande zote zinahusika katika hatua zote muhimu za usuluhishi, ikiwemo kuchagua nani ahusike kuwasuluhisha.

“Ikiwa hakuna mazingira yoyote ya tamaa inayoweza kusababisha upendeleo, mfano rushwa au chochote kile kitakachofanya usuluhishi uegemee upande mmoja, mlolongo wa kisuluhishi hautokei, hivyo kuokoa muda na gharama,” amesema.

Washiriki wa mafunzo hayo wakifanya mtihani wa kuandika, lengo likiwa ni kupima uelewa wao kuhusu maarifa waliyoyapata kwenye mafunzo hayo.

Mhandisi wa kujitegemea, Julius Mamiro anayefundisha mbinu hizo, hususan majadiliano ya kisuluhishi ya madai ya kimkataba ya ujenzi, amesema kuwa maadili mazuri yanafanikisha usuluhishi.

Amesema kuwa jambo kubwa wanalolisisitiza ni kuwa wataalamu wa masuala yote yanayoweza kuhusika kwenye migogoro, iwe ya sekta ya ujenzi au ya kibiashara nje ya sekta ya ujenzi, au ya kimkataba kwenye sekta yoyote, wawe na elimu ya namna ya kuitatua migogoro yao bila kupelekana mahakamani, kisha watekeleze mbinu walizofundishwa kwa kuzingatia maadili.

Kwa maelezo yake, kujua kusuluhisha au kutatua mgogoro halafu ukauharibu utatuzi kwa kutoruhusu haki au kwa kupendelea, hata kama umefunzwa vipi,  unabaki kuwa kikwazo cha usuluhishi.

“NCC inatekeleza jukumu la kuhakikisha elimu hiyo inawafikia watu wengi, kwa faida ya wanaoipata, wateja wao, familia zao na taifa kwa ujumla,” amesema.

Amesema kuwa kutokana na umuhimu huo, anawashauri Watanzania kuchangamkia mafunzo hayo pindi wanapopata fursa hiyo nyakati zote yanapotangazwa.

Katika mafunzo hayo yaliyotolewa kwa siku tatu, washiriki walifanya mazoezi ya usuluhishi kwa vitendo na kisha kutahiniwa kwa mtihani wa kuandika, lengo likiwa ni kupima uelewa wao kuhusu maarifa waliyoyapata kwenye mafunzo hayo.

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anayehusika na sehemu ya mikataba, majadiliano na utawala, Mkadiriaji Majenzi Elias Kisamo, pamoja na kufundisha, alijibu maswali tata yaliyoulizwa na washiriki wa mafunzo hayo, hivyo kuongeza uelewa wao juu ya walichojifunza.

 “Ukitaka usuluhishi uende sawa, epuka njia za mkato. Hakuna shortcuts, iwe katika majadiliano au kwenye utatuzi mwingine – epuka shortcuts,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *