FARDC yawaua wapiganaji kumi wa kundi la waasi wa CRP/Zaire Ituri

Jeshi la DRC, FARDC Jumatatu ya tarehe 14 ya wiki hii limethibitisha kuwaua wapiganaji 10 kutoka kundi la wapiganaji wenye silaha la CRP/Zaire linaloshirikiana na waasi wa M23 na ambalo linaoongozwa na Thomas Lubanga.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Taarifa ya FARDC inasema mauaji ya waasi hao yalifanyika wakati wa makabiliano kwenye eneo la Joo, kando kando ya Ziwa Albert katika Wilaya ya Djugu jimboni Ituri.

Kulingana na Luteni Jules Ngongo, msemaji wa jeshi katika jimbo la Ituri, mapigano yalizuka baada ya waasi hao kutekeleza shambulio katika ngome ya wanajeshi wa FARDC kitengo cha 332 cha maofisa wa majini.

Baada ya kuuawa kwa waasi hao na jeshi la kawaida, maofisa wa FARDC pia wamethibitisha kuchukuliwa kwa silaha zao.

Jeshi la DRC aidha limewahakikishia wakazi kwamba hali imerejea tulivu kando kando ya Ziwa Albert na kwamba shughuli za kawaida zinaendelea.

Waasi kutoka kundi la CRP/Zaire wamekuwa wakituhumiwa kwa kutekeleza mashambulio dhidi ya ngome za wanajeshi wa kawaida kwa majuma kadhaa.

Luteni Ngongo amewataka raia kushirikiana na jeshi la serikali FARDC ilikusaidia katika urejeshaji wa usalama kwenye eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *