Hizi hapa mbinu za kukabiliana na homa ya mtihani

Baadhi ya wanafunzi wamekuwa  wakifanya vibaya mitihani yao ya kishule au ya kitaifa kwa sababu tu ya hofu ya mtihani.

Hofu ya mtihani ni wasiwasi anaoupata mwanafunzi wakati wa maandalizi ya mitihani yake au anapokuwa ndani ya chumba cha mtihani.

Mwanafunzi huyu anawaza juu ya mitihani yake, je atafaulu au  la au kama mitihani itakuwa migumu au itakuja katika maeneo aliyoyasomea.

Hofu ya mtihani imegawanyika katika makundi  manne; kimwili (mwili kutokwa na jasho),kiakili (kufikiri kuwa hawezi),kihisia (kama vile kuwa na hasira) na kitabia (kula sana au kukosa hamu ya chakula).

 Chanzo kikubwa cha homa ya mtihani ni maandalizi duni.Mwanafunzi asiyejiandaa vyema,yuko kwenye hatari kubwa ya kupata homa hii.

Zifuatazo ni dalili zinazoonesha kuwa mwanafunzi amepata homa ya mtihani; kuwa na hali ya kutojiamini  hasa wakati wa mitihani, kuwa na wasiwasi kila mara kama atafaulu ama atafeli na kuwa na hasira za mara kwa mara kwa wenzake na wote wanaomzunguka wakati wa maandalizi ya mitihani au wakati wa ufanyaji mitihani.

Nyingine ni kujiona kama hawezi kufaulu na kwamba kufaulu ni kwa ajili ya wanafunzi fulani tu, mwili kutetemeka  anapokuwa ndani ya chumba cha mtihani au kutokwa na jasho karibia kila sehemu ya mwili wake na hasa kwenye viganja vya mikono.

Kujisikia haja kubwa au ndogo na kila akienda chooni hapati haja yoyote,kusikia kuzunguzungu mara kwa mara au kichwa kuuma anapokuwa ndani ya chumba cha mtihani, kula sana au kula kidogo wiki ya mtihani au wiki ya maandalizi ya mtihani na kulala kidogo au kutopata usingizi tofauti na hali yake ya mwanzo.

Mbinu kukabiliana na homa hii

Ikiwa dalili hizi zimejitokeza ndani ya chumba cha mtihani au wiki ya maandalizi ya mitihani, usihamanike.Fanya haya.

Mosi, jiandae vyema kwa kuhakikisha umesoma vyema masomo yote kwa uzani sawa.

Pili, usipende kuongea na wanafunzi ambao unahisi hawajajiandaa vyema,watakuwa ni chanzo kizuri cha kukusababishia hofu.

Tatu, epuka kufanya vitu ambavyo ulikuwa huna utamaduni wa kuvifanya hapo nyuma,kama vile kuoga asubuhi kama ilikuwa siyo kawaida yako usifanye hivyo kwani mwili utaingia katika mabadiliko mengine na hivyo kukusababishia hofu siku ya mtihani.

Nne, nenda msalani kabla ya kuingia kwenye chumba cha mtihani. Choo cha asubuhi kinasaidia kuondoa hofu.

Tano, unapoingia ndani ya chumba cha mtihani, jambo la kwanza anza kwa kuomba dua kwa Mola wako kwa mujibu wa imani yako.

Sita, soma maswali  mara tatu kwa uchache,mtihani huwa umefungwa kwenye maelekezo,ukishindwa kufuata maelekezo ndiyo mwanzo wa kufanya vibaya katika mitihani yako.

Saba, anza na maswali unayoyaweza kwanza,kisha fanye usiyoyaweza mwisho.

Nane, hakikisha unatumia muda wako vizuri. Ni vizuri mwanafunzi kuwa na saa ndani ya chumba cha mtihani ili kujua muda.

  Tisa, hakikisha umeandika taarifa zako muhimu kama vile namba ya mtihani kwenye kila ukarasa wa kujibia.

Fanya haya baada ya mtihani

Unapomaliza mtihani wako,hakikisha haujadiliani na mtu yeyote kuhusu mtihani uliopita,kwani anaweza kukwambia swali fulani umekosa kumbe umelipata na hivyo ukakosa amani na kushindwa kujiandaa vyema kwa mitihani ijayo kwa kufikiria mtihani uliopita.

Jiandae vyema kwa ajili ya mitihani ijayo pasi na kufikiria mitihani iliyopita, kwani mawazo hayo yanaweza kukuathiri usifanye vyema kwenye mitihani iliyobaki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *