
WATETEZI wa Kombe la Shirikisho (FA), Yanga jioni ya leo wanashuka uwanjani kuikaribisha Stand United katika mchezo wa robo fainali ya michuano hiyo, huku Chama la Wana likipiga hesabu ya kuwa klabu ya kwanza ya Ligi ya Championship kutinga nusu fainali baada ya nyingine kutolewa.
Mchezo huo wa hatua ya robo fainali utapigwa kwenye Uwanja wa KMC ambapo timu hizo tatu zitakutana zikitoka kushinda mechi tatu za hatua zilizofuata kila moja ikiing’oa timu nyingine.
Yanga inaonyesha bado inalitaka taji hilo inalolishikilia kwa msimu wa tatu mfululizo sasa baada ya msimu huu kuzitoa Copco katika hatua ya 64 Bora, kisha kuing’oa Coastal Union hatua ya 32 Bora na katika 16 Bora iliitambia Songea United.
Katika mechi hizo Yanga imefunga jumla ya mabao 11, ikiruhusu mabao mawili tu na leo inaenda kukutana na Stand ambao haikufika hapo kwa kubahatisha, kwani ilianza hatua ya 64 Bora kwa kuing’oa Don Bosco kwa mabao 2-0 kisha 32 Bora ikaitupa nje Fountain Gate kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1. Hatua ya 16 iliitupa nje Giraffe Academy kwa mabao 3-1 na sasa inavaana na Yanga ikikumbushia vita yao wakati ikicheza Ligi Kuu.
Taarifa nzuri kwa Stand ni kwamba itaikabili Yanga bila ya viungo wawili wa kikosi cha kwanza Khalid Aucho na Pacome Zouzoua ambao ni majeruhi, lakini bado wasibweteke kwa vile bado wenyeji wana kikosi cha wakali wengi.
Stand inatakiwa kuwa makini na safu ya ushambuliaji ya Yanga inayongozwa na kinara wao wa ufungaji Prince Dube aliyefunga mabao 12, Clement Mzize mwenye mabao 11.
Kocha wa Yanga Hamdi Miloud akizungumzia mchezo huo, alisema hautakuwa rahisi lakini kikosi chake kipo tayari kwa mechi dhidi ya Stand Utd na kwamba hawataki kufanya makosa ya kuidharau timu yoyote.
“Tunahitaji kutetea ubingwa wetu, tunakwenda kukutana na timu ambayo nayo imekuwa na matokeo mazuri, tunahitaji kushinda vizuri na kufuzu, ukiwa kwenye njia ya kupigania malengo yako hutakiwi kumdharau mpinzani yeyote, tunawaheshimu wapinzani wetu,” alisema Miloud.
Mara ya mwisho Yanga kukutana na Stand United ilikuwa mwaka 2018 Machi 12, ikishinda nyumbani kwa mabao 3-1, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Stand hadi kufika robo imefunga jumla ya mabao sita na kuruhusu mawili inatambia wachezaji wanaoibeba katika Ligi ya Championship akiwamo Khalid Jafari anayeweza kufunga kwa mashuti ya mbali na Msenda Senga na Omary Ramadhan ambao wamekuwa na uchu wa kucheka na nyavu.
Kocha wa timu hiyo, Masoud Juma alisema: “Tunakwenda kukutana na timu ngumu na bora ya Yanga, kwanza lazima tuwaheshimu kutokana na ubora wa kikosi chao, tutashambulia kwa hesabu na kujilinda.”