Usafiri wa waya mbioni nchini

Dar es Salaam. Katika jitihada za kuendana na ukuaji wa teknolojia na uboreshaji wa miundombinu Tanzania iko mbioni kuanzisha mifumo ya usafiri wa nyaya (Cable Transport), katika maeneo ya vivutio vya utalii pamoja na maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu.

Akizungumza na waandishi wa habari na wahariri jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra), Habibu Suluo, amethibitisha kuwa mfumo wa udhibiti kwa ajili ya usafiri wa nyaya  umefikia hatua za mwisho, ambapo rasimu ya kanuni tayari iko chini ya mapitio ya Serikali, huku mabadiliko ya taasisi yakiendelea kufanyika ili kuendana na  aina hiyo mpya ya usafiri.

“Hili si suala la utalii tu. Usafiri wa nyaya pia utategemea upangaji wa miji, kanuni za mazingira kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), na mwongozo kutoka mamlaka nyingine husika. Tumetoa kipaumbele kwa mikoa minane kwa sababu ya fursa zake za utalii, lakini hiyo haimaanishi kuwa mikoa mingine haitastahili,” amesisitiza Suluo.

Mikoa iliyotajwa awali ni pamoja na Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, na Mbeya.

Mpango huo wa usafiri wa nyaya ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (2021/2022 hadi 2025/2026) unaolenga kuboresha miundombinu ya utalii kwa kiwango cha kisasa.

Kwa mujibu wa Suluo, Bodi ya Latra iliamua kuwa katika hatua za maandalizi, usafiri wa nyaya usimamiwe chini ya mfumo wa udhibiti wa reli kutokana na ugumu wa kiufundi unaohusiana na miradi hiyo.

“Hii ndiyo sababu wahandisi wetu walitumwa nje ya nchi  katika mataifa kama Korea Kusini, Malaysia na Afrika Kusini kujifunza uzoefu bora wa kimataifa,” amesema Suluo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra), Habibu Suluo.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 17 cha Sheria ya Latra, bodi ina mamlaka ya kubuni muundo wa idara mbalimbali ndani ya mamlaka hiyo.

Suluo ameeleza kuwa, ingawa bodi iliyopita haikuanzisha kitengo maalumu kwa ajili ya usafiri wa nyaya, bodi ya sasa iliyo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imechukua hatua madhubuti kuanzisha mchakato huo.

“Katika hatua hii ya awali, kitengo hiki hakitahitaji idadi kubwa ya watumishi. Tunaweka mazingira wezeshi huku tukiruhusu sekta binafsi kuongoza katika uwekaji wa miundombinu. Kadri mahitaji yatakavyoongezeka, kitengo hiki kitapandishwa hadhi kuwa idara kamili,” ameongeza.

Amefafanua kuwa muundo wa awali wa taasisi umeshawasilishwa kwa Msajili wa Hazina na kupita kwenye ukaguzi wa taasisi mbalimbali, ikiwemo maoni kutoka Wizara ya Uchukuzi na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

“Tunasubiri kuitwa kwenye kikao cha Kamati ya Mashirika ya Umma (PIC) inayoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi. Baada ya hapo, pendekezo litapelekwa kwa Rais kwa ajili ya kuidhinishwa rasmi na kuanzishwa kwa kitengo hiki,” amesema.

Wakati huohuo, rasimu ya kanuni za usafiri wa nyaya iko katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na huenda ikachapishwa wakati wowote.

Mfumo huo wa usafiri, unaohusisha magari yasiyo na injini yanayosukumwa na nyaya za chuma, tayari umevutia wawekezaji wengi wa kimataifa.

“Hili ni sekta mpya kabisa hapa Tanzania. Ndiyo maana bodi yetu ilitushauri tumtafute mshauri wa kimataifa kupitia kanuni kabla ya utekelezaji kamili. Tunaendelea na mazungumzo na washirika wa maendeleo, wakiwemo Benki ya Dunia, ili kuharakisha mchakato huu,” amesema Suluo.

Mkurugenzi huyo wa Latra amethibitisha kuwa Algeria, China, Ufaransa na Misri ni miongoni mwa nchi zilizoonyesha nia ya kushirikiana katika miradi ya usafiri wa nyaya.

“Mtengenezaji mmoja wa magari ya nyaya kutoka Ufaransa pia ameonyesha utayari wa kushirikiana na mwekezaji yeyote anayelenga soko la Tanzania.”

Huku utalii ukiwa kichocheo kikuu cha usafiri huu katika mikoa kama Arusha na Kilimanjaro, Latra imesisitiza kuwa usakinishaji wa baadaye utategemea upangaji wa miji, uendelevu wa mazingira na makubaliano ya wadau.

 “Hata kama mikoa hii minane imepewa kipaumbele kwa sababu ya thamani ya kitalii, mikoa mingine pia ina fursa. Hatubagui kupeleka ubunifu huu sehemu yoyote nchini,” ameeleza Suluo.

Msisitizo wa Latra juu ya ujumuishi na uendelevu unaonyesha dhamira ya Serikali kuunda mustakabali ambapo teknolojia, usafiri na utalii vinaunganishwa kwa tija.

Mamlaka hiyo pia imewahakikishia wananchi kuwa maendeleo yoyote katika eneo hilo yatazingatia viwango vya kimataifa vya usalama na mazingira.

Suluo amesisitiza kuwa, pindi mfumo huo utakapokuwa kamili, unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika namna Watanzania wanavyosafiri hasa katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu na vituo vya utalii,  kwa kutoa mbadala wa usafiri wa barabara ulio rafiki kwa mazingira, wenye ufanisi, na unaovutia kwa mandhari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *