Baada ya mazungumzo ya timu za Simba na Yanga, serikali imesema kuwa imepanga kuzungumza na wadhamini wa Ligi Kuu kuhusu mchezo baina ya timu hizo ‘Kariakoo Derby’ na kuwataka Watanzania na mashabiki wa kuwa na subira wakati mazungumzo hayo yakiendelea.
Dabi ya Kariakoo ilipangwa kuchezwa Machi 8, 2025 lakini haikuchezwa baada ya kuahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na serikali ilianza mazungumzo na timu zote mbili kuhusu mustakabali wa mechi hiyo.
Akizungumza leo Jumatatu Aprili 14, 2025 kuhusu mafanikio ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita jijini Dodoma, Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema mazungumzo kuhusu dabi hiyo yamefikia hatua nzuri baada ya mazungumzo yaliyofanyika kwa klabu za Simba na Yanga.
Amesema kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) na lile la Afrika (CAF), serikali hairuhusiwi kuingilia masuala ya mpira ila kinachoendelea ni kuzikutanisha timu hizo ili waweze kujua muafaka kuhusu dabi hiyo ya Kariakoo.
“Ni kweli Machi 27 tulikutana na timu za Simba na Yanga na nina mpango sasa wa kukutana na wadhamini wa Kariakoo Derby, benki ya NBC lengo letu lilikuwa ni kuwakutanisha wao wakutane waongee. Masuala ya ligi yanasimamiwa na TFF na bodi ya ligi na Waziri hawezi kuyaingilia kwa kanuni za FIFA kama mnavyofahamu,” amesema Kabudi.
Amesema dabi ya Kariakoo imepata umaarufu wa Kimataifa na sasa ina wafuasi wengi kwa hiyo wizara ilichofanya ilikuwa ni kuwaleta pamoja ili waanze mchakato wa wao kufikia maridhiano na maelewano ambayo hatimaye yatafika mahali ambapo wale wenye dhamana ya kisheria na kikanuni kutoa tamko watatoa tamko.
Amesema kazi yake ni kuendelea kuwaweka pamoja ili wafike muafaka ambao utakapokamilika wakutangaza hatakuwa Wizara wala Waziri bali ni yule ambaye sheria imempa dhamana ya kusimamia mambo hayo
“Lakini mambo kama hayo yanapotokea hauwezi kukaa pembeni lengo lako ni kuwaleta, kaeni nini kimesibu, na katika taaluma ya kuwaleta watu ambao wana tofauti moja ya jambo kubwa ni kuwa na ‘embago’ (siri) na lengo lake siyo kuwanyima watu habari ila wakati wake haujafika ila baada ya hapo litafika,” amesema waziri huyo.
Amesema kwa wakati muafaka yote yanayoendelea wana uhakika wakati ukifika watasema na kuwaomba Watanzania wawe na subira kwa sababu hizi klabu zina wafuasi, wapenzi na mashabiki Rwanda Burundi, Kenya Uganda, Kongo, Zambia, Afrika Kusini kwa hiyo hiyo heshima hatuna budi kuienzi na kuitunza
“Na mimi naamini kabisa mwisho wa siku heshima hiyo itafanya tufikie mahali pazuri lakini tumefika wapi? Bado ni embago,” amesema Profesa Kabudi.

Matengenezo ya uwanja wa Benjamini Mkapa
Profesa Kabudi amesema uwanja wa Benjamin Mkapa umefanyiwa matengenezo makubwa kwa ajili ya mashindano ya CHAN na yale ya AFCON ambayo yanatarajiwa kufanyika uwanjani hapo.
Amesema baada ya mechi ya Kimataifa kati ya Simba na Al Masry serikali ilitangaza kuufunga uwanja huo kwa ajili kuukarabati kwa ajili ya michuano ya CHAN na AFCON.
Amesema uwanja huo kwa sasa umeshafanyiwa ukarabati mkubwa kwani ulikuwa haujawahi kufanyiwa ukarabati tangu ulipoanza kutumika ambapo mpaka sasa viti vipya 40,000 vimeshawekwa, bado viti 20,000, wameshafunga taa 360 uwanjani hapo, wameshafunga CCTV kamera na kukarabati vyoo vya uwanjani hapo.
“Kuna matengenezo makubwa yamefanyika kwani kabla ya mechi ya simba na Al MAsry mvua kubwa ilinyesha kwa muda wa saa mbili na baada ya nusu saa timu zikaingia uwanjani kwa hiyo tulilazimika kuufunga uwanja huo ili ufanyiwe ukarabati,” amesema Profesa Kabudi

Barua ya Pongezi kwa Rais wa Yanga
Kufuatia Rais wa Klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa Umoja wa Vilabu Afrika (ACA), Hersi Said kupata tuzo kutoka World Football Summit (WFS), ya kuthamini mchango wake wa kuunganisha vilabu vya soka Afrika, Waziri Profesa Kabudi amesema kuwa atamwandikia barua ya pongezi kwa kupata tuzo hiyo.