Zile 10 za Chikola zapata ugumu

NYOTA wa Tabora United, Offen Chikola amekiri ameanza kupata shaka ya kutimiza ndoto zake za kufunga mabao 10 msimu huu ili kuweka rekodi binafsi katika Ligi Kuu Bara iliyopo ukingoni.

Mshambuliaji huyo, alisema kwa sasa anakuna kichwa ili kuona anazitumia mechi nne zilizosalia za timu hiyo kufunga mabao matatu na kukamilisha hesabu ya mabao 10, kwani tayari anayamiliki saba kupitia mechi 26 zilizochezwa na timu hiyo inayoshika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi hiyo.

Katika mechi hizo nne ni timu moja tu alizoitungua kwenye duru la kwanza, kitu kinachompasua kichwa kujipanga ili kusahihisha makosa na kutimiza ndoto za kumaliza na idadi hiyo ya mabao anayoota.

Tabora imekabisha mechi dhidi ya Singida Black Stars, KMC, Azam na Coastal Union, huku ni KMC tu ndio iliyotunguliwa na Chikola katika ushindi wa mabao 2-0, huku bao jingine likifungwa na Yacouba Songne aliyetumika kwa dakika 45 za kutoka kutokana na kuumia na hadi sasa yupo nje ya uwanja.

Katika mechi dhidi ya Singida matokeo yalikuwa ni sare ya 2-2 mabao yakifungwa na Yacouba Songne na Heritier Makambo), walipoinyoa Azam kwa mabao 2-1, Tabora ilipata mabao yake kupitia kwa Makambo na jingine na kujifunga la kipa wa wageni, Mohamed Mustafa na ilipotoka sare ya 1-1 na Coastal kwa bao la Tabora likifungwa na Benele Sikhondze.

“Natambua ugumu uliopo kwa hizo mechi nne zilizobaki kufunga msimu, ili niweze kufanikisha ndoto ya kumaliza mabao si chini ya 10, ninachokifanya nazidisha mazoezi binafsi, nazingatia muda wa kupumzika na kula kwa wakati ili kuuweka mwili wangu fiti,” alisema Chikola aliyesajiliwa Tabora akitokea Geita Gold na kuongeza; “Natamani kutajwa katika orodha ya wachezaji ambao watamaliza  msimu wakiwa na mabao mengi, kama inavyokuwa kwa washambuliaji wengine bora katika Ligi Kuu.”

Chikola mwenye asisti mbili hadi sasa katika Ligi, alisisitiza endapo akitokea akapata  nafasi ya kutoa pasi za mwisho basi litakuwa jambo jema kuhusika kuisaidia timu hiyo kwa maeneo mengi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *