Diplomasia kutumika kutangaza vivutio vya utalii Tanzania

Arusha. Serikali imeanza kutumia balozi za nje  kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini, ikiwa ni mkakati wa kufikisha malengo ya kitaifa ya kuongeza makusanyo zaidi katika sekta hiyo na pato la Taifa.

Lengo la Tanzania kwa mwaka 2025 ni kuingiza Dola bilioni sita hadi Desemba, ambapo hadi sasa imekusanya zaidi ya Dola bilioni nne huku ikiwa na upungufu wa Dola bilioni mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa amesema kuwa katika kuhakikisha lengo linafikiwa wameandaa ziara maalumu kwa mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, wenye ofisi nchini waliyoiita ‘Diplomatic Safari Tour’.

“Lengo ni kuwapa fursa wataalamu hawa wa kidiplomasia kuona vivutio vilivyoko nchini kama sehemu ya kukuza mahusiano lakini nao kuwa mabalozi wa hiari wa utalii wa Tanzania katika nchi zao” amesema na kuongeza;

“Lakini pia tunalenga kukuza utalii na kuufanya kuwa uti wa mgongo wa Taifa letu, kwani kwa sasa unachangia asilimia 25 ya pato la Taifa  na tunataka ifikie angalau nusu ya makusanyo nchini yatokane na utalii, lakini pia tumeona tuna uwezo wa kutembelewa na watalii hata zaidi ya milioni saba kwa mwaka”.

Amesema kuwa ziara hiyo itakayokuwa ya kila mwaka, kwa awamu hii ya kwanza imekuwa na wajumbe 25 kutoka nchi mbalimbali huku wakiwa na lengo kutembeza mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa wote 93 walioko na wanaofanya kazi nchini Tanzania.

“Wajumbe hawa wametembelea Mbuga ya Serengeti, Ngorongoro na wataenda Zanzibar kujionea vivutio vilivyoko kule pia na tunaamini watakuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu” amesema Balozi Said Shaib Mussa.

Magari waliyopanda Mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa wenye ofisi nchini wakiwa kwenye ziara maalum ya kutembelea vivutio nchini waliyoiita ‘Diplomatic Safari Tour’, ndani ya hifadhi ya Serengeti

Wakizungumza kwenye hafla fupi ya  chakula kilichoandaliwa na Benki ya NMB kwa kushirikiana na wizara hiyo,  mabalozi hao wamesema kuwa Tanzania imebarikiwa kwa kiasi kikubwa katika utunzaji wa bioanuai hali inayostawisha asili yake ya kimazingira lakini pia wanyama pori.

Balozi wa Kenya Nchini Tanzania, Issack Njega ameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuandaa safari hiyo, ambayo amesema kuwa itakuwa ya mafanikio makubwa katika kutangaza vivutio vya Tanzania.

“Tumeona vivutio vingi katika Hifadhi ya Serengeti ambayo ndio kubwa kwa Afrika na yenye hadhi na sifa kubwa duniani kwa vivutio vya utalii hadi kupata tuzo nyingi, na sisi tumekubali kweli inastahili kwa upekee iliyonayo” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuomba Serikali ya Tanzania kuimarisha ushirikiano zaidi na Kenya katika kutangaza vivutio vyao hasa vile vinavyovuka mipaka kama Hifadhi hiyo ya Serengeti ambayo inapakana na hifadhi ya Masai Mara ya Kenya, ambapo misafara mikubwa ya nyumbu huhama kwa kupokezana.

Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Leontine Nzeyimana amesema kuwa mafanikio ya Tanzania katika utunzaji wa bioanuai imekuwa rafiki kwa wanyama na kuleta uasili wake, hivyo kuahidi kutangaza vivutio hivyo kwa wananchi wa Burundi kuja kutembelea Tanzania.

“Kwanza mimi sijawahi kufika katika hiyo mbuga ya Serengeti wala Ngorongoro na kubwa zaidi nilikuwa  naogopa kupanda hiyo puto (Baloon) lakini nilipohamasishwa na kupanda hakika nimefurahi na nitarudi tena na tena na kuwaleta wenzangu wengi”.

Amesema kuwa raia wengi wa Burundi wamekuwa wakitumia gharama kubwa kwenda nchi za Ulaya kipindi cha likizo au mapumziko yoyote ya kujipongeza kwa ajili ya kutafuta upekee, hivyo sasa itakuwa wakati mzuri kwake kuwajulisha kuwa upekee huo upo zaidi Tanzania.

“Pale Ngorongoro nimeona Watanzania walivyobarikiwa hasa baada ya kubahatika kuona wanyama wengi kwa wakati mmoja wakiwemo wale wakubwa watano (Big five), hivyo nikirudi Burundi nitawaambia wenzangu hapa ndio sehemu sahihi na sio ghali maana watatozwa bei ya mwanajumuiya wa Afrika Mashariki”

Balozi wa Comoro, Dr Ahamada El Badaoui Mohamed amesema kuwa imekuwa wakati mzuri kwake kutembelea Hifadhi ya Serengeti na Ngorongoro na kuona wanyama na vivutio vingine.

 “Mimi nimetembea nchi nyingi sana na wanyama wako kila mahali  lakini Tanzania ina upekee wa asili kuanzia bioanuai za wanyama, wadudu na mimea na zaidi nimevutiwa na mazingira asilia” amesema na kuongeza;

“Naishauri Tanzania kuhakikisha wanaongeza nguvu ya kutangaza vivutio hivi na mkifanikiwa mnaweza kuwa nchi iliyoendelea kwa kuingiza mapato mengi kwenye utalii pekee, uzuri mimi naenda kuanza kuwatangaza na naahidi wengi watakuja”.

Naye Mkuu wa kitengo cha miamala ya kibenki kutoka NMB, Linda Teggisa amesema kuwa lengo la kuwakutanisha wadau hao wakiwemo mabalozi na wakuu wa misheni za kidiplomasia, pamoja na wawakilishi wa taasisi za kimataifa ni kuwajulisha masuluhisho ya kifedha wanayotoa hasa za kidijitali na katika sekta ya utalii.

“Masuluhisho yapo mengi ambayo tumewaambia yenye mlengo wa kujenga uwezo wao wa kirasilimali hasa mitaji na mikopo kununua vifaa vya kazi kama magari na vifaa vinginevyo”.

Amesema kwa sasa wanawekeza nguvu kubwa katika kutoa huduma za kidijitali ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Mdau wa utalii, Felex Mhagama amesema kuwa hatua ya nchi kutangaza vivutio vyake kupitia ofisi za mabalozi itaiwezesha kunufaika na uchumi wa kidiplomasia hasa katika sekta ya utalii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *