Dar es Salaam. Wakati mvua iliyonyesha katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam ikisababisha adha kwa wananchi, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) leo Aprili 14, 2025 imetoa angalizo la mvua kubwa kwa siku mbili katika mikoa sita nchini.

Taarifa hiyo inakuja wakati ambapo usiku wa kuamkia leo Jumatatu, Aprili 14, 2025 mvua kubwa imenyesha Dar es Salaam na kusababisha maji kuingia kwenye makazi ya watu, huku baadhi ya wakazi wakikumbana na changamoto za usafiri kutokana na foleni.
Baadhi ya maeneo kama vile Jangwani, Mkwajuni, Posta, na Mabibo yalionekana kuzidiwa na maji, hali iliyosababisha barabara kufurika na kuwa ngumu kupitika.
TMA kupitia taarifa yake imetoa angalizo la mvua kubwa siku mbili kuanzia leo hadi kesho (sawa na saa 48) kwa katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba.
“Taarifa hiyo imeeleza kuna uwezekano wa athari za wastani, ikiwa ni pamoja na baadhi ya makazi kuzungukwa na maji.”
Kwa siku ya kesho Jumanne, Aprili 15, 2025, TMA pia imetoa angalizo la mvua kubwa kwa maeneo ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikiwemo Mafia), Morogoro, Lindi, Mtwara, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Taarifa imeeleza kuwa athari zinazoweza kujitokeza ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji.
Katika Mkoa wa Dar es Salaam, mvua ya leo pia ilisababisha uharibifu wa barabara, ikiwemo barabara ya Kimara King’ongo ambayo ilipata uharibifu mkubwa, na hivyo kusababisha usumbufu kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na ugumu wa kupitika.
Katika eneo la Gongolamboto, wakazi walilazimika kuvushwa kwenye maeneo yenye maji kwa gharama ya kati ya Sh500 hadi Sh1,000, huku wanafunzi wakitozwa Sh200.
Wakazi wa jiji hilo walionekana wakivuka kwenye karavati la reli ya treni ya umeme katika eneo la Gongolamboto, huku wengine wakibebwa kwa malipo hayo.

Hali ikiwa hivyo kwa Dar es Salaam, Aprili 6, 2025, mawasiliano ya barabara kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Kusini yalikatika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha maeneo ya Kilwa, mkoani Lindi.
Mbali na mawasiliano hayo kukatika, baadhi ya madaraja pia yalibomoka, ikiwemo Daraja la Somanga–Mtama na lile la Mto Matandu.