Walioshtakiwa kwa kusafirisha kilo 221.43 za bangi waachiwa huru

Arusha. Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imewaachia huru washtakiwa watatu walioshtakiwa kwa makosa ya kusafirisha kilo 221.43 za dawa za kulevya aina ya bangi.

Hukumu hiyo imetolewa Machi 28, 2025, na Jaji Sedekia Kisanya aliyesema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka ushiriki wao katika shtaka hilo.

Walioachiwa huru ni Rajab Seleman, Mohamed Omary na Peter Valentine waliotetewa na mawakili Michael Kibindu, Frederick Charles na Benjamin Mageni.

Jamhuri ilidai kuwa Januari 21, 2023, katika eneo la Msitu wa Ruvu Kusini, Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, washtakiwa hao walikutwa wakisafirisha dawa hizo kinyume cha sheria.

Upande wa mashtaka, ukiongozwa na jopo la mawakili watatu wa Serikali, uliita mashahidi sita kuthibitisha shtaka hilo pamoja na kuwasilisha vielelezo saba, ikiwemo pikipiki mbili walizodaiwa kukutwa nazo.

Mashahidi hao walikuwa ni Rajabu Mohamed, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Theobald Msungwi, Inspekta Joseph Cosmas, F2462 Sajenti Makwani, G420 Koplo Bonda na G1090 Koplo Faraji.

Shahidi wa pili alidai kuwa akiwa doria na wenzake, akiwemo shahidi wa tano, njiani kutoka Kisarawe kuelekea Kijiji cha Mzenga, Wilaya ya Kisarawe, alipata taarifa za kiintelijensia kutoka kwa mtoa taarifa kuhusu watu wanaoshukiwa kusafirisha vitu visivyojulikana ndani ya msitu wa Serikali wa Ruvu Kusini.

Alidai waliendelea na safari na wakiwa njiani waliona matairi ya pikipiki yakielekea msituni, wakaegesha gari kando ya barabara na kufuata nyayo hizo kwa miguu hadi msituni.

Shahidi huyo alidai kuwa walipoingia msituni, walikuta pikipiki mbili zikiwa zimeegeshwa, na vijana watatu wakiwa wamelala chini, huku zikiwa na vifurushi vilivyofungwa kwenye mifuko ya salfeti.

Alidai kuwa pikipiki ilikuwa na mabegi sita yaliyofungwa kwenye siti ya abiria na sehemu ya kubebea mizigo, huku pikipiki nyingine ikiwa na mabegi sita pia.

Alidai kuwa waliwaamsha na kuwakamata, wakajitambulisha kuwa ni maofisa wa polisi na kuwakamata kwa tuhuma za kusafirisha bangi.

Wakati wa mahojiano ya mdomo, alidai mshtakiwa wa pili (Mohamed) alikiri kumiliki pikipiki MC 695 DNU pamoja na shehena yake, na mshtakiwa wa kwanza (Rajab) alikiri kumiliki pikipiki MC 919 DFY, huku Peter (mshtakiwa wa tatu) akieleza kuwa mizigo hiyo ilikuwa ikisafirishwa kwa kaka yake huko Kibaha.

Shahidi huyo alidai kuwa baada ya kutilia shaka mizigo hiyo, walikamilisha hati ya ukamataji ikieleza vitu vilivyokamatwa kuwa ni mifuko 12 ya salfeti yenye majani makavu yanayodhaniwa kuwa ya bangi na pikipiki mbili.

Alisema kwa kuzingatia umbali wa eneo hilo na kutokuwepo mashahidi wa kujitegemea, shahidi wa tano na Konstebo Iddi walitia saini fomu hiyo kama mashahidi, kisha kuwasafirisha watuhumiwa hadi Kituo cha Polisi Kisarawe.

Shahidi wa tatu alidai kuwa Januari 23, 2023, alipangiwa kuchunguza jalada la kesi hiyo na kupeleka vielelezo kwa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) jijini Dar es Salaam kwa uchunguzi, baada ya kupimwa, iligundulika kuwa ni bangi.

Januari 26, 2023, shahidi huyo alidai kuwafikisha washtakiwa hao Mahakama ya Wilaya ya Kisarawe, ambako walisomewa shtaka la kusafirisha dawa za kulevya.

Katika utetezi wao, mshtakiwa wa kwanza alidai alikamatwa Januari 21, 2023, katika Kijiji cha Gumba akinywa pombe, huku mshtakiwa wa pili akidai alikamatwa kwa tuhuma za wizi akiwa kijiweni eneo la Homboza akiwa na wenzake Juma Said na Said Khalfan.

Mshtakiwa wa tatu alidai alikamatwa akikusanya mkaa katika msitu wa Kijiji cha Mzenga.

Mbali na hayo, kila mshtakiwa alikana umiliki wowote wa pikipiki zilizodaiwa kubeba dawa hizo za kulevya pamoja na kukana kusaini cheti cha ukamataji.

Hukumu ya Jaji

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Kisanya alisema kuwa suala kuu ni iwapo upande wa mashtaka umetekeleza wajibu wa kuthibitisha kesi hiyo pasipo shaka yoyote, kama inavyotakiwa chini ya vifungu vya 3(2) na 114(1) vya Sheria ya Ushahidi.

Alisema vifungu hivyo vinaeleza kuwa mzigo wa uthibitisho katika kesi za jinai uko kwa upande wa mashtaka pekee, ambao lazima uthibitishe hatia kwa kiwango kisicho na shaka yoyote, isipokuwa kama sheria inaeleza vinginevyo.

Jaji alisema, chini ya kifungu cha 15(1)(a) na (3)(iii) cha DCEA, kosa la usafirishaji wa dawa za kulevya linathibitishwa kwa kuonesha kuwa mtu alihusika katika shughuli kama vile uingizaji, usafirishaji, uuzaji au umiliki wa dawa hizo.

Aidha, alisema iwapo dawa zinazohusika ni bangi, kama katika kesi hii, upande wa mashtaka unapaswa kuthibitisha kuwa uzito wake unazidi kilo 100.

Kuhusu mifuko 12 ya bangi, Jaji alisema lazima Mahakama ijiridhishe kuwa mlolongo wa ulinzi wa dawa hizo ulidumishwa kuanzia wakati wa kunaswa hadi kufikishwa kwenye uchunguzi.

“Ni muhimu kubainisha kwamba suala hili lilichunguzwa na maofisa wa polisi, waliopaswa kuzingatia Kanuni za Miongozo ya Jeshi la Polisi (PGO) Na. 229, aya ya 15, inayotaka kudumishwa kwa mlolongo wa ulinzi kwa masharti yaliyowekwa,” alisema.

Jaji aliongeza kuwa upande wa mashtaka haukutoa karatasi za kuthibitisha kila hatua ya mlolongo wa ulinzi wa vielelezo hivyo.

Alisema tofauti za muda kuhusu wakati mifuko 12 ilipofungwa kama ilivyo kwenye kielelezo cha saba, na wakati ilipopokelewa na kuhamishwa Machi 3, 2023, zinaleta shaka kuhusu uhalali wa mlolongo huo.

“Suala jingine lililozua shaka ni namna ya kukabidhi kati ya shahidi wa tatu na wa nne,” alisema.

Baada ya kuchambua hoja zote, Jaji Kisanya alisema Mahakama inahitimisha kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kufikia kiwango cha uthibitisho kinachohitajika, hivyo kuwaachia huru washtakiwa waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *