Dar es Salaam. Unapohisi mpangilio ule ule wa matone ya mvua yakigonga ngozi yako, huenda usifikirie kuhusu sifa za kuvutia za mvua. Hata hivyo, mvua ni sehemu ya ajabu la dunia yetu ya asili inayoficha siri nyingi.
Kwa mujibu wa Mtandao wa FoxWeather, mvua hupitia mabadiliko mbalimbali na hufuata mifumo fulani kutoka utengenezwaji wake juu kabisa mawinguni hadi inapoanguka ardhini, mambo ambayo hayaonekani wazi.
Wakati mwingine mvua inakushangaza kwa kuwasili ghafla, jishangaze mwenyewe kwa kufahamu mambo haya 10 kuhusu tukio hili la kushangaza.

Kuelewa zaidi kuhusu mvua kutakupa uthamini wa kina kwa nguvu hii ya asili inayotoa uhai.
1. Mvua haina umbo la tone la mchozi
Ingawa inaweza kushangaza, matone ya mvua hayapo katika umbo la machozi. Yanaposhuka angani, matone ya mvua hujipatia umbo tambarare la duara lililobanwa kwa sababu ya upinzani wa hewa.
Ukubwa wa matone ya mvua hutofautiana kulingana na mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na unyevunyevu, halijoto na kasi ya upepo wa juu.
Kwa wastani, matone ya mvua huwa na kipenyo cha milimita moja hadi sita. Hata hivyo, baadhi ya matone yanaweza kufikia hadi milimita nane, karibu na ukubwa wa kiduara kidogo cha glasi. Kadri tone la mvua linavyokuwa kubwa, ndivyo linavyoshuka kwa kasi zaidi kutokana na uzito wake mkubwa.

Hata hivyo, hata tone kubwa zaidi la mvua halishuki kwa kasi ya kuweza kusababisha madhara. Idadi ya matone ya mvua yanayoshuka katika dhoruba moja ni ya kushangaza.
Dhoruba ya mvua ya inchi moja huzidondosha takriban galoni milioni 6 za maji katika ekari moja ya ardhi. Kwa kuwa wastani wa tone la mvua lina ujazo wa mililita 0.05, hiyo inamaanisha kuna takriban matone bilioni 120 ya mvua katika ekari moja.
2. Ina harufu ya kipekee
Mvua ina harufu ya kipekee inayotokana na vyanzo mbalimbali. Inapoanguka kupitia anga, huchukua kemikali na gesi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ‘petrichor’ mafuta yanayozalishwa na mimea ambayo hutoa harufu safi na ya udongo mvua inapoanza kunyesha.

Harufu ya petrichor hutoka kwa mimea mbalimbali na hukusanyika kwenye mawe, udongo na maeneo mengine wakati wa hali ya ukame. Mvua inaponyesha, mafuta haya hutolewa hewani na kusababisha harufu ile inayotambulika wakati wa mvua.
Utafiti unaonyesha kuwa wastani wa mkusanyiko wa geosmin kwenye maji ya mvua ni takriban nanogramu 0.2 hadi 2 kwa lita.
Bakteria walioko kwenye udongo na mimea hutoa gesi zenye harufu wakati mvua inaponyesha na unyevunyevu unapoongezeka.
3. Kuna sehemu duniani ambayo haijawahi kuona mvua
Jangwa la Atacama lililoko kaskazini mwa Chile na kusini mwa Peru ndilo eneo kame zaidi duniani kulingana na uchunguzi wa hali ya hewa. Linapokea wastani wa inchi 0.019 (sawa na milimita 0.5) za mvua kwa mwaka, kwa mujibu wa rekodi za Guinness World Records. NASA inasema ni jangwa lisilo la baridi kali, kavu zaidi duniani.
4. Inachukua takriban dakika mbili kwa tone la mvua kufika ardhini
Ingawa urefu ambao matone ya mvua hutoka mawinguni hutofautiana, huanguka kuelekea ardhini kwa kasi ya wastani ya maili 14 kwa saa, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Met Office ya Uingereza.

Ilikadiria kuwa mawingu yako katika urefu wa futi 2,500, hiyo inamaanisha kwa mujibu wa takwimu, tone la mvua litachukua zaidi ya dakika mbili kufika chini.
Met Office pia ilibainisha kuwa matone makubwa ya mvua yanaweza kuanguka kwa kasi ya hadi maili 20 kwa saa, wakati madogo kabisa yanaweza kuchukua hadi dakika saba kufika ardhini.
5. Mvua haifiki kila wakati ardhini
Wakati mvua inapotoka mawinguni, kawaida hufika ardhini na hukulowesha ikiwa hukujitayarisha kwa mwavuli.
Lakini ikiwa hewa ni kavu sana, matone ya mvua yanaweza kuyeyuka kabla hayajafika ardhini, kwa hiyo kwa hali halisi ya hewa, itaonekana tu kuwa na mawingu.
Matone ya mvua yanayoyeyuka kabla ya kufika ardhini huitwa ‘virga.’
6. Mahali penye mvua ndogo zaidi duniani sio jangwa
Huenda pamefunikwa na barafu, lakini Antaktika hupokea wastani wa inchi 6.5 za mvua au theluji kwa mwaka na kuifanya kuwa bara lenye mvua chache zaidi duniani.

Kwa upande mwingine, Lloro, Colombia, hupokea zaidi ya inchi 500 za mvua kwa mwaka. Amerika Kaskazini ni kavu zaidi kwa kulinganisha, ikipokea inchi 256 kwa mwaka.
7. Sio matone yote ya mvua yanayotengenezwa kwa maji
Kwenye sayari kama Zuhura (Venus) na miezi au sayari nyingine, mvua huundwa na asidi ya sulfuriki au methane. Cha kushangaza zaidi, kwenye sayari iliyo miaka ya mwangaza 5,000 kutoka duniani, wanasayansi waligundua mvua inayodondoka ikiwa na madini ya chuma badala ya maji.
8. Umbo na rangi ya mawingu yanaweza kusaidia kutabiri mvua
Kwa jumla, ukiona wingu la lenye umbo la mnara na kilele kilicho bapa au wingu jeupe linaloelea chini na lenye rangi ya kijivu, unaweza kuwa na uhakika kuwa mvua inakuja ndani ya saa 24.
9. Rekodi ya mvua nyingi ndani ya saa 24 ilivunjwa Marekani
Julai mwaka 1979 dhoruba ya Kitropiki ‘Claudette’ ilinyesha inchi 43 za mvua katika mji mdogo wa Alvin, Texas. Alvin ulikuwa na rekodi hiyo hadi Aprili 2018, mita ya mvua huko Hanalei, Hawaii, ilirekodi inchi 49.69 za mvua kwa siku moja.
10. Mvua ni pesa
Katika nchi ya Afrika ya Botswana, fedha ya taifa inaitwa Pula. Neno ‘Pula’ linamaanisha mvua na matumizi yake kama jina la fedha yanaonyesha jinsi mvua ilivyo ya thamani katika nchi hii ya jangwa.