Unaikimbuka TP Mazembe ile ya kuanzia mwaka 2014 hadi 2016? Ndiyo, Kocha wa sasa wa Yanga Miloud Hamdi alikufa na USM Alger yake katika mechi zote mbili za fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2015.
Mazembe hiyo iliyokuwa na rundo la mastaa waliotamaniwa na kila timu Afrika lakini hawakuweza kuchukuliwa.
Kulikuwa na wengi wanaovutia kuwatazama wakiwa na mpira mguuni kama Rainford Kalaba, lakini sisi Watanzania macho na masikio yetu yalikuwa kwa watoto wetu, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
Kwa wakati huo hakuna kitu ambacho ungewaambia mashabiki wa TP Mazembe kuhusu vijana hawa wakakuelewa. Walitunzwa kama mboni ya jicho, unaweza kusema walikuwa miongoni mwa wachezaji pendwa katika timu. Sio kwao tu hata kwetu, Ulimwengu na Samatta ndio walikuwa taswira hali ya timu ya taifa.

Mpira uliwafanya kuwa mapacha wa nje. Kila mara vigogo wa Afrika walipokuwa wanabisha hodi kutaka huduma zao, bosi wa Mazembe, Moses Katumbi alitupilia mbali maombi yao.
Hadi wakati huu, hadithi ya Samatta na ulimwengu zilikuwa zinafanana na kitabu chao kilikuwa kimoja, lakini mambo yalipinduka baada ya kufika muda wa kukua na kupanua mbawa zaidi.

Samatta alilazimika kwenda Ubelgiji kujiunga na KRC Genk Januari, 2016 akimwacha Ulimwengu ambaye alilazimika kusubiri hadi 2017 Julai kabla ya kwenda Sweden kuitumikia AFC Eskilstuna.
Hapo ndio ilikuwa mwisho wa hadithi zao kufanana, kila mmoja alishika njia yake lakini njia ya ulimwengu ilikuwa na miba sana, tangu hapo hakuwahi kurudi kule alipokuwepo zamani, kuwa mchezaji wa kutumainiwa, majeraha yalikuwa sehemu ya maisha yake, Sweden alikaa kwa miezi tisa, akatimkia Bonsia ambako alikaa kwa muda mfupi sana usiozidi hata mwezi mmoja, mwishowe akarudi katika ardhi mama ya Afrika, akicheza Al-Hilal ya Sudan, JS Soura na Algeria, Mazembe mwisho Singida na sasa hana timu kabisa.

Hadithi ya Samatta ilikuwa ya kuvutia, alifanya maajabu akiwa na Genk, akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ubelgiji na kuchukua taji la ligi hiyo, akafunga bao katika Ligi ya Mabinga kwenye dimba la Anfield dhidi ya Liverpool, akatua England, akacheza fainali ya Carabao akiwa ndio mchezaji wa kwanza wa Tanzania kufanya hivyo.
Lakini naye hadithi yake imekuwa tofauti, wakati anasajiliwa Genk, miongoni mwa wachezaji wa kigeni aliowakuta alikuwa ni Leon Bailey, dogo kutoka Jamaica ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa akisaidiana naye sana kiwanjani.
Yeye na staa huyu walionekana kama mhimili wa timu, taswira ya Genk ilionekana katika miguu yao, Bailey hakuwa anafunga sana lakini alihakikisha Samatta anapata huduma stahiki, kiasi cha kuwa mfungaji bora kwa kutupia mabao 20 katika msimu wa 2018/19.

Hivi sasa Samatta yupo kule Ugiriki, chati ya mtandao unaohifadhi taarifa za wachezaji wa Transfermakert imeshuka sana ni kama anaanza upya, lakini ni hadithi yake tu ndivyo ilivyoandikwa.
Wakati Samatta anaweka rekodi mbalimbali na kuandika hadithi zake England, Bailey alikuwa bize kujenga jina lake Bayer Leverkusen, wakati huu ambao Samatta anapata tabu katika kikosi cha PAOK, Bailey ni mchezaji tegemeo ndani ya Aston Villa bora ya Unai Emery.
Bailey ni mmoja kati ya mastaa ambao timu kubwa ikigonga hodi kutaka saini yake haitokuwa rahisi kwa Villa kumwachia kutokana na umuhimu wake na huenda hata akiachiwa basi itakuwa kwa pesa nyingi.
Hadithi yake imepisha na ile ya Samatta kama ilivyo ile Samatta na ulimwengu.
Bailey kwa sasa anacheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, ni jambo ambalo mashabiki wengi tulitamani kuona likitokea kwa Samatta lakini hadithi ndio hivyo, zimekuwa tofauti, walifanya makubwa wakiwa Genk, mmoja ameendelea kufanya hivyo lakini mwingine amelazimika kuwa na stori tofauti ni sawa na ilivyokuwa kwa Ulimwengu, akiwa na Samatta, Mazembe walifanya makubwa sana lakini sasa mambo yamekuwa tofauti, mmoja tupo naye katika ardhi hii tukufu, mwingine anaendelea kukimbiza upepo katika uso wa dunia kule Ugiriki.