
MSHAMBULIAJI wa Trident FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Zambia, Mourice Sichone amesema tayari ameanza kupokea ofa kutoka Ligi Kuu nchini humo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sichone alisema huenda akaondoka kikosini hapo mwishoni mwa msimu huu kama atakubaliana na ofa alizopata.
Aliongeza, kiwango bora alichoonyesha kwenye msimu wake wa kwanza kikosini hapo kimemfanya aitwe kwenye kikosi cha timu ya taifa U-20 ‘Ngorongoro Heroes’ kinachojiandaa na mashindano ya AFCON nchini Misri.
“Kwanza napenda kuwapongeza Mwanaspoti kwa kazi kubwa mmenisapoti sana nimeitwa timu ya taifa ya vijana sababu ya kuniandika ninachokifanya Zambia,” alisema Sichone na kuongeza;
“Ni kweli kama ulivyosema kuna timu kama tatu za Ligi Kuu Zambia zimenitafuta, bado sijafikia maamuzi, naangalia penye ofa nono ndipo nisaini.”
Katika mechi 18 alizocheza kinda huyo amefunga mabao sita na asisti nane akiingia kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja.