
BAADA ya kuizamisha Mbeya City katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la ndani, Simba kwa sasa inaingia kwenye maandalizi ya kuikabili Stellenbosch ya Afrika Kusini katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku mabeki wakongwe wa pembeni wakiachwa msala.
Mabeki hao ni nahodha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ a.k.a Zimbwe Jr. na Shomary Kapombe ambao ndio wachezaji wazoefu wa mechi hizo za kimataifa katika kikosi cha sasa kinachonolewa na kocha Fadlu Davids aliyeifikisha timu katika nusu fainali ya Afrika kwa mara ya kwanza tangu iliporudi kimataifa 2018-2019.
Straika wa zamani wa timu hiyo, Mzambia Moses Phiri anayekipiga kwa sasa Nkana FC iliyopo Ligi Kuu ya Zambia, ndiye aliyesema hayo juu ya wachezaji hao kubeba msalaba wa kuivusha Simba ili kwenda fainali ikiwa ni mara ya kwanza tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwaka 2004.
Phiri, aliliambia Mwanaspoti kuwa, Kapombe na Tshabalala wana nafasi kubwa ya kuivusha klabu hiyo hadi fainali za Kombe la Shirikisho Afrika, kwa uzoefu walionao wa mechi hizo na namna wanavyoweza kuwahamasisha wachezaji wenzao ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi.
Phiri alisema anajua Kapombe yupo Simba kwa muda mrefu tangu alipoanza kuitumikia klabu hiyo msimu wa 2011-13 kisha kurudi tena tangu 2017-2025 wakati Tshabalala ameitumikia timu hiyo tangu 2014 hivyo kuwa waandamizi na ni rahisi kusikilizwa na wachezaji wengine na hata mashabiki katika hamasa za kupambania timu kutinga nusu fainali za michuano hiyo.
“Kapombe na Tshabalala ni viongozi dhidi ya wengine, hivyo wakizungumza jambo wanasikilizwa kwa urahisi, hivyo ni wakati wao wa kujitoa kwa nguvu zote na kuwajenga wachezaji wenzao wawe wazalendo wa kuipambania timu hiyo kuandika historia mpya Afrika,” alisema Phiri na kuongeza;
“Mbali na uongozi walionao wachezaji hao, wana uwezo mkubwa wa kumua mechi kama alivyofanya Kapombe kupiga penalti ya kuivusha Simba kwenda nusu fainali za michuano hiyo.”
Phiri aliitumikia Simba kwa msimu mmoja na nusu akifunga mabao 10 ya ligi msimu wa 2022-23 na mengine matatu msimu uliofuata kabla hajaondoka Januari 2024 kurudi Zambia, alipendwa na mashabiki wa timu hiyo ambayo pia aliifungia mabao kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Alifunga mabao mawili wakati wakiichapa Nyasa Big Bulltes ya Malawi kwa mabao 2-0 ikiwa kwao na ziliporudiana Dar es Salaam alifunga bao jingine katika ushindi mwingine wa 2-0, na pia alifunga bao moja wakati wakiifunga 1st do Agosto ya Angola 1-0 ugenini na kuongeza jingine katika ushindi 3-1 nyumbani KWa Mkapa.
“Nina uzoefu wa michuano ya CAF na niliona namna ambavyo Kapombe na Tshabalala wakati huo sambamba na John Bocco walikuwa wahamasishaji wazuri sana dhidi ya wengine kupambania timu kufika mbali katika michuano hiyo,” alisema Phiri. (Bocco kwa sasa anakipiga JKT Tanzania).
Kuhusu mechi hiyo kwa upande wa Tshabalala alisema anatamani kufanya vizuri zaidi na kuandika historia ya kuivusha timu hadi fainali si tu kwa heshima kwa klabu bali hata kwake kama nahodha.
Tshabalala alisema anatamani uwe mwaka wa kuandika historia itakayofanya waje kukumbukwa na wachezaji wengine watakaokuja nyuma yao.
“Ni hamu ya kila mchezaji kutinga fainali ili kuandikwa katika vitabu vya rekodi ya kutolewa mfano na wachezaji ambao watafuata nyuma yetu, tunajua ni hatua ngumu ila tutapambana kadri tuwezavyo,” alisema Tshabalala aliyetua Msimbazi akitokea Kagera Sugar 2014 na kudumu hadi leo hii.
Simba itaanza mechi hizo za nusu fainali kwa kuikaribisha Stellenbosch ya Afrika Kusini Jumapili ya Aprili 20, kisha kurudiana nayo wiki moja baadaye jijini Cape Town, Afrika Kusini na mshindi wa jumla atatinga fainali na kuvaana na mshindi kati ya RS Berkane ya Morocco au CS Constantine ya Algeria.
Tshabalala alisema kukutana na Stellenbosch anaona itakuwa nafuu kwao kwa vile kocha Fadlu anatokea nchini humo na hivyo kujua namna ya kutumia mbinu zitakazowavusha kwenda fainali.
Stellenbosch inayoshiriki michuano hiyo ya CAF kwa mara ya kwanza, imepenya hapo kwa kuivua taji na kuing’oa Zamalek ya Misri kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0, huku Simba ikiitoa Al Masry pia ya Misri kwa mikwaju ya pebnalti 4-1 baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2 kila moja ikishinda nyumbani 2-0.